Katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu ongezeko la joto duniani
unaofanyika Lima, Peru, upo mvutano kati ya nchi tajiri na maskini
kuhusu hatua za kuchukua ili kuzuia mabadiliko ya tabia ya nchi.
Ni nani anayepaswa kubeba jukumu la kulinda mazingira na kupunguza
utoaji wa gesi ya kaboni katika anga? Hilo ndilo swali wanalojadili
wajumbe kutoka nchi 195 katika mkutano wa Umoja wa Mataifa unaondelea
mjini Lima. Mataifa yanayoendelea yanazinyooshea kidole nchi tajiri na
kusema kwamba zinatakiwa kuwajibika zaidi kwani ndizo zinazochafua
mazingira kwa kiasi kikubwa. Lakini nchi tajiri zinakataa na kutaka
mataifa yanayoinukia kama vile China na India yadhibiti utoaji wa gesi
chafu ya carbon dioxide kutoka kwenye viwanda na magari kwa mfano.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, aliuhudhuria
mkutano wa Lima kwa kifupi na kuzihimiza nchi zote kuchukua hatua. Kerry
pia alisifu makubaliano ambayo yameweza kufikiwa hadi sasa. "Marekani
na China ni nchi mbili ambazo kwa muda mwingi zilionekana kuwa viongozi
wa pande mbili zinazopingana katika mjadala huu," alisema Kerry. "Lakini
sasa nchi hizo zimekubaliana kwenye masuala kadhaa. Hii ni hatua ya
kihistoria na inapaswa kutufundisha kwamba vizuizi tulivyokutana navyo
katika miaka iliyopita vinaweza kuondolewa."
Mkataba kamili kusainiwa Paris 2015
Kerry amezitaka nchi zinazoendelea pia kukubali kufanya na mabadiliko
ya sera na kulivalia njuga suala la ulinzi wa mazingira. Alikumbusha
kuwa hivi sasa asilimia 50 ya gesi ya kaboni inatoka katika nchi
zinazoendelea.
Mpaka sasa mkutano wa Lima haujawa na mafanikio makubwa lakini waziri
wa mazingira wa Peru Manuel Pulgar-Vidal ameahidi kwamba mkutano
hautomalizika bila wajumbe kuweka misingi ya ahadi watakazotoa katika
mkutano wa mazingira utakaofanyika jijini Paris mwakani. Hadi hapo kila
nchi inapaswa kuweka bayana utayarifu wake wa kupunguza utoaji wa hewa
chafu ya kaboni. Lengo la mkutano wa Paris ni kuwa na mkataba
utakaodhibiti uchafuzi wa mazingira na hivyo kufanya kiwango cha joto
duniani kisiongezeke kwa zaidi ya nyuzi joto 2 za celcius ifikapo mwaka
2100.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment