
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein amewaongoza
wananchi mbalimbali katika dua ya kisomo cha hitma cha kumuombea rais wa
kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Aman Karume aliyefariki Aprili 7, mwaka
1972.
Kisomo hicho cha dua kiliongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Alhad Mussa Salum, kilihudhuriwa na watu mbalimbali wa ndani na
nje ya Zanzibar wakiwamo viongozi wa serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kilifanyika katika ofisi kuu za CCM Kisiwandui
mjini hapa.
Baada ya kisomo hicho, Sheikh Mussa aliwapongeza viongozi wa
Zanzibar kwa kufanikisha kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo
imejenga maelewano miongoni mwa viongozi na wananchi. Alisema kuwa Zanzibar ya sasa siyo Zanzibar ya miaka iliyopita
ambapo amani ilipotea na kutokuwepo kwa maelewano miongoni mwao kutokana
na mambo ya kisiasa.
“Hilo ndilo jambo la kujivunia kuwa na amani katika nchi na
viongozi wanadhamana kubwa ya kuilinda amani isitoweke kwani hata siku
ya ufufuo mbele ya Mwenyezi Mungu utaulizwa jinsi mambo mema
uliyoyafanya ikiwamo amani huko huendi kuulizwa chama kama wewe ulikuwa
CUF, CCM au Chadema,” alisema Mussa.
Aidha, alimpongeza rais wa kwanza wa Zanzibar Mzee Karume kutokana
na mchango wake mkubwa wa kuwaunganisha Wazanzibari kuwa kitu kimoja
bila ya kujali dini, rangi au kabila.
Baadhi ya watu waliozungumza na NIPASHE jana walisema Mzee Karume
ni kiongozi wa kupigiwa mfano kutokana na mchango wake mkubwa wa
kimaendeleo. Askofu wa kanisa la Anglikana Zanzibar, Michael Hafidh,
alisema Karume ameacha mambo mengi mazuri katika kuwaletea maendeleo
Wazanzibar bila ya kujali dini.
Alisema misingi hiyo ya Karume katika kudumisha umoja miongoni mwa
waislamu na wakiristo inapaswa kuendelezwa kwani misingi mema ya
kiongozi huyo.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment