Rais Jakaya Kikwete akishuhudia Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir 
(kushoto) akipeana mikono na aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Riek
 Machar  baada ya kuweka saini makubaliano ya kurejesha amani nchini 
mwao na ndani  chama Sudan People's Liberation Movement (SPLM) katika 
hafla iliyofanyika juzi mkoani Arusha.
Viongozi wa Chama tawala cha nchini 
Sudan Kusini, Sudan People Liberation Movement (SPLM) wametakiwa 
kuheshimu makubaliano 43 waliyosaini juzi usiku ili kusitishwa vita na 
kurejesha amani na kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo. Wito huo ulitolewa juzi na marais watatu wa Afrika
 Mashariki, Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais
 wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Chama cha SPLM kimegawanyika katika makundi matatu na kusababisha vita vya wenyewe tangu mwaka 2013.
Makubaliano hayo yalisainiwa saa tatu usiku baada 
ya majadiliano ya marais hao na viongozi wa makundi yanayopingana ndani 
ya chama hicho katika mkutano uliofanyika kwenye Hoteli ya Ngurdoto, 
Arusha na kumalizika saa sita usiku.
“Ili makubaliano haya yadumu, mnapaswa kwanza wote
 muwe na utashi wa kisiasa, mzungumze kila mnapoona kuna jambo 
linawakwaza katika kutekeleza maazimio haya,” alisema Kikwete. Alisema CCM na Chama cha African National Congress
 (ANC), wamekubaliana kushirikiana kutoa msaada wowote utakaohitajika 
katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.
Aliwataka viongozi hao kusitisha vita vinavyoendelea katika nchi yao ili iwe rahisi kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa. Rais Museveni alisema baada ya makubaliano 
yaliyosainiwa na makundi matatu ndani ya SPLM, lazima sasa yarejeshe 
umoja na mshikamano Sudan Kusini.
Alisema chanzo cha kugawanyika viongozi wakuu wa 
SPLM, akiwamo Rais wa Sudan Kusini ambaye pia ni mwenyekiti wa chama 
hicho, Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake, Dk Riek Machar ni 
kutofautiana kimtazamo. “Mgawanyiko wenu unatokana na kuwa na mitazamo 
tofauti katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini sasa 
baada ya majadiliano mmeweza kufikia mwafaka, hivyo hatutarajii kurejea 
kwenye mapigano,” alisema.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta aliwataka viongozi 
wa SPLM kurejea katika mazungumzo ya kuboresha chama kwa manufaa ya 
Sudan Kusini. “Leo ni faraja kwa wananchi wa Sudan Kusini na 
Waafrika wote, kwani mmefikia makubaliano yatakayorejesha amani ndani ya
 Sudan Kusini,” alisema.
Akizungumzia makubaliano hayo, Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, 
Cyril Ramaphosa aliwapongeza viongozi wa CCM kwa kufanikisha makubaliano
 hayo na anaamini sasa amani imepatikana.
Alisema mazungumzo hayo yalikuwa yanafuatiliwa na Afrika yote, hivyo hategemei maazimio yake yatashindwa kutekelezwa kwa wakati. “Nawapongeza CCM kwa kuendeleza kazi ya kusaka 
amani Afrika iliyokuwa inafanywa na hayati Julius Nyerere na leo 
mnaendelea kuthibitisha kuwa Tanzania ni kitovu cha kusaka amani ya 
Afrika,” alisema.
Kwa upande wao, Rais Kiir, Dr Machar na kiongozi 
wa kundi la viongozi waliokuwa wamefungwa, Dk Peter Njaba walieleza 
kuridhia makubaliano yote na kuyatekeleza. Akisoma baadhi ya makubaliano
 waliyosaini viongozi hao, Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana alisema 
ni pamoja na kuifanyia marekebisho Katiba ya SPLM, kutoa fursa kwa 
mwanachama yeyote wa SPLM kugombea uongozi, kufuata misingi ya 
demokrasia na utawala bora ndani ya SPLM.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment