
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe.
Jamii wilayani Serengeti imetakiwa kuachana na tabia
ya kuwakeketa watoto wa kike kwani kufanya hivyo kunawaharibia maumbile
yao ya kiasili na kuwapotezea thamani kwenye tendo la ndoa.
Akizungumza katika kituo cha kuwahifadhi wasichana waliotoroka
kukeketwa toka kwa wazazi wao, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Steven Kebwe (pichani), alisema kitendo cha kumkeketa mtoto wa kike
huharibu umbile la kiungo chake na kupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Alisema kitendo cha baadhi ya wazazi kuwaozesha watoto wa kike
wakiwa na umri mdogo, hakiwezi kuvumiliwa na serikali, hivyo kutoa agizo
kwa viongozi kuwashughulikia kisheria wale watakaobainika kufanya
hivyo.
Wasichana hao kwa sasa wamehifadhiwa katika kituo kilichopo Wilaya
ya Serengeti na kusimamiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mara.
Dk. Kebwe ambaye pia ni Mbunge wa Serengeti, alisema kitendo cha
ukeketaji ni ukatili wa kijinsia ambao hauwezi kuvumiliwa na wakunga
wanaoendekeza mila na desturi hiyo potofu, watashughulikiwa.
Alisema suala la kuwaozesha wasichana wadogo ni sehemu ya ukatili
kwa sababu hawana viungo vya asili ambavyo havina uwezo wa kuhimili
tendo la ndoa ipasavyo hasa anapopata ujauzito. “Serikali haiwezi kuvumilia vitendo hivyo viendelee kwa mtoto wa
kike, ni ukatili wa hali ya juu kumkeketa mwanamke kwani unaharibu
umbile lake la asili hasa kuwapa shida pale wanapoolewa wakiwa na umri
mdogo wanashindwa kufaidi mapenzi zaidi ya kupata maumivu,” alisema.
Kutokana na kanisa hilo kuwahifadhi wasichana hao waliogoma
kukeketwa, Dk. Kebwe alikabidhi baiskeli 48 zenye thamani ya Sh. milioni
7.2 kwa lengo la kuielimisha jamii kuachana na vitendo vya ukeketaji na
uozeshaji wasichana walio na umri mdogo. Naye Mratibu wa mpango wa ‘Serengeti tunaweza bila ukatili wa
kijinsia na maambukizi ya virusi vya Ukimwi’, Rhobi Samwel, alishukuru
kwa msaada huo ambao utasaidia wasichana 34 wanaotunzwa na kituo hicho.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment