Social Icons

Pages

Tuesday, March 17, 2015

NEC, SERIKALI ZASHINDWA KUTEGUA KITENDAWILI KURA MAONI APRIL 30

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikisema kukamilika kwa uandikishaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ndiko kutakakotoa mwelekeo wa ama kupigwa kura ya maoni au la, serikali imesema bado msimamo wake kwamba, kura hiyo itapigwa Aprili 30, mwaka huu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro (pichani), alisema hawezi kupiga ramli kujua ya siri kama kura hiyo, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa, itapigwa tarehe hiyo au la.
Alisema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kukabidhi nakala ya katiba inayopendekezwa kwa wawakilishi wa serikali, binafsi, kidini na kiraia, jijini Dar es Salaam jana. Alisema chombo chenye majibu ya kama kura hiyo itapigwa katika tarehe hiyo au la, ni Nec na kwamba, yeye hawezi kufanya kazi ya kuijibia suala hilo.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inafanya kazi yake hivi sasa, kwa hiyo nisingependa kupiga ramli. Tunachojua kura ya maoni itafanyika tarehe 30 Aprili, nisingependa nijibu kwa niaba ya tume,” alisema Dk. Migiro. Awali, akikabidhi nakala ya katiba inayopendekezwa kwa wawakilishi wa asasi hizo, Dk. Migiro alisema siyo kitabu cha riwaya, bali ni waraka unaotakiwa kusomwa kwa vikundi.
Alisema jana ilikuwa ni hatua ya pili ya kusambaza katiba hiyo baada ya kukamilisha hatua ya kwanza katika mikoa yote iliyoko Tanzania Bara na Zanzibar, huku kila kata zilizoko Tanzania Bara ikipata nakala 300. Dk. Migiro alisema wiki kadhaa zilizopita walikamilisha uchapishaji na usambazaji wa nakala takriban milioni mbili za katiba hiyo na kwamba, Tanzania Bara nakala 1,141,300 zilisambazwa chini ya uratibu wa uongozi wa serikali wilaya na mkoa, huku nakala 658,700 zilizobaki zikikusudiwa kusambazwa kwa wizara, taasisi za serikali, asasi za kiraia, kidini na makundi mbalimbali ya kijamii.
Alisema Zanzibar zimepelekwa nakala 200,000, ambazo zitasambazwa  mikoa yote chini ya ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. Waziri Migiro akisema hayo, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva, alisema kinachoangaliwa na kufanyika kwa ukaribu ni uandikishaji wa wapigakura.
“Kura ya maoni itategemea uboreshaji wa daftari la wapigakura, kama tarehe itafika na haujakamilika tutawajulisha umma wa Watanzania. Uboreshaji wa daftari ndicho cha kwanza halafu mengine yatafuata,” alisema. Alisema hadi sasa vifaa (BVR kits) vinavyotumika mkoani Njombe ni 250 na vifaa 7,750 vipo njiani na serikali imeshavilipia.
Alipoulizwa vitawasili lini na kiasi cha fedha kilichotolewa hadi sasa, alisema “Umma ujue kuwa serikali imetoa fedha tumeagiza vifaa vipo njiani na wakati wowote vitawasili, na tutatoa ratiba ya uandikishaji nchi nzima,” Kwa mujibu wa taarifa ya Nec iliyotolewa mara kwa mara imeeleza kuwa baada ya vifaa kuwasili uandikishaji utafanyika nchi nzima isipokuwa Zanzibar na Dar es Salaam, kutasubiri vifaa vyote na uandikishaji utakuwa kwa wakati mmoja.
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, imesema imeridhishwa na mwenendo wa uandikishaji wapigakura unaoendelea mkoani Njombe. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jasson Rweikiza, alisema kamati yake ilitembelea na kuona jinsi mashine zinavyofanya kazi kwa muda wa dakika tatu, mwananchi anapata kadi ya kupigia kura.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: