Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Ijumaa(19.12.2014)ametia saini kuwa sheria
mswada wenye utata wenye lengo la kupambana na ugaidi na kusababisha
wabunge kutupiana ngumi bungeni na kuzusha madai kuwa unakiuka misingi
ya uhuru.
Kenyatta amesema ameridhishwa kwamba mswada huo umepitishwa na bunge
la taifa siku ya Alhamis na haukiuki katiba ya nchi hiyo. "Wasi wasi
wote uliooneshwa na wadau tofauti umeshughulikiwa na kamati zinazohusika
za bunge," amewaambia waandishi habari, na kuwataka Wakenya wote kusoma
sheria hiyo mpya na kuamua wao binafsi.
Madaraka makubwa
"Lengo lake ni moja - moja tu- kulinda maisha na mali za raia wote wa jamhuri ya Kenya," amesema rais Kenyatta. Sheria hiyo mpya inatoa kwa maafisa wa madaraka makubwa kuwasaka
watuhumiwa wa ugaidi na kuweka mipaka kwa uhuru wa vyombo vya habari
katika nchi ambayo tayari imeathirika na wimbi la mashambulio
yanayofanywa na kundi la al-Shabaab kutoka nchi Somalia lenye
mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda. Hatua hizo zenye utata zinaongeza muda wa polisi kuwashikilia
watuhumiwa wa ugaidi kutoka siku 90 za sasa hadi karibu mwaka mmoja na
kuongeza hukumu inayowakabili.
Waandishi habari wanalengwa
Wakati huo huo , waandishi habari wanaweza kukabiliwa na hukumu ya
hadi kifungo cha miaka mitatu iwapo ripoti zao zitaingilia uchunguzi ama
operesheni za usalama zinazohusika na ugaidi", ama iwapo watachapisha
picha za wahanga wa ugaidi bila ya ruhusa ya polisi. Serikali inadai kuwa hatua hizo ni muhimu kuweza kupambana na
wanamgambo na inasema mabadiliko ya katiba ya msingi, na kutoa kwa
mahakama nafasi kubwa zaidi kwa polisi na idara za usalama, ni sahihi
kikatiba.
Wapinzani wanapinga
Upinzani na makundi ya haki za binadamu , hata hivyo, wanakataa
mabadiliko hayo na kusema ni kisingizio na wanadai sheria hiyo
inahatarisha kuigeuza Kenya kuwa taifa la kipolisi.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki amesema
Marekani "inaiunga mkono kwa dhati Kenya katika juhudi zake za
kulishinda kundi la al-Shabaab na kuhakikisha usalama wa raia zake.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment