
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda.
Tukio la kujiua kwa askari Polisi wa kituo cha
polisi Sikonge, mkoani Tabora, mwenye namba H 3416 PC Charles Mkoyi
(27), limechukua sura mpya, baada ya ndugu kueleza utata wa majeraha
aliyonayo ndugu yao na malalamiko yaliyoelezwa na marehemu siku chache
kabla ya kukutwa na umauti.
Wakizungumza jana na NIPASHE, wanandugu hao ambao hawakutaka kutaja
majina yao gazetini, walidai kuwa kabla ya kifo chake kijana huyo
alilalamika kunyanyaswa na mmoja wa viongozi wa kituo hicho (jina
limehifadhiwa), ambaye aliwaeleza ndugu zake kuwa manyanyaso yalikuwapo
tangu alipoingia kazini.
“Mtoto wetu ni muwazi kila linalotokea alimweleza mama yake,
anamshauri kwa kumwambia tulia tunafanya utaratibu wa kukuhamisha, tuna
jiuliza katoa wapi ujasiri wa kujiua?” alihoji na kuongeza: “Baadhi ya malalamiko aliyotueleza ni kupangwa zamu zisizo na
mpangilio, kwa mfano, anakesha kazini badala ya kupumzika anatakiwa
kurudi tena kazini...muda mwingi alikuwa anachoka sana na hata
alipolalamika hakuwahi kusikilizwa na kiongozi huyo.”
Alisema utata unaanza Kituo cha Polisi alichodaiwa alijipiga risasi
kwa kuwa alitolewa haraka na kupelekwa Hospitali ya Mkoa, huku picha
zilizopigwa kwa ajili ya kuonyeshwa familia na upelelezi, zikionyesha
amekaa kwenye kiti akiwa amekumbatia silaha.
“Tunavyofahamu eneo lolote lenye tukio la mauaji kama hayo, mtu
haruhusiwi kufika wala kusafishwa hadi zipigwe picha na hata ndugu
waone, lakini inaonekana walimnyanyua na kumkalisha kwenye kiti na
kumpiga picha, kwa muda mfupi palisafishwa na mwili ukapelekwa Hospitali
ya Mkoa. Tunajiuliza haraka hiyo ya nini?” alihoji.
Walisema mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha matatu ambayo ni
shingoni kwa nyuma kukiwa na tundu dogo, chini ya kidevu kuna jeraha
kubwa, juu ya jicho alikuwa na mchubuko. Alisema kinachozua utata zaidi ni jinsi Charles alivyojipiga risasi
kwa kuwa inaonyesha risasi iliingilia nyuma na kutokea mbele ambako
kulikuwa na mfumuko mkubwa na nyuma tundu dogo, jambo ambalo lina shaka
kwa kuwa kwa uelewa wa kawaida anawezaje kujipiga risasi kisogoni.
Ndugu hao walidai baada ya kufika kwenye kituo hicho, walionyeshwa
barua mbili zilizoandikwa na askari huyo, moja ikiwa ya kikazi na
nyingine ya familia na kwamba walisomewa kiasi ya familia na ya kikazi
haikusomwa na hawakupewa. “Hata kama wamezichukua kwa ajili ya upelelezi, lakini kwa nini barua moja ya kikazi iwe siri kwa tukio tata kama hili wanachotueleza ndugu yetu alikataa lindo lakini iweje akatae wakati
alikuwa amekwenda kazini siku hiyo?” alihoji mmoja wa wanandugu.
Alisema hadi sasa ndugu hawajapewa simu yake ya kiganjani, vitu
vyake vingine alivyokuwa navyo, nguo zake na vitu vingine vilivyokuwa
kwenye chumba chake na kwamba utaratibu wa kumzika haukuwa wa kuridhisha
na walifanya haraka haraka, jambo ambalo linawafanya wahoji uharaka
ulisababishwa na nini.
“Tunajua mwili wa askari unaposafirishwa wanabeba na vitu vyake
vyote, wanajua alikuwa hajaoa, hana ndugu, wameacha vitu vyake vyote,
kesho tunavunja matanga ndiyo siku ya kugawana nguo za marehemu, kwa
mazingira haya tutagawana nini?” alihoji.
Walisema taarifa ya daktari inaeleza kuwa askari huyo alifariki dunia kutokana na matatizo kwenye ubongo. Walielezwa kuwa kabla ya kukutwa na mauti majira ya jioni, Charles
aliitwa kwenye kikao na baada ya kutoka alilia kutwa nzima na hata
alipokwenda nyumbani na kubembelezwa na mpenzi wake, hakunyamaza na
ilipofika jioni alirudi kazini na baadaye walielezwa uamuzi aliochukua.
Waliongeza kuwa hakukuwa na ukaribu wa polisi katika mazishi, alikuwa askari mwenzao lakini alizikwa kama raia wa kawaida. Askari huyo alizikwa Aprili 5, mwaka huu katika makaburi ya
Makuyuni, Manispaa ya Dodoma, aliajiriwa wilayani Sikonge, Julai, mwaka
2013, baada ya kuhitimu mafunzo katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi
(MPA).
Alisema walionana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Suzana
Kaganda, na kumueleza malalamiko yote na kuahidi kuyafanyia kazi. Kamanda Kaganda akiongea na NIPASHE kwa njia ya simu, alisema ndani
ya Jeshi la Polisi kuna utaratibu wa kufikisha malalamiko yoyote
yanayohusu askari wao.
“Waambie hao ndugu waje kuniona badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari,” alisema Kamanda Kaganda. Askari huyo anadaiwa kujipiga risasi Aprili 4, mwaka huu, ndani ya
Kituo cha Polisi Sikonge na ilielezwa kuwa marehemu hakuacha ujumbe
wowote wa sababu za kujiua.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment