
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba amebainisha sababu nne zinazowafanya wananchi wampendekeze
kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. Nchemba aliyasema hayo
jana kwenye mahojiano wakati wa kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na
ITV kuhusu tafiti zinazofanywa juu ya kukubalika kwa baadhi ya watia nia
ya urais miongoni mwa wananchi wanaomtaja.
“Nisingependa kuwa refarii na mchezaji kwa wakati
mmoja katika hili. Kuna ripoti iliwahi kuonyesha kuwa ninaongoza katika
mbio hizo kwa kupata asilimia 37 na nyingine ikasema nimeshika nafasi ya
pili. Ninawashukuru wananchi wanaoona kuwa nafaa katika nafasi hiyo.”
Aliongeza: “Wanaonipigia kura wanaona nidhamu
katika usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, matumizi. Pia mabadiliko ya
kukomesha ufanyaji kazi wa mazoea.”
Tangu ateuliwe kushika wadhifa wa Unaibu Waziri,
Nchemba alisema amefanya mabadiliko kadhaa ambayo yamesaidia kudhibiti
matumizi ya Serikali, ikiwamo kupitisha malipo ya wafanyakazi wote wa
serikali katika akaunti zao za benki. Sambamba na hilo aliagiza wakuu wa
idara wote kuhakiki taarifa za watumishi walionao katika ofisi zao
jambo lililochangia kuokoa zaidi ya Sh400 milioni zilizokuwa zinalipwa
kwa waajiriwa hewa.
Pamoja na hayo alisema kuwa, kwa sasa amejikita zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya unaibu waziri.
Alipoulizwa anachukuliaje kufananishwa na
aliyewahi kuwa waziri mkuu katika utawala wa awamu ya kwanza, Edward
Sokoine, alijibu kuwa hiyo ni ishara nzuri kwani kiongozi huyo alitukuka
katika utumishi wa umma. “Hilo linanifanya nitende kulingana na mahitaji ya
wananchi. Uongozi wa Sokoine ulipendwa na wengi na kufananishwa na
kiongozi aliyetukuka kama yeye ni sifa nzuri inayoniongezea ari,”
alisema.
Kuhusu kuvaa viatu vyake, Sokoine alibainisha kuwa hilo bado kwani nafasi anayohudumu hailingani na ile aliyokuwa nayo Sokoine.
Akizungumzia mtindo wake wa kuvaa skafu ya bendera
ya Taifa alisema, anatazamia kuwa baada ya muda mfupi itakuwa ni
utambulisho wa taifa kwa kila Mtanzania atakayeenda nje ya nchi. “Nilianza kuvaa skafu tangu nikiwa
sekondari…wakati huo zenye rangi za bendera ya taifa hazikuwa nyingi
lakini kadri siku zinavyosogea zinaongezeka.
Viongozi wakubwa Afrika walikuwa na mavazi
yaliyowatambulisha,” alisema akitolea mfano marais Keneth Kaunda wa
Zambia na Kwame Nkurumah wa Ghana.
Akifafanua kuhusu mpango wa Serikali kuongeza
mapato na migomo ya wafanyabiashara ya mara kwa mara inayoendelea
alisema kuwa inachafua sifa nzuri ya Taifa. “Angalia athari wanazozipata wafanyabiashara kutoka Rwanda,
Kenya, Uganda, DRC, Malawi, Zambia na Zimbabwe wanaokuja kufuata mali
kutoka Soko Kuu la Kariakoo halafu wanakuta limefungwa,” alisema.
Hata hivyo alisema, wafanyabiashara ndiyo
wanaoathirika zaidi kwani bila kujali kilichofanyika bado wanatakiwa
kulipa kodi na gharama nyingine za uendeshaji kwa mwaka mzima.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment