Social Icons

Pages

Friday, April 17, 2015

WAKINA GUNINITA 'WAMTIA' DC MAKONDA KORTINI


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ametakiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kuwasilisha utetezi dhidi ya madai ya makada wawili wa CCM, John Guninita na Mgana Msindai kuwa aliwadhalilisha kwa kuwaita vibaraka wanaotumiwa kuharibu chama hicho kwa nguvu ya pesa.
Katika kesi hiyo ya madai Namba 68/2015,makada hao wawili wanataka walipwe fidia ya Sh100 milioni kila mmoja, Makonda awaombe radhi na mahakama itoe zuio la kudumu kwa kiongozi huyo wa Serikali kuwazungumzia.
Awali, Guninita, ambaye alikuwa mwenyeviti wa wa chama hicho mkoani Dar es Salaam, na Msindai ambaye ni mwenyekiti wa CCM mkoani Singida, walimtaka Makonda kuwaomba radhi kwa kutoa maneno ambayo walidai yanawadhalilisha, na kwamba asingefanya hivyo wangemfikisha mahakamani.
Mahakama ilikuwa imemtaka Makonda, ambaye anawakilishwa na Lusiu Peter, kuwasilisha utetezi wake leo lakini wakili huyo aliomba muda zaidi ili aandae majibu ya tuhuma hizo.
Kutokana na maombi ya wakili huyo wa Makonda, Hakimu Mkazi wa Kisutu, Hellen Liwa, anayeisikiliza kesi hiyo ya madai, alimtaka mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni kuwasilisha utetezi wake ifikapo Aprili 23 na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 27 wakati itakapotajwa. Katika kesi hiyo, Msindai na Guninita wanaiomba mahakama hiyo kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja Sh100 milioni.
Msindai na Guninita wanadai kuwa Makonda aliwadhalilisha wakati akiwa katibu wa uhamasishaji chipukizi wa UVCCM kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwaelezea makada hao kuwa ni vibaraka wanaotumiwa kuiharibu CCM kutokana na nguvu ya pesa.
CHANZO: MWANANCHI

No comments: