Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi, na Teknolojia,
January Makamba, amesema ipo haja kwa serikali kufuatilia fedha
zilizotolewa kwenye sekta kadhaa kama zimeleta mabadiliko chanja kwa
jamii husika.
Aliyasema hayo jana wakati wa kuwasilikiliza wananchi 400 wanaotoka
wilaya mbalimbali nchini ambao watashiriki utafiti wa ushiriki wa
wananchi katika maamuzi ya matumizi ya mapato yatokanayo na raslimali za
gesi na mafuta ulioandaliwa na Center for Global Development (CGD) na
Repoa.
Alisema kwa siku za hivi karibuni katika bajeti ya serikali
zimeongezwa fedha mara dufu kwenye sekta ya elimu, lakini matokeo
yamezidi kuwa mabaya tofauti na inavyotarajiwa. “Siyo kila tatizo unatumbukiza fedha…kwa sasa tunatarajia uchumi wa
gesi, hivyo ni lazima tuangalie namna ya kuzitumia kwa muundo wa
kunufaisha Watanzania wote,” alisema.
Alisema baada ya mahojiano na wananchi wanaoshiriki mkutano huo
kabla ya utafiti, amebaini wana uelewa mkubwa na wengi wamekuwa na maoni
tofauti juu ya matumizi ya fedha za mapato na matumizi ya gesi pamoja
na mafuta na kwamba baadhi wanatamani zitumike kutatua matatizo yaliyopo
kwenye maeneo yao.
“Wananchi ndiyo wenye ufahamu mkubwa wa matatizo yao ambayo
wangependa serikali iyape kipaumbele mara itakapopata fedha zitokanazo
na uchumi wa gesi na mafuta,” alisema.
Alisema kwa sasa serikali inajipanga kikamilifu kabla ya kuingia
kwenye uchumi huo kuwa na wataalamu wengi wenye uelewa wa kutosha wa
sekta hizo ili kuhakikisha Tanzania inanufaika.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment