
Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA),
wamemchagua Daniel Kidega kuwa spika wao kuziba nafasi iliyoachwa wazi
baada ya Dk Margaret Nantongo Zziwa, kung’olewa Jumatano wiki hii.
Kung’olewa kwa Spika Dk Zziwa kulikuja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Sheria, Kanuni na Haki za Wabunge, Frederic Ngenzebuhoro, kuwasilisha
taarifa ya uchunguzi bungeni ambayo iliweka hadharani ushahidi wa tuhuma
za ubadhirifu, upendeleo, ubabe na dharau kwa wabunge na watumishi wa
bunge hilo dhidi yake.Katika uchaguzi huo uliofanyika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki jijini hapa jana, Kidega alipita baada ya mgombea mwenzake Chris Okumu Opoka kujitoa katika kinyang’anyiro hicho. Awali kulikuwa wabunge waliotarajiwa kugombea ni Mike Kennedy Sebalu na Suzan Nakawuki, ambao hata hivyo hawakuchukua fomu. Kidega atakuwa na majukumu ya kuongoza na kusimamia shughuli zote za bunge na kamati zake na kusimamia utaratibu wa kuongoza chombo hicho kwa mujibu wa kanuni za bunge hilo.
Baada ya Dk. Zziwa kung’olewa katika nafasi yake, Uganda ambayo kwa mujibu wa utaratibu wa mzunguko ndiyo inayopaswa kutoa Spika ilipewa muda wa saa 48 kujaza nafasi hiyo, suala ambalo wabunge walifanikiwa kuziba nafasi hiyo jana. Wakati Spika wa zamani aking’olewa hakuwepo bungeni, uamuzi uliochukuliwa baada ya kupata kura 36 dhidi ya 39 za wabunge waliopita kura. Wabunge wawili walipiga kura za kukataa kumng’oa wakati kura moja haikupigwa. Dk Zziwa aliyechakuliwa kushika wadhifa wa Uspika Juni 2012, sasa atabakia kuwa mbunge wa kawaida hadi bunge hilo litakapomaliza muda wake mwaka 2017.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment