Mboni Mhita
Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wa
wakuu wa wilaya 12 na kuwateua wengine 27, akiwamo aliyekuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen na mjumbe wa Bunge la Katiba,
Paul Makonda ambaye aliingia kwenye mzozo na mawaziri wakuu wawili wa
zamani.
Katika uteuzi huo uliotangazwa jana na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda mjini hapa, katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la
Soka (TFF), Frederick Mwakalebela ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Wanging’ombe, huku wakuu wa wilaya 64 wakibadilishiwa vituo vyao vya
kazi. “Mabadiliko haya yamezingatia kuwapo nafasi 27
wazi zinazotokana na kufariki dunia kwa wakuu watatu wa wilaya, watano
kupandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa, saba kupangiwa majukumu mengine na
12 kutenguliwa uteuzi wao. Wakuu wa wilaya 42 wamebaki katika vituo
vyao,” alisema Pinda wakati akitangaza uteuzi huo.
Pinda alitangaza uteuzi huo jana alasiri na baadhi
ya wakuu wa wilaya ambao walibadilishiwa vituo walishangazwa na taarifa
za uhamisho huo, ambao umeelezewa na viongozi wa vyama vya upinzani
kuwa ni wa kufuja fedha za walipa kodi na unalenga kukiandaa chama hicho
kwa Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu ujao. “Yaani unanipongeza kwa nini?... mimi
nimehamishwa? Nimehamishiwa wapi?” alihoji mmoja wa wakuu wa wilaya
baada ya kupigiwa simu na Mwananchi, lakini akaomba asitajwe gazetini.
Katika uteuzi huo yumo Zelotte, ambaye ni kati ya
maofisa wachache wa Jeshi la Polisi kuteuliwa kushika nafasi za ukuu wa
wilaya na hivyo atalazimika kuacha kibarua cha fani yake na kwenda
Musoma. Zelotte anasifika kwa kufanikiwa kukamata vijana 11 waliokuwa
wakihusishwa na mazoezi ya kigaidi mkoani Mtwra mwaka 2013. Pia yumo Makonda, ambaye ameteuliwa kuwa mkuu mpya
wa Wilaya ya Kinondoni. Kiongozi huyo wa Umoja wa Vijana wa CCM
aliandikwa sana na vyombo vya habari wakati wa Bunge la Katiba kutokana
na kutoa maneno ya kumshambulia mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliyewasilisha Rasimu ya
Mabadiliko ya Katiba.
Kiongozi huyo wa UVCCM aliandikwa zaidi na vyombo
vya habari kutokana na kuhusishwa na vurugu zilizotokea Hoteli ya Blue
Pearl jijini Dar es Salaam wakati wa mdahalo wa Katiba Inayopendekezwa
akidaiwa kumshambulia mwilini Warioba, ambaye amewahi kuwa Waziri Mkuu
na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mwishoni mwa wiki iliyopita, makada wawili wa CCM,
John Guninita na Mgana Msindai walimwandikia kusudio la kumfungulia
mashtaka wakidai kuwa Makonda aliwadhalilisha kwa kuwaita kuwa vibara wa
Edward Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli na aliwahi kuwa Waziri
Mkuu.
Makonda aliwahi kuitisha mkutano na waandishi wa
habari na kumtuhumu Lowassa akidai kuwa anawatuma baadhi ya makada wa
chama hicho wanaokivuruga chama. Alidai kuwa Lowassa hawezi kuwa Rais wa
Tanzania na kwamba CCM haitafuti Rais pekee, bali mwenyekiti wake na
mbunge huyo wa Monduli hawezi kuongoza chama hicho kikongwe.
Waliotenguliwa
Ma-DC waliotenguliwa ni pamoja na Martha Umbulla
aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Kiteto, ambayo imekithiri kwa migogoro ya
ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Mgogoro huo umesababisha watu zaidi
ya 10 kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Wengine ni Fatma Kimario (Kisarawe) ambaye alihamishiwa wilaya
hiyo akitokea Igunga, baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni kudhalilishwa
na makada wa Chadema katika kampeni za uchaguzi mdogo. Wengine ambao uteuzi wao umetenguliwa ni James
Kisota Ole Millya aliyekuwa Wilaya ya Longido, Elias Wawa Lali
(Ngorongoro), Alfred Ernest Msovella (Kongwa) na Danny Makanga (Kasulu).
Pinda aliwataja wengine kuwa ni Elibariki Kingu
(Igunga), Dk Leticia Warioba (Iringa), Evarist Kalalu (Mufindi), Abihudi
Saideya (Momba), Khalid Mandia (Babati) na Elias Goroi (Rorya). Hata hivyo, Pinda alisema kutenguliwa uteuzi wa wakuu hao kunatokana na sababu za umri, kiafya na nyinginezo.
Wapya
Mbali na Makonda, Pinda aliwataja ma-DC wengine wapya kuwa ni Mwakalebela, anayekwenda Wilaya ya Wanging’ombe
mkoani Iringa, akiwa amesogezwa karibu na Jimbo la Iringa Mjini
alilogombea ubunge mwaka 2010, na ambaye anadaiwa kulinyemelea tena
mwaka huu. Akizungumzia uteuzi huo, Mwakalebela aliishukuru
Serikali kwa kumuona kwamba bado ana mchango wa kuisaidia nchi yake na
yuko tayari kuwatumikia wananchi. Mwakalebela alisema anataka kwanza kufika wilaya
hiyo na kujua changamoto kubwa zinazowakabili wananchi na baada ya hapo
anataka kuanza kuzitatua moja baada ya ngingine.
“Naijua hii wilaya lakini kwanza nataka kufika
huko kujua ni changamoto gani ambazo zinaikabili,” alisema Mwakalebela
ambaye alieleza kuwa hatazipa nafasi harakati zake za ubunge kwa sasa. “Nitaanza kuangalia tunawezaje kuzipatia ufumbuzi... kikubwa nawaomba wananchi wangu kunipa ushirikiano.”
Wengine wapya, kwa mujibu wa Pinda, ni mtangazaji
wa TBC, Shaaban Kissu (Kondoa), makamu mwenyekiti wa UVCCM, Mboni Mhita
(Mufindi), Mariam Mtima (Ruhangwa), Dk Jasmine Tiisike (Mpwapwa) na
Pololeti Mgema (Nachingwea). Wengine ni Fadhili Nkurlu (Misenyi), Felix Lyaniva (Rorya), Zainab Mbussi (Rungwe), Francis Mwonga (Bahi), Kanali Kimiang’ombe Nzoka, (Kiteto) na Husna Msangi (Handeni). Wapya wengine ni Emmanuel Uhaula (Tandahimba),
Hashim Mngandilwa (Ngorongoro), Mariam Juma (Lushoto), Thea Ntara
(Kyela), Ahmed Nammohe (Mbozi), Pili Moshi (Kwimba) na Mahmoud Kambona
(Simanjiro). Pinda, pia, aliwataja wengine wapya kuwa ni Zainab
Telack anayekwenda Sengerema, Bernard Nduta (Masasi), Zuhura Ally
(Uyui), Mwajuma Nyiruka (Misungwi) na Muftah Mohamed (Sengerema).
CHANZO: MWANANCHI
Waliopangiwa majukumu mengine
Kwa mujibu wa Pinda, waliopangiwa majukumu mengine
ambao ni Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo, aliyekuwa Simanjiro, Kanali
Ngemela Lubinga (Mlele), Juma Madaha (Ludewa) na Mercy Silla (Mkuranga).
Wengine ni Ahmed Kipozi (Bagamoyo), Mrisho Gambo (Korogwe) na Elinas Pallangyo (Rombo).
Waliobadilishwa vituo
Wakuu wa wilaya 64 waliobadilishwa vituo vya kazi
ili kuboresha utendaji wa kazi ni Nyerembe Munasa, anayetoka Arumeru
kwenda Mbeya), Jordan Rugimbana (Kinondoni-Morogoro) na Lephy Gembe
(Dodoma Mjini-Kilombero). Wengine ni Christopher Kangoye (Mpwapwa-Arusha),
Omar Shaban Kwaang’ (Kondoa-Karatu), Fransic Mtinga (Chemba-Muleba),
Elizabeth Mkwasa (Bahi-Dodoma), Agnes Hokororo (Ruangwa-Namtumbo),
Regina Chonjo (Nachingwea-Pangani) na Husna Mwilima (Mbogwe-Arumeru). Wengine ni Gerald Guninita (Kilolo-Kasulu), Zipporah Pangani (Bukoba-Igunga), Kanali Issa Njiku (Missenyi-Milele), Richard Mbeho (Boharamulo-Momba), Lembris Kipuyo (Muleba- Rombo) na Ramadhan Maneno (Kigoma-Chemba).
Venance Mwamoto (Kibondo-Kaliua), Gishuli Charles
(Buhigwe-Ikungi), Novatus Makunga (Hai-Moshi), Anatory Choya
(Mbulu-Ludewa), Christine Mndeme (Hanang’- Ulanga), Jacksone Msome
(Musoma-Bukoba), John Henjewele (Tarime-Kilosa) na Dk Norman Sigalla
(Mbeya-Songea). Pia wamo Dk Michael Kadeghe (Mbozi-Mbulu), Crispin
Meela (Rungwe-Babati), Magreth Malenga (Kyela-Nyasa), Said Amanzi
(Morogoro-Singida), Antony Mataka (Mvomero-Hai), Elias Tarimo
(Kilosa-Biharamulo) na Francis Miti (Ulanga-Hanang’). Wengine ni Hassan Masala (Kilombero-Kibondo), Angelina Mabula (Butiama-Iringa), Farida Mgomi (Masasi-Chamwino), Wilman Ndile (Mtwara-Kalambo), Ponsian Nyami (Tandahimba-Bariadi), Mariam Lugaila (Misungwi-Mbogwe) na Mary Tesha Onesmo (Ukerewe-Buhigwe).
Pia Karen Yunus anatoka Sengerema kwenda Magu),
Josephine Matiro (Makete-Shinyanga), Joseph Mkirikiti (Songea-Ukerewe),
Abdula Lutavi (Namtumbo-Tanga), Ernest Kahindi (Nyasa-Longido), Anna
Nyamubi (Shinyanga-Butiama), Rosemary Kirigini (Meatu-Maswa) na Abdallah
Kihato (Maswa-Mkuranga). Erasto Sima (Bariadi-Meatu), Queen Mulozi
(Singida-Urambo), Yahaya Nawanda (Iramba- Lindi), Manju Msambya
(Ikungi-Ilemela), Saveli Maketta (Kaliua-Kigoma), Bituni Msangi
(Nzega-Kongwa), Lucy Mayenga (Uyui-Iramba), Majid Mwanga
(Lushoto-Bagamoyo) na Muhingo Rwehemamu (Handeni-Makete).
Pia Hafsa Mtasiwa anatoka Pangani kwenda Korogwe,
Dk Nassoro Hamid (Lindi-Mafia), Festo Kiswaga (Nanyumbu-Mvomero), Sauda
Mtondoo (Mafia Nanyumbu), Suleman Mzee (Kwimba-Kilolo), Esterina Kilasi
(Wanging’ombe-Muheza), Subira Mgalu (Muheza-Kisarawe) na Jacqueline
Liana, anayetoka Magu kwenda Nzega.
Wanasiasa wakosoa
Wakizungumzia uteuzi huo, wenyeviti wa Chadema na
CUF, Freeman Mbowe na Profesa Ibrahim Lipumba walisema hawaoni umuhimu
wa wakuu wa wilaya nchini na kuwa uteuzi huo unalenga kuandaa timu ya
uchakachuaji wakati wa Uchaguzi Mkuu na Kura ya Maoni ili kupitisha
Katiba Inayopendekezwa. “Hayo ni maandalizi ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Chadema tulishaeleza kuwa wakuu wa wilaya hawana umuhimu wowote katika
Taifa hili na wanaongeza gharama tu za Serikali,” alisema Mbowe.
Alieleza kuwa uteuzi wao hauzingatii uzoefu, sifa wala weledi na
kwa kuthibitisha hilo, wanapoteuliwa hakuna sehemu inayoeleza
wameteuliwa kwa kigezo kipi. “Haya ndiyo matatizo ya rais wa nchi kuwa na
mamlaka makubwa ya kikatiba ya kuteua kadri atakavyo. Nchi haiwezi
kupata maendeleo kwa kuwa na mambo ya namna hii. Uteuzi huu ni kama
kupeana zawadi tu,” alisema.
Naye Profesa Lipumba alisema: “Ukitazama utaona
kuwa waliochaguliwa ni makada wa CCM walioandaliwa kuchakachua Kura ya
Maoni na Uchaguzi Mkuu. Rais Kikwete anakwenda kumaliza muda wake. Sasa
wakuu wapya wa wilaya au mabadiliko ya kazi gani. “Watakwenda kufanya kazi gani mpya ambayo wengine wameishindwa, watasimamia jambo gani muhimu lililowekwa na Serikali?”
Alisema mamlaka ya rais katika uteuzi madhara yake ndiyo kama hayo kwa kuwa anaweka watu ambao watatekeleza matakwa yake. “Kikubwa ninachokiona juu ya uteuzi huu ni
wahusika kwenda kusimamia mchakato wa kupitisha wagombea wa CCM katika
Uchaguzi Mkuu, zaidi ya hapo hakuna jipya lolote watakalolifanya,”
alisema Lipumba.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment