
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
umesema haumbebi mtu yeyote anayetaka kugombea urais miongoni mwa
wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ndani ya chama hicho katika
uchaguzi mkuu ujao.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, akizungumza na NIPASHE jana,
alisema kwa sasa hakuna mtu yeyote, ambaye ameshachukua fomu ya kuwania
nafasi hiyo, hivyo umoja huo hauna mgombea wanayemuunga mkono zaidi ya
yule, ambaye atapitishwa na chama muda utakapofika.
“Mgombea yupi? Hawa unaosikia wanatangaza nia tuna uhakika gani
kama watagombea? Na wakija kusema walikuwa wanatania? Chama
hakijapitisha yeyote kugombea nafasi ya urais. Hivyo, sisi hatuna
mgombea zaidi ya atakayeteuliwa na chama,” alisema Mapunda.
Kuhusu baadhi ya vijana wa vyuo vikuu na walioanza kueleza msimamo
wao juu ya viongozi na makada waliojitangaza, Mapunda alisema hawezi
kuelezea msimamo wa mtu mmoja mmoja, kwani sheria na kanuni za chama
hicho zitawabana. Alisema kila kijana ana uhuru wa kumpigia kura kiongozi
anayemuhitaji, lakini kama UVCCM wana wajibu wa kusimamia msimamo wa
chama juu ya kiongozi atakayesimamishwa.
“Hatuwezi kumzuia mtu kusema, lakini tuna uhakika gani hao viongozi
wa vyuo walioeleza msimamo wao kama ni wa UVCCM? Hata kama watakuwa
wamesema, kanuni na taratibu za chama ziko wazi na msimamo wetu uko
wazi. Tuna wajibu wa kumsimamia kiongozi aliyepitishwa na chama,”
alisema Mapunda.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment