Shirika la Kimarekani la Uchumi (GFI) limetoa
ripoti mpya na kusema kuwa Tanzania imepoteza jumla ya Dola 1,762
milioni kuanzia mwaka 2011 hadi 2013.
Ripoti hiyo iliyotolewa Desemba mwaka huu,
inaonyesha kuwa Tanzania imekuwa sugu kwa kupoteza kiasi kikubwa kila
mwaka na kwa mwaka 2010, kiasi cha Dola 1,356 milioni kilipotea wakati
Dola 613 milioni zilipotea mwaka 2011 na Dola 717 milioni mwaka 2012.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema tatizo la
udanganyifu katika ankara za malipo ndilo lililotawala zaidi nchini na
kusema linafanyiwa kazi na mamlaka husika.
Mkuya alisema Tanzania inapoteza fedha nyingi
zaidi kutokana na udanganyifu katika ankara za malipo ya kibiashara,
mchezo ambao umekuwa ukifanywa na raia wa China ambao ankara zao za
malipo huonyesha kuwa wameingiza mzigo mkubwa nchini lakini ukifika
katika Bandari ya Dar es Salaam, huonekana mzigo kidogo. “Kutokana na hali hiyo, mfumo wa uingizaji wa
mizigo unaboreshwa na tutakuwa tukifuatilia idadi ya mzigo kamili kule
ulikotoka, inatushangaza kuona kinacholetwa nyumbani ni kidogo lakini
kule kimetoka kikubwa,” alisema.
Kuhusu fedha chafu zinazofichwa katika akaunti za
nje, Mkuya alisema tayari Tanzania imeshaingia katika makundi ya nchi
ambazo zitajumuika kuhakiki mifumo ya kifedha. “Hii itatusaidia kupata taarifa za uhamishwaji wa fedha unaofanyika mara kwa mara,” alisema. Hapa nchini zipo kesi za kampuni zinazofanya kazi
na kudai kupata hasara kwa miaka mingi na kuficha faida waliyoipata ili
kukwepa kodi.
Mapato yanavyopotea
Udanganyifu katika ankara za kibiashara ili
kukwepa kodi hufanyika mathalan, mwekezaji wa Asia aliye nchini anaweza
kununua gari kutoka Marekani kwa Dola milioni moja na anapoliingiza
huandika ankara ya uongo ya ununuzi kuwa amelinunua kwa Dola 1.5
milioni. Zile Dola milioni 5, huzipeleka katika akaunti za nje ya nchi. Kadhalika, wahalifu hao wanaweza kutumia mwanya wa
motisha wa kodi ambao hutolewa kwa wafanyabiashara wa ndani
wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi. Wahalifu hutumia mwanya huo kwa
kuongeza idadi ya uongo ya bidhaa wanazosafirisha. Wafanyakazi wa umma, kutumia kampuni za siri kuhamisha fedha katika akaunti za nje.
Rais wa GFI, Raymond Baker alisema ripoti hiyo
inaonyesha kuwa udanganyifu katika ankara za mapato ndicho chanzo
kikubwa kinachoangamiza uchumi katika nchi zinazoendelea. “Mtiririko huu unapoteza fedha nyingi kiasi kwamba
unazidi hata fedha ambazo wahisani wanazisaidia nchi hizi, ni mienendo
ambayo inahamisha matrilioni ya Dola za Marekani kwa mwaka kutoka katika
nchi hizi maskini,” alisema Baker.
Kwa Afrika Mashariki, Tanzania ilishika nafasi ya
pili baada ya Uganda ambayo iliongoza kwa kupoteza Dola 713 milioni kwa
mwaka 2013 wakati Kenya ilihamisha fedha hizo kiasi cha Dola 86 milioni.
Kadhalika, ripoti hiyo inaeleza kuwa nchi zilizo
Kusini mwa Jangwa la Sahara zimevunja rekodi kwa kupoteza kiasi kikubwa
cha fedha ambacho hakiendani na uchumi wao.
Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara zilipoteza
kiasi cha Dola 991.2 bilioni kwa mwaka 2013 jambo ambalo linatishia
uchumi wa nchi hizo. Ripoti hiyo ilionyesha kuwa rushwa, uhalifu,
ukwepaji wa kodi na udanganyifu wa ankara za malipo unaongezeka kwa
asilimia 9.4 kila mwaka mara mbili zaidi ya pato la uchumi wa dunia
kwa mwaka.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment