Social Icons

Pages

Friday, April 10, 2015

MEMBE KUSHAWISHI TAASISI KUKATAA MIKATABA YA EPA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe amepanga kuzishawishi taasisi zinazohusika na uridhiaji wa Mikataba ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Jumuiya ya Ulaya (Epa), kuangalia masilahi ya nchi kabla ya kuikubali kwa kuwa inanyonya.
Membe alisema jana katika Mkutano wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na watumishi wa wizara yake.
Alisema atazungumza na wizara na Kamati ya Viwanda na Biashara kuhusu madhara ya mikataba hiyo kwa mustakabari wa uchumi wa nchi.
“Tutaenda kuielimisha kamati inayohusika na masuala ya Epa na hatari ilizobeba. Hii mikataba inatunyonya na kutushusha chini na kutuacha palepale. Inabidi tumwambie Spika Anne Makinda wakati suala hili litakapowasilishwa bungeni ni lazima tuangalie mustakabari wa taifa,” alisema Membe.
Alisema tangu mikataba hiyo iliposainiwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Oktoba mwaka jana, hajawahi kuiona na hajui kilichozungumzwa kwenye mikataba hiyo.
Rais Mkapa alisema licha ya kwamba EAC ilishasaini, kuna fursa ya kurekebisha vipengele vya kinyonyaji vilivyopo katika mikataba hiyo.
“Kutiwa saini mikataba hiyo siyo kwamba kila kitu kimeisha. Kuna mambo yanaweza kufanyika yakiwamo kubainisha maeneo yote ya kinyonyaji na kutafuta njia stahiki zitakazorekebisha kidogo ili iwe na masilahi,” alisema Rais Mkapa.
Mkapa aliyewasilisha mada ya namna nchi inavyoweza kutumia diplomasia kukuza uchumi, alisema vipengele kama kuachiana wazi masoko na usawa katika biashara baina ya nchi za Ulaya na Afrika, vitazidi kuzinyonya nchi maskini badala ya kukuza uchumi.
Alisema Nigeria walishakubaliana kuwa hata kama atapita Rais wa chama tawala au upinzani hawataridhia mikataba hiyo kwa kuwa wananyonywa katika kodi za uuzaji na uingizaji wa bidhaa.
Iwapo itapitishwa, Rais Mkapa alisema kampuni za biashara kutoka Ulaya zitazidi kutumia mikataba kufanya biashara kwa wingi na kuathiri kampuni za ndani ambazo hazina uwezo katika ushindani wa kimataifa.
Rais Mkapa ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Epa alisema kampuni ya bima ya Tanzania haiwezi kutoa bima kwa kampuni kubwa zilizopo Ulaya.
Alisema iwapo angevaa viatu vya Serikali basi angeimarisha mizizi katika umoja wa kikanda hasa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na EAC ili kukuza maendeleo ya siasa na uchumi kuliko kufanya mikataba na mataifa ya Ulaya.
Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji, Simon Mlay alifichua siri kuwa mkataba huo umeng’ang’ania kuruhusu masoko na usawa wa kibiashara ambao hautaongeza uuzaji wa bidhaa za Tanzania nje.
Alisema mkataba huo ni mbovu kwa sababu nchi haikujipanga kwenye majadiliano ya awali.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: