Hayo yalisemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kama African Barrick Gold (ABG), Brad Gordon wakati akitambulisha jina hilo jipya la Acacia kwa viongozi wa wilaya na vijiji vilivyopo Kahama na Nyang’whale mkoani Shinyanga katika mkutano uliofanyika kwenye mgodi wa Bulyanhulu wilayani Kahama.
“Juzi usiku (Jumatatu), tumezindua jina jipya la Acacia kwenye jengo litakalokuwa makao makuu ya kampuni yetu kwa bara la Afrika, pale barabara ya Bagamoyo jijini Dar es Salaaam,” alisema Gordon.
Alisema Acacia imekuja na mtazamo mpya ambao umejikita kukuza biashara, kuweka mazingira bora kwa wafanyakazi wake , kuendeleza na kujenga mahusiano mema na jamii inayotuzunguka migodi yake.
Alisema kampuni hiyo ambao iko nchini kwa takriban miaka 15, imedhamiria kuweka mazingira bora kwa wafanyakazi wake na kwamba imeanzisha mkakati wa kuwazawadia wafanyakazi wanaofanya vizuri na siyo kutoa adhabu tu kwa anayekosea.
Alitaja zawadi hizo kuwa ni kupewa kadi itakayomwezesha mfanyakazi kupata zawadi mwisho wa mwaka.
Gordon alizitaja baadhi ya zawadi hizo kuwa ni gari, tiketi ya ndege kwa watu wawili kwenda nchini Uingereza , kupata udhamini wa elimu na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, alisema kuwa kubadilishwa kwa jina la kampuni hiyo hakuna mahusiano yoyote ya kuuzwa au kuuza wafanyakazi wake.
"Tumepewa heshima na nguvu kwa kampuni hii kuhamisha makao yake makuu na sehemu kubwa ya wafanyakazi wake wameletwa nchini kutoka Afrika Kusini, hii inafaida kubwa kwa Watanzania," alisema Mpesya na kuongeza kuwa:
“Ninawaomba viongozi, mkawaeleze vizuri wananchi kwa nini kampuni hii imebadilisha jina ili kuondoa uvumi usiokuwa na maana.”
Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bugarama, James Mhagwa, alitaka kujua kama mabadiliko hayo ya jina hayataathiri mipango ya nyuma ya maendeleo baina ya wanajamii na ABG.
“Kama wenzangu walivyosema awali jina hili jipya ni kuongeza ufanisi, na DC amefafanua, sisi tunachokifanya sasa siyo kuyaacha yale tuliyoanza nayo, bali ni kuongeza ufanisi zaidi, ” alisema mkuu wa kitengo cha mahusiano ya jamii wa Acacia, Steven Kisyake.
Kisyake alisema ahadi zote zilizotolewa na ABG ambayo sasa ni Acacia, itaendelea nazo kutokana na mazungumzo yaliyokwisha kufanyika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Ibrahim Marwa, aliitaka kampuni hiyo kuwashirikisha wananchi kutatua kero zao na kuandaa mapendekezo kwa kuwatumia wataalamu.
CHANZO:
NIPASHE


No comments:
Post a Comment