50% Watu waliojifungua kwa upasuaji mwaka jana.
Wakati idadi ya wanawake wanaojifungua kwa
upasuaji ikizidi kuongezeka nchini, utafiti mpya umeonyesha kuwa
migogoro baina ya wahudumu wa afya ya uzazi imechangia ongezeko la
wajawazito wanaofanyiwa upasuaji bila kuwapo sababu za lazima.
Utafiti huyo uliowahusisha wanawake 13
waliojifungua kwa upasuaji hivi karibuni, madaktari 18 na wakunga 14
jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa baadhi ya wahudumu wa afya ya uzazi
huwafanyia upasuaji wajawazito kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mwanafunzi wa
Shahada ya Uzamivu, kutoka Chuo Kikuu cha Uppsala cha nchini Sweeden,
Helena Litorp anasema, migororo na ‘presha’ ya kazi ni moja ya sababu za
ongezeko la wanawake wanaojifungua kwa upasuaji.
Akizungumza kwa kujiamini, Litorp anasema pamoja
na ukweli kwamba wanawake wanaogopa kujifungua kwa njia ya upasuaji
wakihofia kifo, huku baadhi ya wahudumu wa afya nao wakiamini kuwa njia
hiyo siyo salama kwa wajawazito ikilinganishwa na njia ya kawaida,
makundi yote mawili yanakubali kufanyika upasuaji huo kwa lengo la
kumwokoa mtoto anayezaliwa.
Hata hivyo, anasema matokeo ya utafiti huo
uliofanyika mwaka jana, yanaonyesha kuwa kati ya mwaka 2000 na 2002
asilimia 19 ya wajawazito walijifungua kwa upasuaji huku kiwango hicho
kikipanda hadi kufikia asilimia 49 kati ya mwaka 2009 na 2011.
“Tuligundua kuwa madaktari vijana ambao wamepewa
jukumu la kuzalisha kwa njia ya upasuaji wanakosa msaada kutoka kwa
viongozi wao jambo ambalo wakati mwingine husababisha migogoro baina
yao. Madaktari na wakunga wote walisema wanaogopa kulaumiwa kwenye vikao
kwa uzembe, hivyo wakati mwingine wamejikuta wakilazimika kuzalisha kwa
upasuaji bila kuwa na sababu ya lazima,” anasema.
Madaktari na wakunga wanasema ongezeko la wanawake
wanaojifungua kwa upasuaji linatokana na sababu zilizo nje ya uwezo
wao. Wanawake hufikishwa katika hospitali zisizo na vifaa vya kutosha.
Pia, wengine wanachelewa kwenda kupata huduma kutokana na elimu na
ndogo, lakini wapo baadhi yao ambao hutaka kujifungua kwa upasuaji.
Hata hivyo, anasema kuwa idadi kubwa ya vifo
vilivyotokana na uzazi vilisababishwa na shinikizo la damu wakati wa
ujauzito/kifafa cha mimba na kupoteza damu nyingi muda mchache baada ya
kujifungua, lakini wamebaini kuwa sehemu kubwa ya vifo hivyo (7 asilimia
.9), na vifo (asilimia 13) vinahusiana moja kwa moja na kujifungua kwa
upasuaji.
“Tulipiga hesabu kwa kila operesheni 1,000 na
kubaini kwamba hatari imeongezeka mara tatu zaidi katika hospitali ya
mkoa kuliko ile ya chuo kikuu. Changamoto nyingi zilitokana na utoaji wa
nusu kaputi ama dawa ya usingizi kwa njia ya uti wa mgongo na uambukizi
wa vimelea katika kovu la upasuaji.
Tuliyatafsiri matokeo hayo kama ushahidi wa
ongezeko la kujifungua kwa upasuaji katika maeneo yenye vifaa vya huduma
vichache, hasa katika hospitali ndogo na pia kuna haja ya kuongeza
ubora wa huduma hasa huduma za utoaji dawa za usingizi.
Vilevile, Litorp anasema katika utafiti huo
walitaka kubaini iwapo wanawake wenye makovu yaliyotokana na upasuaji
wapo katika hatari zaidi ya kupoteza maisha yao au watoto wao. Matokeo
yameonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya mambo hayo mawili,
badala yake wanawake hao walijifungua salama.
“Matokeo yanatofautiana na vitabu kadhaa
vilivyoandikwa awali, lakini yanaweza kuwa hivyo kutokana na kwamba
wanawake waliowahi kujifungua kwa upasuaji huangaliwa kwa makini
wanapopewa huduma ya afya. Kwa sababu hiyo hutakiwa kuja hospitali
mapema wanapokaribia kujifungua, mara nyingi hupelekwe kwenye hospitali
zenye huduma bora zaidi,” anasema.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Uuguzi MNH, Dk Agnes Mtawa anasema,
operesheni hizo zimeongezeka kwa asilimia 31 katika kipindi cha miaka 11
iliyopita. “Ongezeko la ghafla la idadi ya kina mama
wanaojifungua kwa operesheni kutoka asilimia 19 mwaka 2000 hadi asilimia
50 mwaka 2011 linatisha na linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina,”
anasema Mtawa.
Mtawa anaeleza kuwa pamoja na kwamba kujifungua
kwa njia ya upasuaji ni njia ya kuokoa maisha, utaratibu huo umegeuka
tishio kwa wajawazito na jamii kwa ujumla.
Anasema hali hiyo imefika hapo ilipo kutokana na
sababu mbalimbali zikiwamo miundo mbinu hafifu ya afya, uhaba wa
rasilimali watu, ukosefu wa vifaa na wafanyakazi kukosa motisha. “Ninafurahi kutambua kwamba zipo tafiti
zinazoendelea kufanywa kuhusu uzazi kwa njia ya upasuaji na kueleza
mtazamo wa watoa huduma za afya kuhusu upasuaji huo. Nina hamu ya
kusikia matokeo ya tafiti hizo,” anasema.
Hata hivyo, anasema pamoja na wajawazito
wanaojifungua kwa upasuaji kuongezeka, vifo vya kinamama hao vimepungua
kwa kiasi kikukwa katika miaka 10. Hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa
wanafariki wajawazito 478 kati 100,000 wanaokwenda kujifungua.
Mkurugenzi huyo anasema pamoja na mafanikio hayo,
Tanzania haijaweza kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia yanayotaka
kuwe na vifo chini ya 200 kwa kila wajawazito 100,000. Pia, anasema
idadi kubwa ya wajawazito hufariki dakika 30 tangu wamefika hospitalini
kutokana na kuchelewa.
Mkunga katika hospitali hiyo, Gloria Mkusa anasema
kwa mwaka anazalisha wanawake wengi wanaojifungua kwa upasuaji kuliko
wanaojifungua kwa njia ya kawaida. “Zaidi ya nusu ya wamama tunawapokea wanajifungua
kwa upasuaji. Sababu zinategemeana, mara nyingine inakuwa sababu ni
mtoto, mara nyingine ni mama,” anasema na kuongeza kuwa mwaka 2014
hospitali hiyo ilipokea wajawazito zaidi ya 11,000.
Hata hivyo, Mkunga na Mhadhiri wa Ukunga wa Chuo
Kikuu cha Tiba cha Muhimbili, Dk Sebalda Leshabari aliwahi kunukuliwa na
gazeti hili, akisema kuwa upasuaji si jambo zuri kwa wajawazito. “Upasuaji siyo jambo zuri kabisa katika muktadha wa uzazi na ndiyo maana watu huita ni kujifungua kusiko kwa kawaida,” anasema.
Anataja madhara yanayowapata wajawazito wengi
baada ya kujifungua kwa upasuaji kuwa ni pamoja na maziwa kutotoka kwa
siku kadhaa baada ya kujifungua. “Maziwa yasipotoka ina maana mtoto anakosa yale maziwa ya kwanza ya mama ambayo huwa na virutubisho vyote,” anasema.
CHANZO: MWANANCHI
Anaongeza kuwa wajawazito wengi wanaofanyiwa
upasuaji hulalamika kupata maumivu ya kichwa kwa muda mrefu pamoja na
maumivu ya uti wa mgongo. Pia, anasema baadhi ya wanawake hutaka
kujifungua kwa upasuaji bila kuwa na sababu maalumu kutokana na kuwa na
dhana potofu.
Taarifa nyingine zinaonyesha kuwa hospitali
binafsi zina tabia ya kulazimisha wanawake kujifungua kwa njia ya
upasuaji kwa malengo ya kuongeza mapato.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa kujifungua kwa upasuaji katika hospitali binafsi ni gharama inayozidi mara tatu ya ile ya kawaida.
Hii ina maana kwamba wanawake watatu wanaojifungua
kwa njia ya kawaida kwenye hospitali hizo, gharama zake ni sawa na
mmoja anayejifungua kwa upasuaji.
Tatizo jingine linatokana na wanawake wenyewe ambao huona taabu au karaha kujifungua kwa njia ya kawaida.
Hii inaweza ikawa ni kwa kushauriwa vibaya na
jamii ama watu wa karibu. Baadhi ya watu mitaani wanadai njia hii
haiathiri viungo vya uzazi vya mwanamke na wala hapati maumivu. Ukweli ni kwamba wataalamu wanapendekeza njia ya kawaida kuwa ni bora zaidi.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment