Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal,
akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala,
Raymond Mushi, juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali kwa waathirika
wa mafuriko eneo la Buguruni Kwa Mnyamani, jijini Dar es Salaam, wakati
alipotembelea eneo hilo jana.Zaidi ya wakazi 5,000 wa Buguruni kwa Mnyamani,
jijini Dar es Salaam hawana makazi kutokana na nyumba zao zaidi ya 500
kujaa maji. Idadi hiyo ilijulikana jana baada ya Makamu wa Rais Dk. Mohamed
Gharib Bilal, kutembelea eneo hilo lililoathiriwa na mvua zinazoendelea
kunyesha jijini humo.
Dk. Bilal ambaye aliongozana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond
Mushi, alisema serikali iko tayari kuwasaidia wakazi hao na kuahidi
kupeleka haraka kikosi cha maafa kutoka Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya
Waziri Mkuu kushughulikia tatizo hilo. Pamoja na kuwapa pole kwa kukumbwa na adha hiyo, Dk. Bilal aliahidi
pia kwamba serikali itapeleka dawa kwa ajili ya kupuliza katika maji
hayo ambayo yametuama.
Alisema kwa kuwa maji hayo ni machafu ni rahisi wakazi hao kupatwa na magonjwa.
MKUU WA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, naye jana
alitembelea maeneo hayo yaliyokumbwa na mafuriko na kusema serikali ipo
tayari kuwasaidia waathirika ikiwa watahitaji msaada. “Serikali tuko tayari kuwasaidia wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani
tena haraka endapo watasema wanahitaji msaada, kwa sababu tukio lao
halina uhusiano na lile la wakazi wa mabondeni ambao tumepiga kelele
sana kuhusu kuhama, lakini bado wanaendelea kukaidi,” alisema na
kuongeza: “Eneo la Buguruni halina historia ya mafuriko isipokuwa eneo lao
kujaa maji kumesababishwa na kuziba kwa bomba la kupitisha maji, hivyo
maji kupoteza mwelekeo na kusambaa katika makazi. Mpaka sasa uongozi wa
mtaa haujatueleza matatizo yao, lakini wakisema wanahitaji tuko tayari
kuwasaidia.”
Kadhalika, alisisitiza kuwa, serikali haitawajibika kwa kuwasaidia
wakazi wa mabondeni ambao wameendelea kukaidi agizo la serikali la
kuhama katika maeneo hayo. “Serikali tumesisitiza sana kuhusu wakazi wa mabondeni kuhama,
lakini wameendelea kukaidi. Ni lazima watambue kwamba serikali
haitawajibika kwa lolote endapo yatatokea maafa mengine kwa wakazi hao
kwa sababu tumepiga makelele sana na wale wastaarabu wamekwisha hama.
Kama yatatokea maafa wakaumia tutawatibu kama ajali lakini sio msaada
mwingine,” alisema.
Kuhusiana na jitihada za kuondoa maji Buguruni Mnyamani, Sadiki
alisema tayari wameomba msaada kutoka kwa kampuni ya Wachina ya Railway
Jianchang Engineering (CRJE) kusaidia kunyonya maji hayo. Pia alisema wameagiza mipira mingine ya kutolea maji hayo baada ya iliyokuwapo kuzidiwa nguvu.
Akizungumzia idadi ya watu waliokufa mpaka sasa, Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema waliokufa
kutokana na athari za mvua ni watu watano na kwamba watu wawili
waliokufa kwa kuangukiwa na nguzo, Kimara Baruti ilikuwa ni ajali ya
kawaida. “Idadi ya waliokufa kutokana na athari za mvua hadi sasa ni watano
na wale waliokufa juzi huko Kimara haikusababishwa na mvua isipokuwa
kuna mtu aligonga nguzo ya umeme na katika harakati za kutaka
kuwakimbia polisi aliita ndugu zake wamsaidie kutoa gari lake ndipo
walipigwa na shoti ambayo ilikuwa imesambaa kwenye maji,” alisema Kova.
Kova alisema bado Jeshi la Polisi linaendelea na doria katika eneo
lote la jiji kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
pamoja na Kikosi cha Zima Moto.
LIPUMBA ATOA POLE
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ni
miongoni mwa viongozi waliokwenda kuwatembelea waathirika hao na kutoa
msaada wa Sh. 500,000. Prof. Lipumba alisema ilitakiwa kutatua tatizo hilo mapema hata
kabla ya kutokea kwa sababu lilikuwa linajulikana hata katika serikali
ya mtaa.
Alisema majanga mengi nchini yanatokea kutokana na uzembe wa
uwajibikaji kuanzia serikali za mtaa hadi serikali kuu na kwamba ikiwa
kila moja kwa upande wake ingekuwa inawajibika ipasavyo matatizo kama
hayo yasingekuwa yanatokea. Alisema anasikitishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali kwa wakazi hao ambao mpaka sasa hawana chakula wala mahali pa kulala.
“Sifurahishwi na hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwasaidia
waathirika hawa, wamepata matatizo ni siku ya tatu sasa, watu hawana
mahali pa kulala, watoto na wanawake wanahangaika, lakini serikali
haijahangaika kufahamu wanaishije,” alisema Prof. Lipumba. Aliongeza: “Ni vema serikali ikaleta msaada wa haraka kuwasaidia
waathirika hawa, ikiwamo kuleta kikosi cha maafa kutoa msaada wa
haraka.”
MWENYEKITI WA MAAFA
Mwenyekiti wa Maafa wa mtaa huo, Ahmad Abdulfaris, alisema
wanashangaa hadi sasa hawajapatiwa msaada wowote wa kuhakikisha maji
hayo yanaondolewa japokuwa waliahidiwa kusaidiwa na ofisi ya mkuu wa
mkoa tangu Machi 20 yalipotokea. “Mkuu wa mkoa alikuja akasema wanaleta vifaa ambavyo vitaondoa maji
hayo, wameleta havijafanya kazi ikabidi waondoke na hadi sasa wanakuja
wanaondoka hawafanyi kazi yeyote, kwa kifupi hatujaona jitihada za dhati
za kushughulikia tatizo hili,” alisema.
Mpaka sasa watu watano wameshafariki kutokana na athari za mvua
zilizoanza kunyesha Machi 20, mwaka huu, mmoja akiangukiwa na nyumba,
mwingine kusombwa na maji hadi mto Mbezi na wengine watatu wakiangukiwa
na nguzo za umeme. Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agness
Kijazi, akizungumza juzi na NIPASHE, alisema mvua hizo zitaendelea
kunyesha kwa mfululizo kuanzia jana, leo na kesho.
Alisema mvua hizo zitanyesha katika ukanda wote wa Pwani, Tanga, Mtwara, Dar es Salaam, Lindi, Visiwa vya Unguja na Pemba. Alisema mvua hizo zitanyesha kwa saa 24 kwa ukubwa wa milimita zinazozidi 50.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment