Ikiwa imesalia 
miezi kumi kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kuwa na 
ushindani mkubwa, hadi sasa majimbo sita yako wazi baada ya wabunge 
wanaoyaongoza kutangaza kutogombea tena ubunge.
Ni wazi kuwa uamuzi wa wabunge hao, wengi wao 
wakiwa wameamua kupumzika baada ya kushikilia viti hivyo kwa vipindi 
zaidi ya viwili, utaibua ‘vita kali’, vikianzia ndani ya vyama wakati wa
 kura za maoni na baadaye baina ya vyama wakati wa kuomba ridhaa kwa 
wananchi. Mbunge aliyetangaza kuachia jimbo hivi karibuni ni
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa mbunge wa Katavi kwa vipindi 
vitatu kuanzia mwaka 2000 akisema anakwenda kufanya kitu kingine.
“Wapo ambao hawatagombea sababu wanataka kuwania 
urais. Wapo waliotangaza kutogombea sababu tu ya demokrasia na kutaka 
kuwapisha wengine. Hilo ni jambo zuri,” alisema Profesa wa Chuo Kikuu 
cha Ruaha, Gaudence Mpangala. Profesa Mpangala alikumbushia pendekezo 
lililokuwapo katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko
 ya Katiba ambayo ilipendekeza kuwa mwisho wa kugombea uwe vipindi 
vitatu. “Pendekezo lile lilikuwa zuri ili kuwaondoa 
wanaokaa madarakani zaidi ya miaka 50, ila wapo wanaotangaza kutogombea 
kwa sababu tu za kisiasa,” alisema.
Vyama vya upinzani pia safari hii vitakuwa na kazi
 ngumu ya kuteua wagombea baada ya kufikia makubaliano chini ya Umoja wa
 Katiba ya Wananchi (Ukawa) kusimamisha mgombea mmoja kutoka miongoni 
mwao katika ngazi zote kuanzia Serikali za Mitaa. Vyama vilivyo chini ya mwavuli huo ni 
NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, wakati chama kipya cha ACT - Tanzania
 kilionyesha nguvu katika uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa na 
kama hakitamaliza mgogoro, kinaweza kuwa tishio wakati wa kutafuta kura 
za wananchi utakapowadia.
Bernard Membe (Mtama)
“Unajua nimekuwa mbunge wenu kwa vipindi vitatu. 
Hivi leo ninawaaga rasmi kuwa sitagombea tena nafasi hii ya ubunge,” 
alisema Membe katika hafla ya Mwaka Mpya aliyoandaa nyumbani kwake 
Januari, 2013. Membe ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa 
kutaka kuwania urais, ingawa amekuwa akieleza kuwa anasubiri 
“kuoteshwa”. Iwapo atajitosa kugombea kuwania nafasi hiyo ya juu nchini,
 jimbo hilo litabaki wazi na tayari linawaniwa na kiongozi mmoja wa juu 
wa CCM. 
Hezekiah Chibulunje (Chilonwa)
Kiongozi huyo alitumia staili nyingine kutangaza 
uamuzi huo. Alichagua Desemba 26, mwaka jana kufanya ibada ya kumshukuru
 Mungu kwa kumwezesha kuwa Mbunge wa Chilonwa tangu 1995 na akatangaza 
kutogombea kwa maelezo kuwa umefika wakati wa kupumzika na kuwapisha 
wengine. Chibulunje amewahi kuwa Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula; Viwanda na Biashara; Kazi; Miundombinu na Ushirika na Masoko. “Katika nafasi hizi zote za ubunge na unaibu waziri, sijawahi kupata misukosuko,” alisema.
Mizengo Pinda (Katavi)
Agosti 17, 2010, Waziri Mkuu Pinda, ambaye tayari 
ameshatangaza nia ya kugombea urais kimyakimya, alieleza kwa mara ya 
kwanza kuwa hatagombea tena ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, 
kauli ambayo wakati huo haikuhusishwa na mbio za urais na aliirudia hivi
 karibuni katika mkutano wa hadhara jimboni kwake akisema muda wa kuwa 
mbunge umetosha na sasa anatafuta kitu kingine cha kufanya. Awali, alisema mwaka 2010 ndiyo ungekuwa mara yake
 ya mwisho kugombea ubunge katika jimbo hilo, kauli aliyoitoa kwenye 
Ukumbi wa Katavi Resort, Mpanda wakati wa sherehe ya kumuaga aliyekuwa 
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, John Mzurikwao, aliyekuwa akihamishiwa Wilaya 
ya Sumbawanga.
Deogratias Ntukamazina (Ngara)
Mbunge huyo aliwaeleza wapigakura nyumbani kwake Ngara kuwa anahitaji kupumzika baada ya kukamilisha kazi yake. Alisema wakati akiingia madarakani mwaka 2010, 
aliwaahidi wananchi wa Ngara kupata umeme hadi vijijini na kwamba kazi 
hiyo ameifanya kwa kiwango kikubwa.
Anne Makinda (Njombe Kusini)
CHANZO: MWANANCHI
Kwa nyakati tofauti, Spika Makinda ambaye amekuwa mbunge wa 
kuteuliwa tangu 1975 kabla ya kuchaguliwa kushika ubunge wa Njombe 
Kusini mwaka 1995, amekaririwa na vyombo vya habari akisema mwaka huu 
hatagombea tena. Makinda amewahi kushika nafasi za ukuu wa mkoa, uwaziri
 na unaibu spika.
Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini)
Mbunge ambaye ameachia ngazi kwa staili ya pekee 
ni Zitto, ambaye awali, alionekana kuwa na nia ya kugombea urais lakini 
nia yake hiyo ilikwama kutokana na Katiba ya sasa na Katiba 
Inayopendekezwa kutaja umri wa mgombea urais kuwa ni kuanzia miaka 40. 
Mwaka huu Zitto anatimiza 39. Lakini, mbunge huyo kijana ameamua kutogombea 
Kigoma Kaskazini ambako ameongoza kwa vipindi viwili, lakini atagombea 
jimbo la Kigoma Mjini ambalo kwa sasa linaongozwa na Peter Serukamba 
(CCM).
Hamad Rashid Mohammed (Wawi)
Kwa upande wake, Hamad ambaye kwa sasa ana mgogoro
 na chama chake cha CUF ambao umewafikisha mahakamani, amesema mara 
kadhaa kuwa hatarudi jimboni kwake Wawi, Pemba. Sasa anawania urais 
kupitia ADC.

No comments:
Post a Comment