
Moja ya ajali zilizotokea hapa nchini
Wakati ajali za barabarani
zikiendelea kukithiri nchini na kugharimu maisha ya mamia ya watu na
wengine kubakia na ulemavu, wadau wanaamini kuwa janga hilo linaweza
kupunguzwa ikiwa hatua kadhaa zitachukuliwa.
Kumekuwa na ajali nyingi katika miezi ya karibuni,
hasa zinazohusisha mabasi ya masafa marefu, na juhudi za Serikali
kuzipunguza, ikiwa ni pamoja na kutaka madereva warudi mafunzoni kila
baada ya miaka mitatu, hazijafanikiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za ajali zilizotolewa juzi
na mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga,
kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu ajali zilikuwa 2,116 ambazo
zilisababisha vifo 866 na kujeruhi watu 2,363.
Ajali hizo zimetokea katika kipindi tofauti na
miaka iliyopita ambayo ajali nyingi zilikuwa zikitokea mwishoni mwa
mwaka, kipindi ambacho mwaka jana kikosi hicho cha usalama barabarani
kilisema kiliweka mkakati madhubuti wa kupunguza matukio hayo na hivyo
kufanikiwa.
Wakati Kamanda Mpinga akitoa taarifa hizo, Jeshi
la Polisi, Kanda ya Dar es Salaam limesema kuanzia Machi Mosi, kulikuwa
na makosa 34,641 kwenye mkoa mmoja pekee na hivyo kulifanya Jeshi la
Polisi kuvuna Sh1.04 bilioni zinazotokana na faini.
Wakizungumza na Mwananchi jana, wadau kadhaa
walipendekeza mambo kadhaa ambayo walisema yanaweza kupunguza ajali,
ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria kali na kuwapo kwa elimu ya mara
kwa mara kwa madereva. “Sheria zikibadilishwa na kufanywa kuwa kali
zaidi, lazima tutaona mabadiliko,” alisema makamu mkuu wa Chuo cha
Usafirisaji (NIT), Dk Simon Lushakuzi.
Mkuu huyo alisema sheria za usalama barabarani zinazotumika sasa ni lazima ziboreshwe. “Dereva anaweza kusababisha ajali na kuua mtu,
lakini faini anayotakiwa kulipa ni Sh20,000. Ndiyo maana wanakuwa
wazembe barabarani,” alisema mkuu huyo. Hata hivyo, katika kuboresha sheria hizo, Serikali
iliunda kanuni zinazotaka madereva wapate mafunzo ya muda mfupi kabla
ya kupewa leseni mpya.
Kanuni hizo pia ziliweka adhabu kali kwa madereva
ambao magari yao yanahusika kwenye ajali, ikiwa ni pamoja na
kunyang’anywa leseni na kuwekwa mahabusu, lakini madereva wakafanya
mgomo mkubwa nchi nzima uliosababisha Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka kutangaza kutengua kuanza kutumika kwa kanuni hizo.
Tangu kuzimwa kwa mgomo huo Jumapili iliyopita,
ajali zimekuwa zikitokea takriban kila siku na jana basi la Air Jordan
lilipata ajali wilayani Nzega, Tabora na kuua mtu mmoja na kujeruhi
wengine 28.
Dk Lushakuzi, ambaye chuo chake ni moja ya taasisi mbili ambazo
Serikali iliziteua kwa ajili ya kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa madereva
kila mara leseni zao zinapoisha, alisema mafunzo ya mara kwa mara kwa
madereva pia ni muhimu. “Miji inakua kwa kasi kwa hivyo ni lazima madereva
wapate mafunzo ili waende sambamba na mabadiliko hayo dereva aliyewahi
kuendesha gari jijini hapa miaka mitatu iliyopita na kuondoka ukimleta
hawezi kuendesha gari vizuri kama zamani lazima apate mafunzo.”
Mmiliki wa mabasi ya Mrindoko, Hussein Mrindoko aliungana na Dk Lushakuzi kuhusu umuhimu wa elimu.
“Elimu ni kila kitu. Tukielimishana vizuri namna
ya kufuata miongozo na kanuni za barabarani bila kusukumana, tutafika
mbali na siyo kutegemea Polisi kwa kila kitu,” alisema Mrindoko.
Mmiliki wa mabasi ya Ngorika, George Temba
alipingana na dhana kuwa chanzo cha ajali ni madereva kuchoka kutokana
na kutokuwa na wasaidizi, badala yake akaelekeza lawama kwa Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra).
Alisema mamlaka hiyo imeweka utaratibu wa mabasi ya mikoani kutoka kwa vituo vya mabasi asubuhi saa 12:00. “Mabasi yanaporuhusiwa kuondoka kituoni, madereva huwa wanakimbizana ili kuwahi abiria kituo kinachofuata,” alisema Temba. “Sumatra wanatakiwa kubadilisha huo utaratibu.
Kama inawezekana magari yawe yanaruhusiwa kutoka kituoni kwa kupishana
hata kwa dakika kumi na tano.”
Temba, ambaye magari yake hufanya safari kati ya
Dar es Salaam na Kilimanjaro, alisema njia nyingine ni kutoa vibali kwa
wamiliki wa mabasi kutumia barabara mpya.
“Si sawa magari zaidi ya 60 kutumia ruti moja
wakati kuna barabara mpya ambazo wamiliki wapya wa mabasi wanaweza
kupewa kibali cha kuzitumia kuliko kulundika magari kwenye barabara
moja,”alisema na kutoa mfano wa barabara kutoka Dodoma kwenda Mbeya
kupitia Mtera ambayo haina mabasi mengi.
Nassoro Sanga, dereva wa malori ya mizigo
yanayofanya safari za Zambia, alisema ili kupunguza ajali madereva
wanatakiwa kuzingatia alama za barabarani.
“Uzembe wa kutozingatia alama hizo umekuwa
ukisababisha ajali hata mwendo kasi pia. Kuna madereva wanakimbiza sana
magari wakati mwendo unaotakiwa unafahamika,” alisema Sanga.
Alisema, madereva wanatakiwa kuacha kunywa pombe. “Huwezi kuamini alfajiri tukiwa tunaanza safari
unakuta mtu ‘anabugia kiroba’ cha pombe halafu anaendesha gari. Huko
barabarani uendeshaji wake ni hovyo sana. Unategemea asisababishe ajali?
Hakuna.”
Dereva wa lori linalosafirisha mizigo kwenda
Congo, Jerry George alisema endapo kipato cha madereva kikiongezeka na
kukidhi mahitaji yao, itasaidia kupunguza ajali za barabarani.
“Madereva wanalazimika kwenda mwendo kasi ili
wawahi kule wanakokwenda na kurudi haraka kwa sababu ya maslahi yao.
Lakini kama mtu analipwa hela ya kutosha kukidhi mahitaji yake, haraka
ya nini?” alihoji. Alisema, akienda safari ya wiki moja analipwa Sh 200,000, fedha ambazo alisema hazitoshi.
Kaimu katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alieleza
kusikitishwa kwake na kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na ajali za
barabarani. “Mara nyingi serikali imekuwa ikitoa salamu za
rambirambi kwa wahanga wa ajali hizo. Kama si Rais mwenyewe, basi
wasemaji wake lakini hatuambiwi ni mikakati gani ipo mezani ili
kukabiliana nazo,” alisema Mnyika.
Mnyika aliiomba jamii kwa ujumla kutumia nguvu
kama ile inayotumika kupambana na mauaji ya albino na kueleza kuwa ajali
hizo zimekuwa ni janga la Taifa kutokana na kupoteza maisha ya wananchi
wengi ndani ya muda mfupi.
Neema Fanuel, mkazi wa Mwanza alisema: “Watu wakiacha kutoa na kupokea rushwa, nadhani tutapunguza ajali,” alisema. “Unakuta mtu amevunja sheria halafu anatoa kitu kidogo na kuachiwa.”
Wakati huohuo, Mustapha Kapalata anaripoti kutoka
Tabora kuwa jinamizi la ajali limeendelea baada ya basi la Air Jordan
lililokuwa likitoka Mwanza kwenda Arusha kupata ajali katika Kijiji cha
Ngonho, Kata ya Kitangili wilayani Nzega na kusababisha kifo cha mtu
mmoja na kujeruhi wengine 28 wakijeruhiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Jackline Liana alisema
mtu huyo aliyefariki ambaye alikuwa fundi wa gari hilo, ametambuliwa kwa
jina mmoja la Emmanuel na uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo cha
ajali hiyo ni mwendokasi. Dereva wa basi hilo alitoweka.
Mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk Erick Mbuguye alisema walipokea majeruhi 28, akisema hali ya majeruhi wanne ni mbaya.
CHANZO: MWANANCHI
Mganga mkuu mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk Erick Mbuguye alisema walipokea majeruhi 28, akisema hali ya majeruhi wanne ni mbaya.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment