Wapiganaji wa peshmerga baada ya ushindi kwenye mji wa Zumar dhidi ya Dola la Kiislamu.
Operesheni ya siku mbili ya kijeshi ya wapiganaji wa Peshmerga katika
jimbo la Kurdistan imefanikiwa kufungua njia kuelekea Mlima Sinjar,
uliokuwa umezingirwa na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu.
Mafanikio haya ni muhimu sana katika mapambano ya kuuchukuwa mji wa
Sinjar, ulio chini ya mlima wenye jina hilo hilo, ambao ulichukuliwa na
IS tangu mwanzoni mwa mwezi Agosti mwaka huu. Mkuu wa Baraza la Usalama
la Mkoa wa Kurdistan, Masrur Barzani, amesema vikosi vya Kikurdi
vilisonga mbele jioni ya jana kuelekea kwenye mlima huo.
"Leo tumekamilisha operesheni ambayo tuliianza jana, na ambayo
inasimamiwa na mwenyewe Rais Masoud Barzani, ikihusisha eneo zima kutoka
Zumar hadi Mlima Sinjar, kulikomboa eneo kubwa la Kurdistan, na pia
kuwaokoa watu wa jamii ya Yazidi waliokwama mlimani. Ilikuwa operesheni
kubwa na tunashukuru imefanikiwa," amesema kiongozi huyo.
Maelfu ya Wayazidi walikuwa wamekwama kwenye mlima huo mwanzoni mwa
mwezi Agosti, wakati wapiganaji wa IS walipoichukua miji hiyo ya Sinjar
na Zumar, na hivyo kuchochea wimbi kubwa la uhamaji.
Licha ya kwamba wengi wao waliondoshwa kwa njia ya anga au
kusindikizwa na vikosi vya usalama kupitia Syria na kisha kurudi Iraq
kujihifadhi kwenye jimbo la Kurdistan, lenye mamlaka yake ya ndani,
lakini wengine wengi walikuja baadaye na kubakia wamekwama mlimani.
Marekani yauwa viongozi wa IS
Vijiji ambavyo vimechukuliwa hivi karibuni na vikosi vya
Peshmerga vinaonesha ishara za mapigano makubwa, huku majengo mengi
yakiwa yameharibiwa vibaya kwa mashambulizi ya anga ya Marekani. Mkuu wa
operesheni ya Marekani, Luteni Jenerali James Terry, amesema eneo
lililochukuliwa na peshmerga lina ukubwa wa kilomita za mraba 100.
Katika hatua nyengine, Marekani inasema operesheni yake ya kijeshi
nchini Iraq na Syria imewauwa viongozi kadhaa wa IS, katika siku za hivi
karibuni. Msemaji wa jeshi, Admirali John Kirby, amesema wanaamini kuwa
IS imepoteza viongozi wake muhimu wa ngazi za juu na kati, miongoni
mwao ni Haji Mutazz, naibu wa kiongozi mkuu wa IS, Abu Bakr al-Baghdadi.
Wengine ni Abdulbasit, ambaye alikuwa akishughulikia wapiganaji wa
kigeni, na Radhwin Talib, ambaye alikuwa msimamizi wa IS kwenye mji wa
Mosul. Jarida la Wall Street liliripoti hapo awali kwamba vikosi vya
Marekani vilikuwa vimewalenga viongozi kadhaa muhimu wa IS, likimnukuu
Mkuu wa Majeshi, Jenerali Martin Dempsey. Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya IS mwezi Agosti
mwaka huu, ambayo sasa yanazijumuisha nchi kadhaa washirika, ndani na
nje ya Ghuba na Mashariki ya Kati.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment