Social Icons

Pages

Friday, March 13, 2015

UCHAKACHUAJI MAFUTA WAISABABISHIA SERIKALI HASARA YA SH BIL 5

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndasa.
Serikali  inapoteza zaidi ya Sh. bilioni tano za kodi kwa mwaka kutokana na mafuta yanayodaiwa kwenda nje kuchakachuliwa na kurudishwa nchini, hivyo kusababisha hasara kubwa.
Kadhalika, serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, imetakiwa kuwasimamia  wafanyabiashara wa mafuta kuhakikisha haipati hasara katika mapato yake. Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndasa, wakati akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam.
Alisema mapato ya serikali kupitia mafuta yanapungua kutokana na Wizara ya Fedha kuwasiliana moja kwa moja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) badala ya Wizara ya Nishati na Madini kinyume cha utaratibu. “Mafuta yanayoingia nchini asilimia kubwa kumbukumbu zinaonyesha yanakwenda nje, lakini hayafiki kwa kuwa yanazunguka na kurudi kutumika ndani bila kulipiwa kodi na kuipotezea serikali zaidi ya Sh. bilioni tano kwa mwaka…lazima Wizara ya Nishati na Madini ishirikishwe,” alisema. Ndasa.
Akizungumzia kero ya mara kwa mara ya kukatika umeme, alisema kamati yake inataka kupata taarifa kutoka kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na matatizo ya ukosefu wa huduma ya mfumo wa Luku yanayoendelea nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Tanesco, Felchesmi Mramba, akizungumzia mfumo wa Luku, alisema matumizi ya huduma hiyo yameongezeka kutoka watu 300,000 hadi kufikia zaidi ya milioni moja. Alisema mfumo huo ulianza kutumika mwaka 2004 na kwamba kwa wakati walihudumia watu 300,000 tofauti na sasa.
“Watu wanaotumia Luku kwa sasa ni zaidi ya milioni moja, mfumo umezidiwa, shirika linafanya marekebisho ili kuendana na idadi ya watu, ukarabati wa mfumo huo utakapokamilika huduma itaendelea kuwa sawa kwa wananchi, “ alisema Mramba. Aidha, alisema kukatika kwa umeme mara kwa mara kunatokana na ukarabati wa vituo vya kuongeza nguvu ya huduma hiyo unaoendelea hivi sasa nchini kote.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: