Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuwa
mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Jukwaa la Viongozi wa Afrika na China
litakalofanyika jijini Arusha kuanzia Machi 27 hadi 31, mwaka huu. Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM), litahudhuriwa na nchi 43 kutoka Afrika na vyama 57
vya siasa, wafanyabiashara 32 kutoka nchi za Afrika, vijana 70 wa nchini
na vijana 50 kutoka nchini China.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sixtus Mapunda,
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema
lengo la Jukwaa hilo ni kuimarisha mahusiano baina ya Afrika na China
kwenye nyanja tofauti za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Alieleza kuwa pia jukwaa hilo litajadili maendeleo ya mahusiano
kati ya Afrika na China, ushiriki na uhusiano wa vijana katika maendeleo
na wajibu wa asasi zisizo za kiserikali katika kukuza mahusiano na
maendeleo kati ya Afrika na China. “Jukwaa hili ni la tatu kufanyika tangu lilipofanyika kwa mara ya
kwanza mwaka 2011 Windhoek, Namibia na kufuatiwa na la pili la mwaka
2012 Beijing, China, hivyo sisi tumepata fursa ya kuliandaa," alisema.
Alisema pia vijana hao watapata fursa ya kubadilishana mawazo na
wenzao na kuona namna ya kuzifikia fursa mbalimbali nchini na nje ya
nchi. Aidha, alisema Jukwaa hilo linatarajiwa kufungwa na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment