
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere, Dar es Salaam jana akitokea Marekani.
Katibu mkuu wa Chadema, Dk
Willibrod Slaa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza
kuandikisha wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM na kwamba ile
yenye upinzani itaandikishwa kwa kulipua ili watu wengi wenye sifa ya
kupiga kura wasiandikishwe.
NEC ilianza kuboresha Daftari la Wapigakura kwa
kuandikisha wananchi wa Mkoa wa Njombe, ambako watu 300,080
waliandikishwa kati ya 392,634 waliotarajiwa na sasa inaelekea mikoa ya
Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa baada ya kupokea mashine nyingine 1,600.
Kazi hiyo itaendelea kwenye mikoa ya Katavi, Mbeya na Dodoma wakati
mashine 1,600 zaidi zitakapowasili.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva
amesema hilo ni jambo jipya kwake kwa kuwa hawakuangalia suala hilo
wakati wa kupanga mikoa hiyo.
Akizungumza jana kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere mara baada ya kuwasili nchini akitokea
Marekani, Dk Slaa alisema wamegundua kwamba mwishoni mwa kazi ya
uandikishaji kwenye mikoa ambayo ni ngome ya vyama vya upinzani, watu
wengi hawataandikishwa.
“Tumegundua hujuma zao, NEC wameanza kuandikisha
wapigakura kwenye mikoa ambayo ni ngome ya CCM. Huko wanajitahidi
kuandikisha wapigakura wote na wanachukua muda mrefu,” alisema Dk Slaa
akionekana kurejea Mkoa wa Njombe ambako NEC imetumia takriban miezi
miwili kuandikisha wapigakura.
“Mikoa yenye ngome ya Chadema na vyama vingine vya
upinzani itakuwa ya mwisho kuandikisha wapigakura na uandikishaji huo
utakuwa wa harakaharaka ambao utawaacha mamia ya watu bila kuandikishwa
kwa sababu muda utakuwa hautoshi,” alisema Dk Slaa.
Alisema suala hilo linaweza kuvuruga uchaguzi, hasa ikizingatiwa kwamba mchakato wa uandikishaji umekuwa na sintofahamu nyingi.
Kwa mujibu wa matokeo ya urais katika Uchaguzi
Mkuu wa 2010, CCM ilivuna kura 128,809 katika majimbo matatu ya mkoani
Njombe (Njombe, Ludewa na Makete) wakati huo ukiwa ndani ya Mkoa wa
Iringa. Chadema ilifuatia kwa kupata kura 36,928 na CUF/NCCR zilipata
kura 1,670
Kwa kujumuisha kura hizo na majimbo mengine ya
Iringa CCM ilipata jumla ya kura 299,799 ikifuatiwa na Chadema iliyopata
kura 76,010. CUF na NCCR-Mageuzi zilipata jumla ya kura 3,137. Hadi
sasa upinzani una mbunge mmoja tu kwenye mikoa hiyo miwili, Mchungaji
Peter Msigwa wa Iringa Mjini.
Kwenye uchaguzi wa Rais mwaka 2010 mkoani Lindi,
mgombea wa CCM alipata kura 150,118 akiwa mbele ya mgombea wa CUF
aliyepata kura 64,875 wakati wagombea wa Chadema na NCCR walipata jumla
ya kura 12,880. Wapinzani wana wabunge wawili mkoani Lindi ambao ni
Selemani Bungera wa Kilwa Kusini na Salum Barwany wa Lindi Mjini, wote
kutoka CUF.
Mkoani Mtwara, mgombea urais wa CCM alipata kura
213,844 akimuacha mbali mgombea wa CUF aliyepata kura 81,953, huku
wagombea wa Chadema na NCCR wakipata jumla ya kura 82,233. Hakuna mbunge
kutoka upinzani mkoani Mtwara.
Takwimu za 2010 pia zinaonyesha kuwa mkoani
Ruvuma, mgombea urais wa CCM alipata kura 198,090, akimuacha kwa mbali
mgombea wa Chadema aliyepata kura 36,044, CUF (28,873) na NCCR kura 397.
“Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete atuepushe na vurugu zinazoweza
kutokea. Kwa kuwa anamaliza muda wake Oktoba 28, mwaka huu, ahakikishe
kwamba NEC inaandikisha watu wote bila kupendelea mikoa yenye ngome ya
CCM,” alisema.
Alisema Rais anatakiwa ahakikishe kwamba kwa
kutumia bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/16, NEC inawezeshwa kupata
fedha za kutosha ili iweze kuandikisha watu kwa ufanisi zaidi. “Tungependa Rais Kikwete aiache nchi ikiwa salama
kwa sababu kasoro zilizojitokeza katika zoezi hili ni nyingi na
zikiendelea zinaweza kuvuruga uchaguzi... uchaguzi ndiyo kipaumbele
chetu mwaka huu, ” alisema.
Alisema Serikali ihakikishe inashinikiza kuingizwa
kwa vifaa vya BVR ambavyo vinaingia kwa mafungu ili wananchi wenye sifa
waweze kuandikishwa. Hadi sasa kati ya mashine za BVR 8,000 ambazo
zinatakiwa kuingizwa nchini kwa ajili ya kazi hiyo, ni 2,098 tu ndizo
ambazo zimeshawasili.
NEC yajibu
Akijibu madai hayo Jaji Lubuva alisema hilo ni
jambo jipya kwake: “Hatufahamu kwamba mikoa hiyo ni ngome ya CCM,”
alijitetea Jaji Lubuva. “Tumeanza kuandikisha bila kujali kwamba hiyo ni
ngome ya chama fulani cha siasa.” Alisema Dk Slaa anachotakiwa kufahamu
ni kwamba kila mwananchi mwenye sifa atakayejitokeza kuandikishwa,
ataandikishwa.
“Sisi hatuangalii ngome za vyama vya siasa, kazi yetu ni kuandikisha bila kujali hapa ni ngome ya nani,” alisema.
Ziara ya Marekani
Dk Slaa, ambaye aliambatana na mkewe, Josephine
Mushumbushi alisema wamekubaliana kuanzisha ushirikiano hasa katika
nyanja za kiuchumi na Jimbo la Indiana.
“Tumekubaliana kwamba tukiingia Ikulu tutapenda
kuwa na wawekezaji, lakini tofauti na ilivyo sasa. Watakaotaka kuja
kuwekeza nchini watatakiwa kufanya hivyo kwa kufuata masharti yetu na
siyo masharti yao,” alisema.
Dk Slaa aliwasili jana saa 2.30 asubuhi kwa ndege
ya Shirika la Qatar Airways na kulakiwa na wafuasi wa chama hicho
waliokuwa na bango linalosomeka, “Karibu nyumbani rais wa awamu ya tano
Dk Willibrod Slaa.”
Mauaji ya Afrika Kusini
Dk Slaa alikwenda Marekani kwa mwaliko wa Gavana wa Jimbo la
Indiana, Mike Pence pamoja na taasisi mbalimbali, vikiwamo vyuo vikuu,
baada ya kutambua mchango wake na wa chama chake katika masuala ya
kisiasa na kijamii katika maendeleo ya Bara la Afrika.
Akifafanua, alisema alipata fursa ya kutembelea
sehemu mbalimbali za vyuo na kujionea namna nchi hiyo inavyothamini
tafiti za wasomi. “Wenzetu wamewekeza kwenye tafiti, moja ya vipaumbele
vikubwa kwa Serikali yao ni kutoa fedha za kutosha kwenye tafiti tofauti
na hapa nchini ambako utafiti siyo kipaumbele chetu,” alisema.
Alisema pia alitembelea shamba la mifugo lenye
ng’ombe wa maziwa 15,000 ambako alikuta ng’ombe mmoja anatoa lita 27 kwa
siku na kwamba linatoa mchango mkubwa katika uchumi. “Nikajiuliza, sisi Tanzania ni nchi ya tatu kwa
kuwa na ng’ombe wengi Afrika, lakini wanasaidia vipi katika uchumi wetu
wakati hata viatu tunaagiza kutoka China wakati tuna ngozi ya kutosha?”
alisema.
Mauaji ya Afrika Kusini
Dk Slaa pia amemtaka Waziri wa Mambo ya Nje ya
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuacha kufanya siasa wakati
maisha ya Watanzania wanaoishi Afrika Kusini, yako hatarini.
“Watanzania hao wanatakiwa kurudishwa nchini
haraka hadi hali ya usalama itakaporejea Afrika Kusini. Serikali
isikwepe jukumu la kuwarudisha wananchi wake,” alisema.
Alisema anashangazwa na kauli ya Membe kwamba Mtanzania aliyekufa Afrika Kusini aliuawa kwa ujambazi. “Unadhani watasema ameuawa kwa sababu gani wakati
hata polisi wa Afrika Kusini wako upande wa vijana hao wanaofanya
vurugu? Alitakiwa kufanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha kwamba
Mtanzania huyo aliuawa kwa ujambazi,” alisema.
Juzi, Membe alikaririwa akisema kuna Watanzania
watatu ambao wamekufa lakini akakanusha kuwa waliuawa kwenye vurugu
zinazoendelea Afrika Kusini. Miongoni mwa waliokufa ni Rashid Jumanne
ambaye aliuawa kilomita 90 kutoka mji wa Durban.
ACT- Wazalendo
Akizungumzia ujio wa chama cha Alliance for Change
and Transparency (ACT-Wazalendo), alisema kwa kifupi: “Nakiona kama
vyama vingine lakini siyo tishio kwa Chadema kwani chama chetu kina
misingi imara ambayo inakifanya kila siku kuwa juu,” alisema kwa kifupi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment