Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kama hali ya kuwaengua wagombea wa chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa itaendelea kama ilivyo sasa, basi wataupinga uchaguzi huo mahakamani.
Mbowe alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa operesheni mshikemshike mzizima uliofanyika Vijibweni Kigamboni.
“Tangu kampeni zianze kumekuwa na tabia ya kuengua
 wagombea wetu kiholela. Tumeshaweka angalizo mahakamani na kama hali 
ikiendelea hivyo tutaupinga uchaguzi mahakamani.”
Alisema baada ya kuibuka kwa tabia ya wagombea 
kuenguliwa aliwasiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimsihi alitizame
 kwa kina suala hilo kwa sababu wagombea walienguliwa kimakosa.
“Alisema atalifanyia kazi lakini naona bado hali 
hiyo inaendelea na alisema atazungumza na Katibu Mkuu wa CCM, 
Abdulrahman Kinana kuhusu jambo hili.
Nilipowasiliana naye mara ya pili alisema kama 
tunataka ushindi uchaguzi uwe wa haki. Kuona hivyo tumekwenda kutoa 
angalizo mahakamani,” alisema.
Aliongeza, “Tukutane katika uchaguzi na tuone nani
 ni bingwa kati ya CCM na Ukawa baada ya kutumia njia za mkato kama wao 
wanavyofanya.
Hata sisi hatutaki ushindi wa dezo ila wakitumia 
dola kutuyumbisha kamwe hatutokubali maana polisi wamekuwa wakitumika 
kama mawakala wa uchaguzi. Hilo halitakubalika.”
Aliwataka wananchi kutokaa mbali na vituo vya 
kupigia kura mara baada ya kuwachagua viongozi wanaowataka huku 
akisisitiza, “Msikubali kura zikahesabiwe sehemu nyingine 
watazichakachua.
Hata katika sheria za Uchaguzi hakuna sehemu 
inayosema baada ya kupiga kura, mpigakura anatakiwa kukaa umbali wa mita
 100 kutoka katika kituo cha kupiga kura. Tumeweka mawakala nchi nzima 
kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.”
Alisema hakuna dhambi mbaya kama wananchi 
kushindwa kuleta mapinduzi ndani ya nchi yao, hasa nchi kama Tanzania 
ambayo ina kila aina ya umasikini.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment