Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), John Brennan,
amelitetea shirika lake dhidi ya tuhuma za Baraza la Seneti kwamba
wamekuwa wakitumia mateso ya kikatili kuwahoji watuhumiwa wa ugaidi.
Katika hali isiyo ya kawaida, jioni ya jana CIA iliamua kuvunja
ukimya juu ya ripoti ya Baraza la Seneti iliyoonesha kuwa maafisa wa
shirika hilo la kijasusi wamekuwa wakitumia mbinu zilizopigwa marufuku
kisheria na pia kulidanganya bunge na taifa kuhusiana na operesheni zake
za kusaka taarifa dhidi ya ugaidi.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari kwenye makao makuu ya CIA,
mjini Virginia, Brennan alisema programu ya shirika hilo kuwahoji
washukiwa iliisaidia sana Marekani kama baadhi ya maafisa wake walitumia
njia alizoziita "za kuchukiza sana" ambazo "haifahamiki" ikiwa
ziliwezesha kupatikana taarifa za maana.
"Tayari nimeshaeleza kwamba uhakiki wetu unaonesha kwamba programu ya
kuwaweka kizuizini na kuwahoji washukiwa ilitoa taarifa zenye maana
sana ambazo ziliisaidia Marekani kupangua mipango ya mashambulizi,
kuwanasa magaidi na kuokoa maisha. Lakini nifahamike wazi, hatujasema
kwamba ni matumizi ya mbinu hizo kali za kuhoji ndani ya programu hiyo
ndizo zilizotuwezesha kupata taarifa hizo kutoka kwa mahabusu," alisema
Brennan.
Washirika wa Marekani wangiwa na wasiwasi
Juzi, Baraza la Seneti lilitoa ripoti yake inayoonesha kwamba
CIA iliipotosha Ikulu na umma wa Marekani kuhusu ilivyowatesa mahabusu
baada ya mashambulizi ya tarehe 11 Septemba 2001, na ilitumia mbinu za
kikatili na kinyama zaidi kuliko ilivyosema. Brennan amekiri baadhi ya
maafisa wake walichupa mipaka katika mbinu zao za kuwahoji mahabusu.
Washirikia wengi wa Marekani ambao walichangiana taarifa na CIA, sasa
wameonesha wasiwasi, baada ya kuchapishwa kwa ripoti hiyo. Poland,
Afghanistan, Uingereza na Saudi Arabia, ni miongoni mwa mataifa
yanayoshirikiana na Marekani katika kile kinachoitwa "vita dhidi ya
ugaidi" na ambayo viongozi wake wamejitokeza kuilaumu CIA baada ya
ripoti hiyo.
"Bush alidanganya kuhusu Iraq"
Wakati hayo yakiendelea, CIA imechapisha barua inayoonesha kwamba
walikuwa na mashaka na hoja ya rais wa zamani, George Bush, kuhalalisha
vita vyake nchini Iraq.
Kuelekea uvamizi wa Machi 2003, makamu wa rais wa wakati huo, Dick
Cheney, na wenziwe serikalini walisema mmoja wa watekaji nyara wa ndege
zilizotumika kwenye mashambulizi ya Septemba 11, Mohammed Atta, alikuwa
amekutana na jasusi wa Iraq, Ahmad al-Ani, mjini Prague, lakini barua
hiyo iliyopelekwa kwa Seneta Carl Levin mwezi Machi mwaka huu, inaonesha
kwamba hilo halikuwa kweli.
Levin anasema ameiruhusu CIA kuichapisha barua hiyo ili kuonesha namna Bush alivyoidanganya Marekani kabla ya uvamizi wa Iraq.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment