
Askofu Josephat Gwajima.
Maaskofu na Wachungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima
linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima (pichani), waliokamatwa na
Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kutaka kumtorosha kiongozi huyo, kutoka
hospitali ya TMJ, wanatarajia kufungua kesi mahakamani.
Wafuasi hao wapatao 15 waliokamatwa na Jeshi la Polisi Machi 29,
mwaka huu usiku wakituhumiwa kutaka kumtorosha Askofu Gwajima
wanatarajia kufungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Jeshi la Polisi.
Wakili wa utetezi wa Askofu Gwajima na Kanisa la Ufufuo na Uzima,
Peter Kibatala, alisema jana kuwa wachungaji na viongozi hao
waandamizi wamepanga kufungua kesi kulalamikia namna walivyotendewa na
Jeshi la Polisi walipokamatwa.
Alisema wamepanga kufungua kesi hiyo kuanzia leo kwa lengo la kudai haki ya kuonewa kwa watumishi hao. Kibatala alieleza kuwa mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa
na Kamanada wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
ulikuwa na mahudhui ya kuwahukumu viongozi hao waandamizi kama wahalifu
wakati walikuwa hawakuwa wameshtakiwa na chombo chochote.
“Press conference (mkutano wa waandishi wa habari) unapaswa
kuendeshwa kwa namna ambayo haimhukumu mtu moja kwa moja, lakini Kamanda
Kova aliendesha mkutano ule kwa kuwahukumu moja kwa moja,” alisema
Kibatala.
Madai mengine ni wafuasi hao kukaa polisi muda mrefu kuliko muda uliowekwa na sheria bila kufikishwa mahakamani. Lingine ni miongoni wa Maaskofu na wachungaji hao, wawili waliteswa na maofisa wawili wa Jeshi la Polisi wakati wanahojiwa. Alisema kutokana na mambo hayo matatu, viongozi hao wanalalamika kuwa yamevunja haki yao ya kikatiba.
Aliongeza kuwa hata barua aliyowaandikia Jeshi la Polisi juzi
kutaka Askofu Gwajima kutofika kituo cha polisi hadi pale watakapopata
nyaraka ya kisheri kutoka kwa Jeshi hilo, pia ilielezea matarajio ya
kufungua kesi mahakamani juu ya malalamiko ya viongozi hao.
Kibatala alivitaja vitu walivyorudishiwa viongozi hao ni pamoja na
magari matatu pamoja na vifaa vya matangazo walivyonyang’anywa na Jeshi
la polisi. “Kwa hiyo leo (jana) wafuasi hao wameambiwa wasiende kuripoti
polisi hadi pale watakapotaarifiwa na Jeshi la Polisi,” alisema
Kibatala.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment