Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

WANAFUNZI 438,960 KUANZA KIDATO CHA KWANZA JANUARI

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Kassim Majaliwa. Wanafunzi 438,960 (97.23%)  wamechaguliwa katika awamu ya kwanza kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza katika shule za serikali Januari, 2015.
Idadi hiyo ni kati ya wanafunzi 451,392 waliofaulu mitihani hiyo iliyofanyika mwaka huu na watajiunga katika shule za sekondari za serikali 3,517. Jumla ya wanafunzi 792,122 sawa na asilimia 98.02 walifanya mitihani ya kumaliza darasa la saba mwaka 2014.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa (pichani), alisema idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kijiunga kidato cha kwanza imeongezeka kwa asilimia 1.08 na kwamba mwaka jana waliochaguliwa walikuwa asilimia 96.3.
Hata hivyo, wanafunzi 12,432 katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mtwara na Katavi, licha ya kufaulu masomo yao,  wameshindwa kujiunga na sekondari kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Majaliwa aliziagiza Halmashauri za mikoa hiyo kuhakikisha zinakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi waliokosa fursa ya masomo katika awamu kwanza waweze kujiunga na kidato cha kwanza kabla ya Machi, 2015.
Alisema katika idadi ya wanafunzi  hao waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza wasichana ni 219,996 na  wavulana ni 218, 964. Aliwataka wadau mbalimbali kushirikiana na Halmashauri nchini ili  kuhakikisha wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza wanasoma na kumaliza masomo yao. Alisema wanafunzi wanne wamefutiwa matokeo yao kutokana na sababu mbalimbakli ikiwamo udanganyifu ikilinganishwa na wanafunzi 13 mwaka 2013.
Kuhusu shule ambazo hazina vyumba vya maabara ama kutokamilika, Majaliwa alisema Serikali imetenga Sh. milioni 15 kwa shule 75 ambazo maabara hazijakamilika ili kukamilisha ili  wanafunzi waweze kusoma masomo ya sayansi.
Katika kupambana na ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi, Majaliwa alisema Serikali inawasomesha mafunzo maalum kwa miaka miwili wanafunzi 2,000 waliomaliza kidato cha nne kwa masomo ya sayansi, ambao walikosa nafasi ya kuendelea na masomo ili waweze kufundisha. Alisema wanasoma masomo ya sayansi kidato cha tano na sita kwa mwaka mmoja na kozi maalum ambayo watapata cheti cha diploma ili kufundisha masomo ya sayansi katika shule za serikali zenye upungufu wa walimu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: