Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Mvutano mkubwa umeibuka kati ya Jeshi la Polisi na
vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kufuatia
kupotea kwa Mwenyekiti wao wa Vijana, George Mgoba, katika mazingira ya
utatanishi.
Hata hivyo, viongozi wa vijana hao wamehojiwa kwa zaidi ya saa nane
katika kituo cha polisi kati kwa kile polisi walichokiita walikuwa
wakizungumza nao kuhusu madai yao. Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti
wa Askari hao, Parali Kiwango, alisema mwenyekiti wao alipotea
Jumatatu, majira ya saa ya saa 3:00 nyumbani kwake Mabibo Royola.
Alisema tangu siku atoweke, hawana mawasiliano naye baada ya namba za
simu zake za mikononi kuwa zimezimwa.
Kiwango alisema kwa mujibu wa mke wake, Mgoba alipigiwa simu na mtu
ambaye hajafahamika akimtaka wakutane eneeo la Mabibo mwisho,
alipoondoka hakurejea tena. “Kwa mujibu wa mke wake anasema mtu huyo alijitambulisha kwa askari
mwenzake, lakini sisi hatukumpigia simu ya aina hiyo, tunajua vyombo
vya usalama vimehusika,” alisema Kiwango
Vijana hao waliomaliza mafunzo yao ya kijeshi katika kambi
mbalimbali za JKT nchini, wamekuwa wakidai kupewa ajira kulingana na
mafunzo waliyopewa. Hata hivyo, wametishia kuitisha maandamano ya siku tatu
yatakayoishia Ikulu ili kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete kusikiliza
kilio chao.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
akizungumza na NIPASHE ofisini kwake, alikana jeshi hilo kuhusika na
kupotea kwa Mgoba na aliahidi kutoa kauli kuhusu suala muda utakapofika. Viongozi wa vijana hao wamehojiwa na polisi kwa muda wa saa tisa kwa kile kinachoelezwa kuzima jaribio la mandamano.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Kiwango alisema walihojiwa
na maafisa wa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kuhusu madai ya wao kutaka kuandamana. Alisema mahojiano hayo yalianza kufanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi
hadi majira ya saa 7:00 mchana na kupewa mapumziko mafupi na illipofika
saa 8:00 waliitwa Ofisi ya Kova na kuhojiwa hadi saa 10 jioni
walipoachiwa. “Kiujumla sisi tulitoa maelezo yetu kwa nini tunataka kuandamana,
lakini tuliwaambia watuonyeshe mwenyekiti wetu na wamuachie haraka,”
alisema.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment