Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya EU, yanaonekana kuanza kuchoshwa na
vitisho vya Uingereza kujitoa katika umoja huo, kutokana na madai ya
waziri mkuu David Cameron kutaka kubadilisha kanuni za msingi wa umoja
huo.
Wakati king'ora cha kuashiria moto kilivyokatiza hotuba kubwa ya waziri
mkuu David Cameron kuhusu Ulaya katika kiwanda kikubwa cha kutengeneza
mitambo mwezi Novemba 2014, alitania kuwa hadhira yake ilikuwa ikisikia
kengele zikilia mjini Brussels kuhusiana na uwezekano wa Uingereza
kuondoka katika Umoja wa Ulaya.
Ukosoaji wa Umoja wa Ulaya ni jambo linalopokelewa vyema nchini
Uingereza, ambako chama kinachoupinga umoja huo cha UK Independent UKIP,
kilijizolea ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge la Ulaya mapema
mwaka 2014.
Shinikizo la kisiasa
Akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa wapinzani wa Umoja wa Ulaya ndani na
nje ya chama chake, waziri mkuu Cameron ameahidi kura ya maoni kuamua
ama kubakia au kutoka ndani ya umoja huo mwaka 2017, ikiwa atachaguliwa
tena kuliongoza taifa hilo mwezi Mei mwaka 2015. Wakati akisema
angependa kuona Uingereza ikibakia katika umoja wa Ulaya, Cameron
amedokeza pia kwamba anaweza kubadilisha msimamo wake ikiwa matakwa
muhimu hayatatekelezwa.
Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Waingereza hawana ari ya kuwa katika
Umoja wa Ulaya, licha ya nchi hiyo kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya
kisiasa na kiuchumi kwa miaka 40. Hata uongozi wa chama cha upinzani cha
Labour, ambacho hakiahidi kura ya maoni, kinapambana kutoonyesha hisia
kali kuhusu umoja huo wenye wanachama 28.
Suala moja muhimu na linalozua tafrani ni kuhusu uhamiaji, na hasa
kushindwa kwa Uingereza kuwazuwia wahamiaji wa EU kuingia nchini humo
kutokana na kanuni ya umoja huo inayowapa raia wake uhuru wa kutoka
sehemu moja kwenda nyingine bila kuwekewa vikwazo.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa raia 228,000 wa Umoja wa Ulaya
wamewasili nchini Uingereza kufikia Julai mwaka huu -- hii ikiwa ni
zaidi ya mara mbili ya shabaha ya wahamiaji 100,000 aliyoiahidi Cameron
kufikia Mei 2015.
Msimamo usiyoeleweka
Lakini Cameron anatuma ujumbe mchanganyiko kuhusu uanachama wa Umoja wa
Ulaya. Wakati chama chake cha Wahafidhina kikipoteza umaarufu kwa chama
cha UKIP, wafanyabiashara wengi wanasisitiza umuhimu wa kubaki katika
Umoja wa Ulaya, ambao unatoa fursa makhsusi za kuwafikia walaji wake
milioni 500.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anataka UK ibakie katika EU lakini
hakubaliani na madai ya Cameron kubadilisha kanuni za msingi za umoja
huo.
Michael Rake, kiongozi wa shirikisho la viwanda la Uingereza, alionya
kuwa kuondoka katika Umoja wa Ulaya kutaifanya Uingereza kujifungia nje
ya ulimwengu katika wakati ambapo dunia inapitia mabadiliko
yasiyozuwilika.
Jambo la muhimu ni kwamba Cameron aliamua kutoa hotuba yake kuhusu Ulaya
katika kiwanda cha mitambo mikubwa cha JBC, ambacho pengine
hakingekuwepo bila faida za soko la pamoja linalotokana na uanachama wa
Umoja wa Ulaya.
Na licha ya kupendekeza kupunguzwa kwa mafao ya kijamii kwa wahamiaji wa
EU, Cameron anasisitiza kuwa hataki kuharibu kanuni ya uhuru ya kutoka
sehemu moja kwenda nyingine, ambayo Waingereza zaidi ya milioni 1.3
wamenufaika nayo.
Badala yake, mkwara wa Cameron unalenga kuilainisha Brussels kwa
kutishia kuiondoa Uingereza katika EU ikiwa hakutakuwa na makubaliano
kuhusu masuala muhimu kama vile uhamiaji. Lakini Umoja wa Ulaya
umesisitiza msimamo wa kupinga jitihada zozote za kubadili kanuni yake
hiyo ya uasisi kuhusu uhuru wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Chini ya uongozi wa Cameron, Uingereza imejikuta ikizidi kukwaruzana na
wanachama wengine, kuhusiana na masuala kuanzia uteuzi wa rais wa
Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claud Juncker, na kura ya turufu ya
Uingereza mwaka 2011 kupinga hatua zilizonuwiwa kushughulikia mgogoro wa
kiuchumi wa umoja huo. Lakini tabia hii inaonekana kuwachosha wanachama
wengine.
'Cameron anachezea moto'
Mwezi Oktoba, aliyekuwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose
Manuel Barroso alionya kuwa Cameron anachezea moto kwa kuchochea hisia
za chuki dhidi ya Umoja wa Ulaya, akisema katika mahojiano na
televisheni ya France 24 kuwa "huwezi kuikosoa EU kuanzia Jumatatu hadi
Jumamosi, na kuwaomba watu kuipigia kura EU siku ya Jumapili.
Mrithi wake Jean-Claud Juncker, ameahidi kufanya kazi kuibakiza
Uingereza katika Umoja wa Ulaya, lakini mataifa mengi hayako tayari
kubadili mikataba ya EU kwa lengo la kubadili sheria za msingi za
uanachama, yakihofia kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo
mengine yasiyotarajiwa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliripotiwa
kukosa uvumilivu pale Cameron alipozungumzia kuanzisha ukomo wa
wahamiaji - hatua ambayo aliamua kutoichukuwa wakati akibainisha mipango
yake ya kupunguza uhamiaji.
Wengine wanaona katika mtazamo wa Uingereza, ukaida wa kudumu wa
kuachana na historia yake ya zamani, ilipokuwa taifa lenye nguvu kubwa
duniani, lenye mahusiano maalumu na Marekani, na pia njozi ya ufahari wa
utamaduni wake ulioanzishwa karibu miaka 2000 iliyopita, na ambao sasa
unatishiwa na wale wanaowachukulia kuwa ni washenzi wanaomiminika nchini
mwao.
CHANZO: DW KISWAHILI

No comments:
Post a Comment