Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es
Salaam, imetoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paulo Makonda,
kuwasilisha utetezi wake dhidi ya kesi ya madai iliyofunguliwa na
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Singida, Mgana Msindai
na Mwenyekiti CCM mkoa Dar es Salaam, John Guninita.
Kesi hiyo namba 68 ya 2015, Makonda alitakiwa kuwasilisha utetezi
wake mahakamani jana, lakini wakili kupitia wakili wake, Lusiu Peter,
ameomba Mahakama kumuongezea muda. Hakimu Mkazi Mkuu, Hellen Riwa amekubali ombi la utetezi na ametoa
siku saba kwa Makonda kuwasilisha uetetezi wake hadi Aprili 23, mwaka
huu.
Hakimu Riwa alisema kesi hiyo itatajwa Aprili 27,mwaka huu. Katika kesi ya msingi, Msindai na Guninita wanaiomba mahakama hiyo
kumuamuru Makonda awaombe msamaha na kumlipa kila mmoja Sh. milioni
100.
Wanadai fidia hiyo kutokana na maneno ya kuwadhalilisha
yanayodaiwa kutolewa na Makonda kama Katibu Uhamasishaji na Chipukizi wa
CCM katika mkutano wake na waandishi wa habari. Msindai na Guninita kupitia wakili wao, Benjamini Mwakagamba,
wanaiomba Mahakama pamoja na mambo mengine itoe zuio la kudumu kwa
Makonda asizungumze tena maneno ya kashfa wala kuyasambaza kama
alivyofanya awali.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment