
Ni takriban miezi minne sasa tangu vyama vinne
vya upinzani nchini kupitia ushirikiano wao walioupa jina la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), kusaini makubaliano ya kushirikiana pamoja
na kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi zote zijazo.
Umoja huo unaoundwa na vyama CUF, Chadema, NCCR- Mageuzi na NLD, unakabiliwa na kazi moja ngumu ya kufikia mwafaka wa kumpata mgombea urais, kabla filimbi ya uchaguzi kupulizwa. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanasema kabla ya kumpata mgombea mmoja, vyama hivyo vinne, vitalazimika kufanya uamuzi katika sera zao kabla ya kuja na jibu la mgombea kutoka chama kimojawapo atakayekuwa na sifa ya kupeperusha bendera kwa niaba ya umoja huo.
Umoja huo unaoundwa na vyama CUF, Chadema, NCCR- Mageuzi na NLD, unakabiliwa na kazi moja ngumu ya kufikia mwafaka wa kumpata mgombea urais, kabla filimbi ya uchaguzi kupulizwa. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanasema kabla ya kumpata mgombea mmoja, vyama hivyo vinne, vitalazimika kufanya uamuzi katika sera zao kabla ya kuja na jibu la mgombea kutoka chama kimojawapo atakayekuwa na sifa ya kupeperusha bendera kwa niaba ya umoja huo.
Kufikia hatua hiyo, changamoto kubwa inayoukabili
umoja huo ni namna ya kumpata mgombea wa urais atakayetoa upinzani
mkubwa zaidi kwa mgombea wa chama tawala.
Historia ya wanaoweza kugombea
Mpaka sasa aliyekuwa mgombea wa urais katika
uchaguzi wa mwaka 2010 kupitia Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye
anayeonekana kuwa anaweza kupata mtaji mkubwa wa kura. Matarajio haya yanahanikizwa na takwimu za
uchaguzi wa mwaka huo zinazoonyesha kuwa ndiye aliyepata kura nyingi
kulinganisha na wagombea wa vyama vingine vitatu ambavyo mwaka huu
vimeamua kujiunga pamoja kupitia Ukawa. Katika uchaguzi wa mwaka 2010,
Dk Slaa alipata asilimia 26.34 ya kura zote na kuweka rekodi ya upinzani
ikilinganishwa na wagombea wengine miongoni mwa wanaotajwa kuwania
nafasi hiyo ya Ukawa waliowawahi kugombea siku za nyuma.
Kwa CUF kuna kila dalili kuwa Profesa Ibrahim
Lipumba anaweza kupendekezwa kugombea kiti cha urais kupitia Ukawa.
Mgombea huyu si mgeni katika chaguzi, ameshiriki tangu mwaka 1995 bila
ya mafanikio.
Katika chaguzi nne zilizopita CUF kupitia Profesa
Lipumba kimekuwa katika mtiririko usioridhisha wa kupanda na kushuka
katika upataji wa kura za wananchi.
Katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka
1995, alipata kura 418,973, sawa na asilimia 6.43 ya kura zote na
kushika nafasi ya tatu akiwa nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM na Augustine
Mrema aliyegombea kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi.
Profesa Lipumba aliingia tena katika uchaguzi wa
mwaka 2000 na kushika nafasi ya pili baada ya kupata kura 1,329,007
(sawa na asilimia 16.26) akiwa nyuma ya Mkapa na uchaguzi uliofuata
alipata kura 1,327,125 (sawa na asilimia 11.68) kabla ya kushuka tena
mwaka 2010 alipopata kura 695,667 (8.06%).
Kigogo mwingine wa Ukawa ni Mwenyekiti wa NCCR-
Mageuzi, James Mbatia. Hata hivyo, hajaonekana kuleta upinzani kwani
hana historia ya kugombea urais, licha ya kuwa chama chake kimepata
kusimamisha mgombea wa nafasi mara tatu.
CHANZO: MWANANCHI
Ukiachilia mwaka 1995 aliposimama Augustino Mrema na kuibuka na
idadi kubwa ya kura pengine kuliko mgombea yeyote wa upinzani, NCCR
imewahi kuwasimamisha aliyekuwa kada na nguzo muhimu ya chama, Marehemu
Dk Sengondo Mvungi mwaka 2005 na baadaye mwaka 2010 kikamsimamisha
Hashim Rungwe. Wagombea wote hawa walipogombea urais kupitia
NCCR-Mageuzi, hawakuonekana kuleta ushindani wowote wenye kukipa chama
hicho mtaji wa kuanzia.
Chama kingine kilichopo kwenye umoja huo na
ambacho hakina historia ya ushindani ni NLD chini ya mwenyekiti wake, Dk
Emmanuel Makaidi ambaye naye ushiriki wake katika siasa si wa
ushindani.
Nani anapewa nafasi Ukawa?
Tayari wafuasi wengi wa kambi ya upinzani
nchini wanaielekeza kete yao kwa Chadema na mgombea wake aliyejizolea
umaarufu Dk Wilbroad Slaa. Miezi kadhaa iliyopita Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), David Kafulila alianza kumpigia chapuo Dk Slaa kuwa ni
mtu anayefaa na kwamba ili kuleta ushindani Ukawa inapaswa kumsimamisha.
Kwa maoni yake, siyo kwamba viongozi au wanachama
wa vyama vingine vinavyounda Ukawa hawana sifa za kuwania nafasi hiyo ya
juu katika siasa nchini, bali Dk Slaa ana nafasi kubwa kwa sababu
anakubalika zaidi katika jamii na ana sifa ya ziada ya kuwa na mvuto.
“Bado namwona Dk Slaa kuwa ana nafasi kubwa kuliko wenzake. Kwa vyovyote
itakavyokuwa yeye anawazidi wenzake kwa kukubalika,” anasema Kafulila
na kuongeza: ‘’Siyo kama wengine hawawezi, ila si kila mwenye
mvuto anaweza kuongoza na wala si kila mwenye sifa anayeweza kuwa na
mvuto. Pia si kila anayekubalika anaweza na siyo kila anayeweza
anakubalika.’’
Kauli ya Profesa Lipumba
Profesa Lipumba anasema utaratibu wa kumpata
mgombea mgombea wa Ukawa bado unaendelea na kuwa lazima atoke kwenye
moja kati ya vyama vinne vinavyounda umoja huo.
Anaongeza kuwa endapo makubaliano yatakuja na
uamuzi wa kumpitisha mgombea urais kutoka nje ya chama chake, yeye na
chama chake watamuunga mkono yoyote atakayeteuliwa. “Tutamuunga mkono yeyote atakayechaguliwa ndani au
nje ya CUF, tutafanya hivi kwasababu bila ukawa kuiondoa CCM madarakani
itakuwa kazi ni ngumu,” anaeleza.
Michakato yaendelea ndani ya vyama
Wakati vyama vingine vinavyounda Ukawa,
vikiendelea na mchakato wa kutafuta jina litakalopendekezwa kugombea
kiti cha urais, Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi
amesema, tayari chama chake kimeshapendekeza jina lake kuwa miongoni mwa
watu watakaoshindanishwa kwenye kinyang’anyiro hicho. Chama cha NCCR-Mageuzi nacho kimeshamtangaza
mgombea wake ambaye wanaamini anavyo vigezo stahiki vya kusimama kuwania
nafasi hiyo nyeti nchini.
Aliyeteuliwa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk George Kahangwa. Huyu ni msomi wa fani ya elimu hususan
katika maeneo ya uongozi, sera na mipango. “Tulikaa kwenye vikao halali vya chama na kuamua
kwa pamoja kupitisha jina la Dk George Kahangwa kuwa mgombea urais kwa
tiketi ya NCCR-Mageuzi, jambo ambalo limetufanya tuutangazie umma,
anasema Mwenyekiti wa vijana wa NCCR-Mageuzi, Deo Meck.
Historia ya nyuma
Uchaguzi Mkuu wa mwakani utakuwa wa Tano chini ya
Mfumo wa Vyama vingi uliorejeshwa nchini mwaka 1992. Tayari Chama cha
Mapinduzi-CCM kimetoa marais wawili mfululizo baada ya kushinda chaguzi
zote nne za 1995, 2000, 2005 na 2010. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanatoa nafasi
kubwa kwa upinzani kufanya vizuri katika uchaguzi huu endapo utaamua
kuunganisha nguvu na kumsimamisha mgombea mmoja mwenye ushawishi na
kumpigia debe dhidi ya CCM.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment