
Ubora wa bidhaa huvutia wateja na kumhakikishia mapato mazuri mjasiriamali.
     Siku zinakwenda kasi kwa namna ya ajabu leo ni Ijumaa ya kwanza ya mwezi huu wa kumi na mbili na kwa sasa, wapo ambao wameshaanza kufanya maandalizi mbalimbali kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka. Maandalizi ya safari mbalimbali yameanza!
Wakati wajasiriamali wengine wameanza maandalizi ya sikukuu za mwisho wa mwaka, leo natoa mwito kwa wajasiriamali kutumia mwezi huu wa kumi na mbili kufanya tathmini ya biashara zao ili kuweza kupima mafanikio waliyoweza kuyapata.
Leo katika kona hii ya mjasiriamali tuone baadhi ya njia bora za kupima mafanikio katika biashara. Inashauriwa kwa lolote unalofanya lazima ufike mahali, ufanye tathmini ili kuweza kujua umefanikiwa ama hujafanikiwa na nini kiwe kipaumbele kwa wakati ujao.
Tukiwa tumeanza mwezi wa mwisho katika mwaka huu 2014 na wakati tunaelekea mwishoni mwa mwaka, ni kipindi cha wewe mjasiriamali kukaa chini na kupima kile ulichofanya mwaka huu kama ulifanikiwa ama hukufanikiwa na kwa kiasi gani.
Baada ya mihangaiko ya hapa na pale, kule na huko wakati mwingine kushindwa hata kulala au kuhatarisha maisha yako katika safari mbalimbali, jiulize je, wewe ni mmoja kati ya wajasiriamali ambao wanaweza kusimama na kusema mwaka huu wamefanikiwa?
Lazima ifike mahali ujifanyie tathmini ya kile amabacho umefanya kwa mwaka mzima, kama ambavyo wanafunzi hupimwa kwa kupewa mitihani mwishoni mwa mihula ya masomo, ndivyo ilivyo kwa mjasiriamali kukaa chini na kujipima wewe mwenyewe.
Tunapozungumzia mafanikio katika biashara yafaa kutofautisha na ile hali ya wewe kukidhi mahitaji yako ya msingi kama vile chakula, mavazi, malazi na matibabu. Kumbuka hata wale ambao si wajasiriamali wanaweza kukidhi mahitaji haya ya msingi.
Lakini kwa mjasiriamali kupima mafanikio ni kuangalia mtiririko mzima wa kile ambacho umekifanya kwa kipindi kizima cha mwaka. Njia za kupima mafanikio ni nyingi, zifuatazo ni baadhi ya njia hizo unazoweza kuzitumia katika kujitathmini.
Njia ya kwanza ya kupima mafanikio katika biashara yako ni uwapo wako katika biashara (business survival). Jiulize je, ni kwa muda gani biashara yako imedumu tangu ulipoianzisha ? Je, imesimama? Unajifananisha vipi na washindani wako na soko ulilomo?
Uwapo wako na wewe kuendelea kufanya kile ambacho uliamua kukifanya katika ubora uliotamani ni kipimo kizuri cha kama umefanikiwa ama la. Hii ni kutokana na kwamba biashara nyingi hufa baada ya muda mfupi kwa kushindwa kuhimili mikiki.
Njia ya pili ya kupima mafanikio katika biashara yako ni kupima ukubwa wa mauzo (sales volume). Je, mauzo yako kwa kipindi cha mwaka huu unaoisha yamekuwaje ? Je, unayaelezeaje mauzo yako ukilinganisha na ukubwa wa shughuli unazofanya ?
Je, mtiririko wa mauzo katika biashara yako ulikuwaje ? Je, mauzo yamekuwa yakiongezeka au yakipungua au hayaeleweki? Ni kutokana na mauzo mazuri yanayoweza kutoa mwelekeo mzuri wa kupata mapato mazuri zaidi.
Njia ya tatu ya kupima mafanikio katika biashara yako ni tathmini ya faida. Wengi wanapoulizwa kama biashara imefanikiwa ama la, la kwanza kufikiria ni juu ya faida wanayopata, lakini pia kuna haja ya kujiuliza baadhi ya maswali juu ya faida.
Jaribu kujiuliza kama faida yako imekuwa ikiongezeka au ikipungua na kwa kiwango gani? Je, unafikiri faida uliyopata ni faida stahili ya kile unachofanya ama la. Hii ni kutokana na kwamba faida nyingine hazina uwiano na kile kinachofanyika.
Njia ya nne ya kupima mafanikio ya biashara ni uwezo wa kuongeza mali katika biashara yako (asset acquisition). Je, biashara yako imeweza kuongeza mali kiasi gani katika kipindi chote cha mwaka huu 2014 au mali zimetaifishwa kulipia madeni?
Uwezo wa biashara kujiongezea mali ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya kibiashara ni njia mojawapo ya kupima mafanikio katika hicho ambacho umekifanya kama mjasiriamali, katika kipindi chote cha mwaka. Je, biashara yako imeweza kumiliki vitendea kazi gani?
Wapo wajasiriamali ambao ukiongea nao watakwambia biashara zao haziwaangushi kwa kuwatengenezea faida nzuri, lakini ukienda katika biashara zao utakuta wanakosa baadhi ya mali ambazo zingeweza kurahisisha utendaji kazi na kuwawezesha kupata faida zaidi.
Njia tano ya kupima mafanikio katika biashara yako ni uwezo wa kudhibiti madeni na matumizi katika kuendesha biashara yako. Baadhi ya wajasiriamali wameshindwa kumudu biashara kutokana na kuelemewa na madeni na gharama za uendeshaji.
Wakati ulifikiria kujitengenezea faida nzuri katika biashara yako, je, ulikumbuka kujenga nidhamu ya kudhibiti madeni na matumizi ya biashara yako? Je, kwa mwaka huu ulikopa kwa hitaji maalum au ulifuata mkumbo ? Je matumizi yako yalikuwa yale ya lazima au?
Kwa mfano wapo wajasiriamali ambao wameshindwa kuendelea na biashara zao kutokana na mizigo ya madeni. Saccos, benki na Vicoba kote kapita kuomba mkopo, mwisho anashindwa kuhimili mizigo hii ya madeni na kufilisiwa, je umesimama wapi?
Vile vile kuna wale ambao katika kuendesha biashara zao hawaangalii juu ya matumizi yasio ya lazima katika biashara zao. Wanafika mahali wanashindwa kutofautisha matumizi binafsi na yale ya biashara, jiulize kwa mwaka huu mtaji wako umesalimika?
Njia ya sita ya kupima mafanikio katika biashara yako ni kupima ukuaji wa mtaji wako. Kukua kwa mtaji wako uliokuwezesha kufanya hicho unachofanya ni kielelezo cha wewe kufanikiwa katika biashara yako, kama mtaji haujakua jiulize kwa nini mtaji haukui?
Wapo wajasiriamali ambao miaka nenda miaka rudi wamekuwa hawapigi hatua na mitaji yao haikui, lakini kila kukicha wanaonekana wako ‘bize’. Biashara itafanya vizuri na kufanikiwa iwapo tu mjasiriamali una nidhamu ya kulinda na kukuza mtaji wako.
Mjasiriamali anaweza kujiuliza ikiwa alianza na mtaji mdogo katika biashara yake ni kwa namna gani ataweza kulinda mtaji huo. Napenda kuwapa moyo kuwa, kuna njia mbalimbali za kulinda na kukuza mitaji ambazo tutaziona katika makala za usoni.
Njia ya saba ya kupima mafanikio katika biashara yako ni kupima juu ya ongezeko la wateja. Pamoja na kupata faida, je, umepata ongezeko la wateja katika biashara yako mwaka huu ukifananisha na kipindi kingine cha biashara ?
Wateja ni msingi wa mafanikio yoyote katika biashara, bila wateja hakuna litakalofanyika hivyo ongezeko la wateja katika biashara yako ni ishara nzuri kwamba kumekuwa na mwamko mzuri wa wateja juu ya kile unachofanya katika biashara yako.
Tatizo kubwa lililopo kati ya wajasiriamali wengi ni yale mazoea ya kupenda kuhesabu hela zaidi na kutopenda kufanya tathmini ya wateja ili kuweza kujua wateja ambao wameweza kufika kwenye biashara zao, yafaa kufahamu wale waliokuunga mkono.
Unapokuwa na utaratibu wa kufanya tathmini ya wateja waliofika katika biashara yako, utakuwa katika nafasi ya kufanya tathmini ya kujua kwa nini wamekuja kwako na kutafuta njia bora za kuweza kuwadumisha katika kile unachofanya.
Pamoja na kupima juu ya ongezeko la wateja wako katika kile unachofanya, yafaa pia kufanya tathmini ya kwa namna gani uliweza kuwaridhisha wateja wako. Kuridhika kwa wateja ni ishara ya kuwa biashara yako inayaelewa na kukidhi mahitaji ya wateja.
Kuwa na uwezo wa kuwaridhisha wateja wako kutasaidia biashara yako kueleweka vema miongoni mwa wateja wengine ambao si wako. Mteja aliyeridhika atakusaidia kutoa neno zuri kwa wengine na hivyo kufanya biashara yako iendelee.
Jiulize kwa namna gani biashara yako ingeweza kuendelea bila kuwa na wateja ili kuweza kukidhi mahitaji yao. Kumbuka chochote unachofanya kifanye katika namna bora ya kuweza kukidhi mahitaji ya wateja, kumbuka mteja hakosei mteja ni mfalme!
Mwisho mpendwa mjasiriamali ni muhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote na hasa kwa kuweza kutufikisha hapa tulipofika, tumuombe ili tuweze kumaliza mwaka huu salama. Kumbuka hata magumu uliyokutana nayo yawe changamoto ya kujipanga upya.
Karibu juma lijalo kwa mada nyingine ya namna bora ya kuendeleza biashara. Mwandishi ni Mshauri wa Biashara anayepatikana kwa Simu: 0754/ 0715 363800 au kwa barua pepe kupitia james@nikuze.com
CHANZO:
     NIPASHE
    

No comments:
Post a Comment