Social Icons

Pages

Friday, December 19, 2014

SERIKALI YASHAURIWA KUTOA RUZUKU KWA ASASI ZA MAZINGIRA

Dk. Binilith Mahenge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira)
Serikali kupitia ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), imeshauriwa kutenga bajeti kwa ajili  ya kuwezesha utendaji wenye ufanisi wa asasi za kutunza na kuhifadhi mazingira kutokana na umuhimu wake katika kupambana uharibifu wa mazingira.
Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira nchini (JET), Deodatus Mfugale, alisema wakati umefika kwa serikali kuthamini mchango wa asasi zisizokuwa za serikali zinazojihusisha na utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kuzipatia ruzuku ili zifanye shughuli zake kwa uhakika.
Alisema asasi hizo zina mchango mkubwa katika kusaidia juhudi za serikali za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira. “Kwa kweli kuna kila sababu ya taasisi hizi kutoachwa kama yatima wakati zina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii masuala mbalimbali ya athari na faida za kutunza na kuhifadhi mzaingira,” alisisitiza Mfugale.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na tatizo la ongezeko la joto kutokana na shughuli za kibinadamu na kusababisha taifa kukabiliwa na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi na kuathiri shughuli nyingine za maendeleo kama kilimo.
Katika hatua nyingine, Mfugale alisema Tanzania haijaweza kunufaika ipasavyo na fedha za mazingira kutoka mfuko wa dunia wa kupambana na mabadiliko ya tabia nchi (UNFCCC) ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Kwa mfano Kenya, alisema hadi sasa ina zaidi ya miradi 19 baada ya kuwezeshwa fedha kutoka mfuko huo kupitia programu ya uhifadhi wa mazingira kukabiliana na tabianchi (CDM) ya mfuko huo.
Bila kutaja sababu ya udhaifu huo, aliishauri serikali kupitisha fedha za mazingira moja kwa moja kwenye asasi za mazingira badala ya mfumo wa sasa wa fedha hizo kutolewa kwa mlolongo mrefu.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: