
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju.
Utata umegubika uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi
baada ya Serikali kutaka kuwasilisha ‘kinyemela’ muswada wa uanzishwaji
wa Mahakama hiyo, kwenye Mkutano huu wa 19 wa Bunge unaondelea mjini
Dodoma bila kuupitisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba,
Sheria na Utawala kama utaratibu unavyotaka.
Pamoja na utata huo, kwa mujibu wa ratiba ya Bunge iliyotolewa
jana, muswada huo utawasilishwa kwenye kikao cha mwisho cha Mkutano huu
Aprili Mosi, saa chache kabla ya hotuba ya Waziri Mkuu ya kuahirishwa
kwa Bunge. Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya Bunge, muswada huo utawasilishwa
Jumatano ya Aprili Mosi, mwaka huu baada ya kipindi cha maswali na
majibu na umewekwa kwenye Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2014.
Alipoulizwa na NIPASHE ikiwa muswada huo utapata nafasi ya
kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
George Masaju, alisema kwa kifupi: ‘Muulize Katibu wa Bunge, mimi
sipangi ratiba ya Bunge.’ Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, hakupatikana kwa maelezo kuwa yuko nje ya ofisi kikazi.
Alipoulizwa kuhusu msimamo wa Maaskofu wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania ambao wanapinga kuwasilishwa kwa muswada huo, alisema hawezi
kuzungumzia jambo hilo. Naye Waziri wa Uchukuzi ambaye pia anakaimu nafasi ya Waziri Mkuu,
Samuel Sitta, alisema kura ya maoni iko pale pale na kwamba msimamo wa
Maaskofu ‘hauna’ nguvu kwa kuwa nao wamegawanyika kwa maelezo kuwa wapo
wanaounga mkono kura ya maoni na wapo wanaopinga.
Alisema viongozi hao wa dini wanapaswa kuwaacha wananchi waamue
wenyewe kuhusu Katiba inayopendekezwa hivyo suala la Mahakama ya Kadhi
na Kura ya Maoni, linapaswa kuamuliwa na Watanzania wote. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala, Jasson
Rweikiza, aliliambia gazeti hili kwamba kamati yake haijapokea muswada
huo na kuupitia.
Akizungumza na NIPASHE jana, Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria,
Tundu Lissu, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala, alisema inashangaza serikali kutaka kuuwasilisha muswada huo
bungeni kinyemela bila kuuwasilisha kwenye Kamati. Alisema awali kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, Kamati ilipokea
maoni ya wadau mbalimbali, zikiwamo taasisi za Kiislamu na viongozi wa
dini za Kikristo, ambao walionyesha kasoro nyingi kwenye muswada na
hivyo Kamati iliiagiza serikali ikafanye marekebisho na kuyawasilisha
kwake kabla ya kupeleka bungeni.
“Sisi (Kamati), ndiyo wenye muswada na tulikuwa hatujakubaliana,
tukawaambia serikali tupate kwanza maridhiano ya jambo hili kwa sababu
tulipokea maoni ya wadau wengi ambao walibaini makosa na kasoro za
kitaalam; serikali ikaahidi kuyafanyia kazi lakini hadi leo hawajarudi
kwenye kamati kutuletea marekebisho, sasa tunashangaa wameuweka kwenye
ratiba ya Bunge,” alisema.
Alisema ni hatari kwa mambo yanayoweza kuligawa taifa kama
uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi na Katiba inayopendekezwa kufanywa kwa
hila na ubabe na kuishauri serikali ihakikishe wananchi wameelewa kwa
kina jambo hilo ili kuepuka mgawanyiko usio wa lazima. Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Ofisi za Bunge,
zinaeleza kuwa muswada huo unaweza kusomwa kwa mara ya pili ukiwa sehemu
ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa mwaka 2014.
Chanzo chetu kilieleza kuwa hata hivyo, kuwasilishwa kwa Muswada wa
Mhakama ya Kadhi kutategemea makubaliano kati ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusiana na
mambo gani yawasilishwe. Utata huo umeibuka takribani mwezi mmoja baada ya Serikali
kuuchomoa muswada huo bungeni kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge iliofanyika
Februari, kwa nia ya kutafuta maridhiano kwanza.
Aidha, taasisi 11 za Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania
ziliazimia kuwahamasisha wana jumuiya wake kususia Kura ya Maoni ya
Katiba Mpya hadi watakapopata uhakika wa kuwa na Mahakama ya Kadhi yenye
meno. Baada ya serikali kuuchomoa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala
ilikutana Dodoma na serikali iliomba muda wa kufanya maridhiano kabla ya
kuwasilishwa muswada huo kwenye Bunge hili.
Mbali ya maridhiano, Kamati hiyo ilitaka muswada huo uwasilishwe
wenyewe badala ya kuingizwa kwenye muswada wa marekebisho ya sheria
mbalimbali wa mwaka 2014, jambo ambalo hata hivyo, halijafanyika kwa
kuwa umewasilishwa ukiwa kwenye muswada wa sheria mbalimbali.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment