Social Icons

Pages

Thursday, December 04, 2014

KAFULILA: NITFUATILIA MAAZIMIO YA BUNGE YA KUWANG'OA VIGOGO

Sakata la wizi wa Sh. bilioni 306, uliyofanywa kwenye akaunti yaTegeta-Escrow, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), limeingia katika sura mpya baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha maazimio dhidi yake.
“Kilichobaki ni kuendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya tuliyofikia sasa, ili hiki ambacho tumekiazimia leo, kiweze kutekelezwa kama mbunge mwenye maslahi nayo, nitaendelea kufuatilia kwa karibu sana.”
Hiyo ni kauli yake, David Zacharia Kafulila, Mbunge wa Kusini (NCCR-Mageuzi), ambaye aliibua madai ya kuwapo wizi huo, kupitia mkutano wa 15 wa Bunge Mei, mwaka huu.
Kafulila anasema  maazimio hayo ya Bunge hayatarajiwi kubaki kwenye makaratasi badala yake atayafuatilia huko huko yakipelekwa Ikulu.
“Hata katika mikutano ya Bunge ijayo, nitaendelea kufuatilia ili maazimio haya yasibaki kwenye makaratasi kama ambavyo tumekuwa tukishuudia kwa baadhi ya maazimio yanayofikiwa,” anaeleza Kafulila.
Kafulila anabainisha kuwa anajisikia fahari kutokana na alichosema, awali kikadaiwa na baadhi ya watuhumiwa kuwa ni uzushi, ufitini na uongo, kimedhihirika kuwa kweli.
Anashukuru wabunge wenzake walioshikamana katika kuishauri serikali, ambayo kwa kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ikaagiza mamlaka zake kufanya uchunguzi na hatimaye ukweli kubainika.

Kuitwa Tumbiri
Anasema miongoni mwa mambo yaliyowahi kumhuzunisha katika kutumikia jamii ya Watanzania, ni siku ambayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alimuita  Tumbiri.
Hilo lilitokea kwenye mkutano wa 15 wa Bunge, wakati Kafulila akijenga hoja kwa lengo la kuelewesha wabunge, waelewe madai yake kwamba kulikuwa na wizi wa kiasi kikubwa cha fedha, uliofanyika ndani ya akaunti ya Escrow ya  BoT.
“Hata hivyo kwa sasa nalichukulia jambo hilo kuwa ni moja ya changamoto, ambazo kila mtu anayeamua kufuatilia jambo hususani lenye maslahi kwa umma, lakini pia linalogusa maslahi ya wachache hasa wenye nguvu kimadaraka, anakabiliana nazo ama hadharani au kwa siri,” anaeleza Kafulila.

Wabunge waelewa madai yake
Hali ya hewa katika mkutano huo, nusura ichafuke kufuatia wabunge hususan wa kambi ya upinzani, akiwamo John Mnyika (Ubungo),Tundu Lissu (Singida Mashariki), Halima Mdee (Kawe), Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) kuwa na msimamo wa kutaka iundwe kamati maalumu ya Bunge, kuchunguza madai hayo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliomba Bunge liridhie kutoundwa kamati ya Bunge, badala yake vyombo vya serikali vishughulikie uchunguzi huo, jambo ambalo hatimaye liliridhiwa na kuachwa mikononi mwa CAG akishirikiana na Takukuru.
Licha ya kupitia vielelezo mbalimbali, vyombo hivyo vilifanya mahojiano na wale wote waliotuhumiwa kuhusika kwa namna tofauti katika kuchukua fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Escrow, baadaye ripoti ya uchunguzi huo ikatolewa na kuwasilishwa kwa uongozi wa Bunge.
Novemba 19 mwaka huu, Naibu Spika wa Bunge alimkabidhi Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe na Makamu wake, Deo Filikunjombe, ripoti ya CAG kwa ajili ya kuipitia na kuandaa ripoti yake ambayo iliwasilishwa bungeni Novemba 26, mwaka huu.
Kazi ya kujadili ripoti hiyo ambayo ilitarajiwa kufanyiwa kazi kwa siku mbili; 27 na 28 Novemba mwaka huu haikuwa rahisi.
Maswali, wasiwasi na hofu vilitawala miongoni mwa wabunge, katika kipindi chote cha kusubiriwa ripoti hiyo kutawaliwa na fununu, zilizotaja majina yao zikiyahusisha na wizi huo.
Hata hivyo, taarifa hiyo ikabainisha majina ya viongozi ambao wanahusishwa na wizi huo, kwa namna tofauti tofauti.
Wanaohusika kwa mujibu wa ripoti ya PAC, ni waliobainishwa na uchunguzi uliofanywa na CAG, Takukuru na hao ndiyo ambao Bunge limefikia azimio la kuwapeleka kwa mamlaka iliyowateua ili uteuzi wao utenguliwe.

Waliopelekwa kwa mamlaka ya uteuzi
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,Joachim Maswi na Wajumbe wote wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) ndiyo ambao Bunge limeazimia Rais awawajibishe.
Azimio hilo ambalo ni la pili, linasema viongozi hao wamehusishwa na vitendo vya kijinai ambavyo pia vinakiuka maadili ya viongozi wa umma na hivyo kukosa uhalali wa  kuwa viongozi wa umma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: