
Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa.
Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na idadi
kubwa ya wananchi wenye sifa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015, kwa kuwa na watu 2,932,930.
Ripoti ya makadirio ya idadi ya watu na wapiga kura kwa mwaka 2015
iliyowekwa kwenye mtandao wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),
iliyoonyesha idadi ya watu watakao kuwa na sifa ya kupiga kura mwaka huu
kimajimbo na kitaifa kuwa ni watu 24,253,541.
Taarifa hiyo ilisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa
(pichani), na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk.
Mohamed Hafidh Rajab. Taarifa hiyo imeeleza majiji yanayofuata ni ya Mbeya lenye watu
wenye sifa ya kupiga kura 1,477,365, Mwanza 1,403,743 na Morogoro
1,264,829 huku mikoa mitatu yenye wapiga kura wachache kwa Tanzania Bara
ikiwa ni Rukwa 472,796, Njombe 392,634 na Katavi 271,160.
Kwa upande wa Zanzibar mkoa wenye wapiga kura wengi ni Mjini
Magharibi wenye watu wenye sifa ya kupiga kura 346,524 na wenye wapiga
kura wachache ni Kusini Unguja 63,546. Pia, imeeleza kuwa hadi kufika siku ya uchaguzi mkuu, Tanzania
itakuwa na watu wapatao 48,522,228, ikiwa ni watu 47,110,506 wa Tanzania
Bara na 1,411,722 wa Zanzibar.
Taarifa hiyo imeainisha kuwa idadi ya wenye sifa ya kupiga kura
kati ya hao kwa Tanzania Bara ni 23,533,050 na Zanzibar ni 720,491. Taarifa hiyo imeanisha majimbo ya Tanzania bara ni 189, Zanzibar
ikiwa na majimbo 50, huku kwa Tanzania Bara mikoa inayoongoza kwa
majimbo mengi na idadi kwenye mabano ni Tanga (11), Mbeya (11), Morogoro
(10) na mingine ikiwa na majimbo chini ya kumi, na wenye majimbo
machache ni Katavi ambayo ni matatu.
Upande wa Zanzibar mkoa wenye majimbo mengi ni Mjini Magharibi majimbo 19 na Kusini Unguja majimbo matano. Taarifa hiyo imebainisha kuwa makadirio ya idadi ya wapiga kura
yametokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kwa kutumia mbinu za
kidemografia zinazohusisha mabadiliko katika viwango vya uzazi, vifo,
uhamaji na uhamiaji katika ngazi ya Taifa, mkoa, wilaya, majimbo ya
uchaguzi na kata au Shehia husika.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment