Kamati ya uongozi wa shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA
inakabiliwa na mgogoro mpya kufuatia kujiuzulu kwa Michael Garcia,
akipinga kuchakachuliwa kwa ripoti yake ya rushwa katika zabuni za kobe
la Dunia.
Uamuzi wa ghafla wa Garcia kujiuzulu siku ya Jumatano huenda ukazidisha
shinikizo ndani ya kamati ya uongozi ya rais wa FIFA Sepp Blatter
kuchapisha ripoti ya wakili huyo Mmarakeni yenye kurasa 430,
inayotathmini kura zilizozipatia ushindi wa kuandaa kombe la dunia, nchi
za Urusi kwa mwaka 2018 na Qatar mwaka 2022.
Akiwa ameshtushwa na kujiuzulu kwa Garcia, Blatter aliliambia shirika la
habari la Associated Press kuwa jambo hilo moja ya mada za mkutano wa
siku mbili wa bodi ya uongozi wa FIFA, uliyofanyika Alhamisi na Ijuma.
Wajumbe 27 wa Bodi hiyo wamegawanyika juu ya ama kutangaza sehemu au
ripoti kamili ya Garcia, jambo lililosababisha watatu kati yao
kushtakiwa kwa mienendo inayokiuka maadili.
Uozo ndani ya FIFA
Sifa ya FIFA ilipata pigo jingine baada ya Garcia kusema kuwa hakuna
kamati huru ya uongozi, mchunguzi, au kamati ya upatanishi inayoweza
kubadilisha utamaduni wa shirikisho hilo. Blatter alieleza kushangazwa
na uamuzi huo wa Garcia, lakini alisema kazi ya kamati ya maadili
itaendelea na kuwa sehemu muhimu ya mkutano huo wa bodi ya uongozi.
Mchunguzi huyo Garcia alijiuzulu siku moja baada ya FIFA kutupilia mbali
rufaa yake dhidi ya mukhtasari wa uchunguzi wake uliyotangazwa na
shirikisho hilo, kuhusu utoaji wa zabuni za maandalizi ya kombe la dunia
mwaka 2018 na 2022.
Katika taarifa, Garcia alisema kulikuwa na ombwe la uongozi katika FIFA,
na kwamba alikuwa amepoteza imani na Hans-Joachim Eckert, mwenyekiti wa
chemba ya maamuzi ya idara ya maadili, na kwamba jukumu lake katika
mchakato huo lilikuwa limefika mwisho.
Urusi, Qatar zasafishwa na FIFA
Urusi ilishinda zabuni ya kuandaa mashindano ya kombe la dunia mwaka
2018, huku Qatar ikishinda uwenyeji wa mashindano ya mwaka 2022. Lakini
kufuatia madai ya rushwa, Garcia alipewa jukumu la kuchunguza na
kuripoti juu ya mchakato wa maombi ya zabuni hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Garcia aliyoitoa siku ya Jumatano, ripoti yake
ilibaini masuala mazito na mapana kuhusiana na mchakato wa maombi.
Lakini mukhtasari wa Eckert wa ripoti hiyo uliyochapishwa mwezi Novemba,
ulizisafisha Urusi na Qatar kutokana na makosa yoyote.
Garcia aliukatia rufaa mara moja mukhtasari uliyotolewa na Eckert,
akisema ripoti yake imewasilishwa isivyo. Lakini rufaa yake ilielezwa
kama isiyokubalika na FIFA, kwa hoja kwamba mukhtasari huo uliyotangazwa
hauhusishi maamuzi, na kwa hivyo hauna nguvu ya kisheria na wala
hauwezi kukatiwa rufaa.
Mapambano yanaendelea
Mtendaji kutoka Ujerumani Theo Zwanziger anapanga jaribio lingine
kuichapisha kikamilifu ripoti ya Garcia, na pia kwenye ajenda ya mkutano
wa Marrakeshi kunajadiliwa sheria za kazi nchini Qatar.
"Fifa katika zahma," liliandika gazeti la Uingereza la The Guardian
katika toleo lake la jana Alhamisi, huku Sueddeutsche Zeitung la
Ujerumani likiitaja hatua ya Garcia kuwa kilele cha muda cha malumbano
yaliokuwa yanatokota kwa muda mrefu."
Rais wa shirikisho la mpira wa miguu barani Ulaya UEFA Michel Platini,
ambaye anamtaka Blatter aachie ngazi kama mkuu wa FIFA mwakani, aliitaja
hatua ya kujiuzulu kwa Garcia kama upungufu mpya. Afisa mtendaji wa
zamani wa FIFA Jerome Champagne, ambaye anapanga kupambana na Blatter
katika kinyanganyiro cha urais wa shirikisho hilo aliitaja kama hatua ya
kurudi nyuma.
CHANZO: DW KISWAHILI
No comments:
Post a Comment