Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif
Sharif Hamad, amewataka wanachama walioomba nafasi mbali mbali ndani ya
chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu kujenga
imani na kamati za uteuzi wa wagombea.
Alisema kamati zote zilizoteuliwa kufanya kazi hiyo zitafanya kazi
zake kwa umakini bila ya kujali wadhifa au umaarufu wa mgombea. Maalim Seif alieleza hayo jana katika kikao maalum cha
kubadilishana mawazo na wanachama walioomba kugombea nafasi za ubunge,
uwakilishi na udiwani upande wa Unguja, kilichofanyika mjini hapa.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
alisema kamati zilizochaguliwa zimewekewa vigezo maalum na zitafanya
kazi ya kuwateua wanachama wenye moyo wa kujituma na kukitumikia chama
ili kipate ushindi. Aliwapongeza wanachama wa chama hicho kwa kujitokeza kwa wingi
kugombea nafasi hizo, hali inayodhihirisha demokrasia ndani ya chama
hicho.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema
wanachama 310 wamejitokeza kugombea uwakilishi na ubunge katika majimbo
32 ya Unguja na Pemba. Alisema hatua inayofuata sasa ni kwa wagombea hao kufanyiwa usaili,
kazi inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii na kwa upande wa
Pemba tayari kazi hiyo imeshafanyika.
Shehe alisema kwa mara ya kwanza kufanyika kwa uchaguzi chini ya
mfumo wa vyama vingi wa mwaka 1995, chama hicho kinatarajia kusimamisha
wagombea wa udiwani katika wadi zote za Zanzibar, hatua inayoonesha
kupevuka kwa chama hicho kisiasa.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema kinatarajia kufanya mchujo wa wagombea mwezi ujao. Mchujo huo utakuwa na ushindani mkali kutokana na wanachama wengi kujitokeza kutaka kuwania nafasi hizo.
Vigogo wengi wa CUF wamepata wapinzani, ambao wanataka kuwaengua
katika nafasi za uwakilishi na ubunge wanazoziwakilisha hivi sasa. Akizungumza na NIPASHE, Ofisa Uchaguzi wa CUF, Mhene Said Rashid,
alisema idadi ya wanachama waliojitokeza kuomba kugombea nafasi hizo
mwaka huu imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2010.
Alisema wanachama 559 wamejitokeza kugombea nafasi za uwakilishi na
ubunge katika visiwa vya Unguja na Pemba, huku wanachama 381 wakiomba
kuwania nafasi za diwani.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment