Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za
Binadamu, Jaji Agustino Ramadhani ameziomba asasi na taasisi za kisheria
na haki za binadamu kuzihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU),
kuridhia mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Akifungua mkutano wa jukwaa la wanasheria na wadau
wa haki za binadamu barani Afrika jijini Arusha jana, Jaji Ramadhani
alisema hadi sasa ni nchi 28 pekee kati ya 54 wanachama wa AU ndizo
zimeridhia mkataba huo.
“Kati ya hizo, ni mataifa saba pekee yametoa
azimio la kuruhusu raia wake na asasi zisizo za kiserikali kuwasilisha
maombi yao mbele ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu,” alisema
Jaji Ramadhani na kuhoji:
“Iwaje nchi 35 ziridhie Mkataba wa Rome
ulioanzisha Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, lakini zinashindwa
kuridhia mkataba wa kuanzishwa kwa Mahakama yao wenyewe?
“Kama raia wa nchi za Afrika hawana fursa ya
kufikisha madai yao mbele ya mahakama yao kwa sababu mataifa yao
hayajaridhia mkataba wa kuwa na mahakama yao wenyewe, ni sawa na kutoa
haki kwa kutumia mkono mmoja na kuichukua kwa mkono mwingine,”
alisisitiza Jaji Ramadhani.
Katibu mtendaji wa jukwaa la wanasheria na wadau
wa haki za binadamu, Wedi Djamba alisema jukwaa hilo litaendelea
kupigania na kutetea misingi ya utawala unaojali na kulinda haki za
binadamu barani Afrika.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment