Social Icons

Pages

Wednesday, December 31, 2014

HIVI KERO ZA MVUA ZITAISHA LINI DAR?

Ni janga kwa sababu watu waishio mabondeni hupoteza maisha, hupoteza makazi, hupoteza mali na hupoteza biashara zao, ingawa huwachukua muda mfupi kurejea kwenye makazi hayo mara tu mvua zinapoisha.

Kwa kawaida mvua ni neema kutokana na faida nyingi inazoleta kwa jamii, hasa kwa nchi maskini kama Tanzania ambazo hutegemea sana kilimo ambacho hakijaendelezwa sana kiasi cha kuwa cha kisasa kwa sehemu kubwa ya nchi.
Kwa maana hiyo, mvua ni baraka kwa kuwa ndio tegemeo kubwa la mafanikio katika kilimo endapo wananchi wanaelekezwa vyema kuhusu matumizi mazuri ya vipindi vya mvua. Faida nyingine ni kama maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ingawa bado wananchi hawajaeleweshwa wala kupewa stadi za kutosha za uvunaji maji.
Pia, kwa Jiji la Dar es salaam, ni sawa kabisa wanaposema “watu wa Dar es Salaam wanaogopa mvua kuliko magari” kwa kuwa mvua ni janga, hata iwe ya saa chache kama ilivyokuwa Jumatatu.
Ni janga kwa sababu watu waishio mabondeni hupoteza maisha, hupoteza makazi, hupoteza mali na hupoteza biashara zao, ingawa huwachukua muda mfupi kurejea kwenye makazi hayo mara tu mvua zinapoisha.
Ni janga kwa sababu mvua zinaponyesha barabara nyingi hazipitiki na hivyo kusababisha foleni kubwa kwenye barabara zinazopitika kwa sababu magari yote hukwepa barabara mbovu na kutumia chache nzuri.
Lakini ni janga kubwa kwa sababu miundombinu ya majitaka, si tu ni mibovu, bali pia hailingani na mabadiliko makubwa ambayo jiji limepitia katika miaka michache ya hivi karibuni; kushamiri kwa majengo mengi katikati ya mji na majengo ambayo yanazuia mikondo ya maji kuelekea baharini isifanye kazi vizuri.
Hili ni tatizo ambalo linaonekana kuwa la kawaida sasa na si ajabu viongozi wetu wanaposikia mvua kubwa imenyesha, hufahamu kuwa baadhi ya maeneo yamefurika maji kwa sababu, kwanza, njia ambayo zingetumiwa na maji hayo kuelekea baharini zimebanwa kutokana na ujenzi holela na pili, miundombini ya majitaka inazidiwa na wingi wa maji yanayoongezewa na mvua.
Kwa hiyo, ni jambo ambalo linaonekana la kawaida kuona vinyesi vikisambaa kwenye mitaa ya katikati ya jiji baada ya mvua kidogo kunyesha, picha za magari yaliyokwama kwenye maji katikati ya mji na picha za nyumba zinazoonekana paa tu mita chache kutoka katikati ya jiji.
Haya huanikwa kila wakati mvua zinaponyesha na hatujui wala hatuoni mkakati wowote mkubwa ukichukuliwa kuhakikisha miundombinu ya majitaka inapanuliwa ili istahimili ongezeko la majengo katikati ya jiji. Haiboreshwi kuhakikisha inadhibiti uwingi wa maji yanayosababishwa na mvua zinazoweza kuwa kubwa kama ilivyokuwa juzi.
Hatujui kama viongozi wetu wanaguswa na matatizo haya, ambayo ni kero kubwa hasa kwa wananchi wa kawaida au wameshayazoea kwa kuwa hutokea kila mwaka na baada ya mvua kuisha husahauliwa?
Hivi hadi lini viongozi wetu wataendelea kuona tatizo hili la mvua linahitaji mkakati mkubwa wa kukabiliana nalo? Hivi ni lini viongozi wetu wataona kuwa miundombinu ya majitaka haistahimili ongezeko la majengo linalosababisha ongezeko la majitaka? Hivi ni lini wataona kuwa miundombinu ya majitaka haistahimili ongezeko la maji yanayoletwa na mvua?
Hivi itakuwa ni nchi gani ambayo wananchi wake wanaandaliwa kuzoea matatizo badala ya viongozi kushughulika kuwatatulia kama wanavyoahidi wakati wakitoa jasho kuomba madaraka?
Sisi tunadhani kuwa wakati huu tunajiandaa kuingia mwaka mpya, viongozi wetu waanze kuyachukia matatizo na kufikiria njia za kuwapunguzia wananchi wao kero za kila mwaka ili waanze kuishi kwa matumaini.

CHANZO: MWANANCHI

No comments: