Social Icons

Pages

Wednesday, November 19, 2014

USHIRIKI WA WEREMA, MASWI IPTL HUU HAPA

Joto la uchunguzi wa hamisho la zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za umeme baina ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likizidi kupanda, taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha kuwa kazi itakuwa nzito kwa wakuu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Nishati na Madini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Taarifa zinadai kuwa wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ikiwa imejichimbia Dodoma kuchambua ripoti ya uchunguzi ya Mkaguzi na Madhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuna ushahidi unaoonyesha jinsi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, walivyohusika kumuamuru Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Beno Ndulu, aidhinishe uchotaji wa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwenda IPTL.
Akaunti hiyo ilikuwa imefunguliwa BoT ili kuhifadhi fedha zilizokuwa zinabishaniwa kati ya Tanesco na IPTL.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Jaji Werema anadaiwa kuandika barua Oktoba 2, mwaka 2013 yenye Kumbukumbu Namba AGCC/E.80/6/65 kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha (Hazina), Dk. Servacius Likwelile, akitaka fedha hizo zitolewe haraka.
Walioiona barua hiyo wanasema kuwa Jaji Werema aliinakili barua hiyo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.
Katika barua hiyo Jaji Werema amenukuliwa akibariki kuchotwa kwa fedha hizo kwa msingi wa maamuzi yaliyotolewa na Mahakama Kuu chini ya Jaji John Utamwa.
“Maamuzi yoyote ya kuidhinisha kuchotwa kwa fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow yanalindwa na maamuzi ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Utamwa,” kilisema chanzo chetu kikinukuu barua ya Werema.
“Mahakama Kuu imetupa wito wa msaada,” amenukuliwa Jaji Werema huku akisisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kutumia fursa adimu iliyopatikana kujitoa kwenye madai yasiyofaa katika mgogoro wa fedha hizo.
Katika barua hiyo, Jaji Werema amenukuliwa akifafanua kwamba, ameisoma ripoti na kuwa suala ambalo lilioonekana kuishughulisha timu iliyohusika, ni uwekezaji wa fedha za Escrow.
Chanzo chetu kinasema kuwa Jaji Werema alisisitiza kuwa Akaunti ya Escrow ilikuwa ni zao la makubaliano juu ya akaunti ya Tegeta Escrow yaliyofanyika Julai 5, 2006, huku akiirejea kuwa BoT kama wakala wa Escrow, aliruhusiwa kuziwekeza fedha hizo kwenye “uwekezaji ulioruhusiwa” kama inavyoelekezwa kwenye Kifungu cha 3.4 na 7.2 (c) cha makubaliano hayo.
Mpashaji wa NIPASHE alisema kuwa Jaji Werema katika barua yake alisema, njia sahihi na ya busara ni kwa wakala wa Escrow kuijulisha IPTL kuhusiana na uwapo wa “uwekezaji ulioruhusiwa” na lini utaiva.
Chanzo chetu kinasema kuwa Jaji Werema alikwenda mbali na kusisitiza kuwa hakuna pingamizi lolote kuhusu IPTL kupewa fedha hizo kwa sababu tayari kulikuwa na hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji Utamwa.
“Kwa hiyo kwa uthabiti wa maoni yangu, ninasema, suala pekee lenye mashiko hapa ni lile linalohusiana na zile fedha za “uwekezaji uliokubalika”,  chanzo chetu kilikariri msimamo wa Jaji Werema kuhusu fedha hizo ambazo sasa zimekuwa ni gumzo hasa baada ya walionufaika nazo kudaiwa kuzigawa kama njugu.
Mpashaji wetu alisema kuwa kwa kuhimiza umuhimu wa kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo, Jaji Werema anadaiwa kusema kuwa “serikali isije ikaonekana inashindwa kufanya maamuzi ya kutekeleza hukumu iliyoamriwa na mahakama.”
Anadaiwa kusema kuwa uamuzi wa mahakama unalinda maslahi mapana ya umma dhidi ya malalamiko yasiyoisha juu ya fedha za akaunti ya Escrow.
Jaji Werema anadaiwa kuweka msisitizao katika barua yake akisema kuwa maamuzi yoyote ya kuidhinisha kuchotwa kwa fedha kutoka kwenye akaunti ya Escrow yanalindwa na maamuzi ya Mahakama Kuu chini ya Jaji Utamwa.
“Kwa hiyo hakuna kizuizi au pingamizi la kushughulika na akaunti hiyo kuanzia sasa,” chanzo chetu kilinukuu barua ya Jaji Werema.
Jaji Werema ananukuliwa akisema, kwa mujibu wa maoni yake, wakala wa Escrow (yaani BoT), anapaswa kuifahamisha IPTL juu ya uwapo wa uwekezaji ulioruhusiwa na pale ambapo fedha zitawekezwa, na sheria na masharti ya uwekezaji huo.
Anadaiwa kusema kuwa ni maoni yake vile vile kwa wakala wa Escrow na serikali wazungumze na kukubaliana na IPTL juu ya nani anahusika na kukumbushia fedha hizo kabla hazijaiva kwa maslahi ya kampuni ili iendelee kufanya kazi.
Jaji Werema ananukuliwa akisema kuwa, udhamini wa serikali chini ya PPA ulikuwa umepitwa na wakati, na kuonya kuwa serikali haiwezi kuwekwa kwenye hatari isiyotarajiwa kwa kuendelea kuhusika na fedha hizo.
Jaji Werema ananukuliwa akipuuzia juu ya athari zinazoweza kutokea kutokana na kesi iliyofunguliwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong (SCB-HK) dhidi ya wamiliki wa IPTL kuwa haitakuwa na madhara juu ya uamuzi wa kuhamisha fedha hizo kutoka Escrow kwenda IPTL na kama ni mashitaka mapya atakayeshtakiwa ni IPTL wala siyo Serikali ya Tanzania.

MASWI NAYE
Werema akidaiwa kunogesha suala hilo kwa maandishi yaliyofanikisha uchotwaji wa mabilioni hayo, habari za ndani zinasema kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anadaiwa kushiriki kwa kumuandikia barua Gavana Ndulu, Oktoba 21, mwaka 2013, siku moja tu baada ya barua ya Jaji Werema kwa Dk. Likwelile inayomuelekeza kuruhusu uchotwaji wa fedha hizo.
Chanzo chetu kilisema kuwa barua ya Maswi ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘kuidhinisha kutolewa kwa fedha kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, akirejea barua ya Jaji Werema ambayo ilisisitiza umuhimu wa utolewaji wa fedha hizo haraka iwezekanavyo.
Katika barua hiyo, Maswi naye anadaiwa kuinakili kwa Sefue, Jaji Werema na Dk. Likwelile.
Katika barua hiyo, Maswi anadaiwa kukiri kupokea barua ya Jaji Werema yenye kumbukumbu namba AGC/E.80/6/65 ya Oktoba 2, 2013 iliyotumwa kwa Dk. Likwelile.
Maswi anadaiwa kujiegemeza kwenye barua ya Werema juu ya umuhimu wa kutekeleza maamuzi ya Mahakama Kuu bila ya kuchelewa, ikiwa ni pamoja na kumaliza ubishi juu ya fedha za akaunti ya Escrow.
Maswi anadaiwa kukumbushia kuwa serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na IPTL waliingia kwenye makubaliano ya Escrow Julai 5, 2006 kwa mujibu wa makubaliano ya kuuziana umeme (PPA) kwa ajili ya kuhifadhi kwa usalama kiasi cha fedha kilichokuwa kinabishaniwa chini ya PPA.
Pia anadaiwa kusema katika barua yake kwamba kwa mujibu wa kifungu 7.7 cha makubaliano ya Tegeta Escrow (Tegeta Escrow Agreement), wabishani kwenye makubaliano ya Escrow walikubaliana kimsingi kuhamisha fedha zote zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti ya Escrow, Dola za Marekani na Shilingi ya Tanzania na kuwapa IPTL.
Kwa msingi huo, chanzo chetu kimenukuu barua ya Maswi akimwelekeza Gavana Ndulu kama wakala wa akaunti ya Escrow kuhamisha fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na kuzipeleka IPTL kufuatana na makubaliano ya kuzipeleka fedha ITPL yaliyofikiwa kati ya Wizara ya Nishati na Madini na IPTL ya Oktoba 21, 2013.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), amelishauri Bunge kuongeza siku za kujadili taarifa maalumu ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusiana na kashfa ya kuchota Sh. bilioni 306 katika akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Alitoa ushauri huo jana wakati akiomba mwongozo wa Spika akisema kutokana na umuhimu wa taarifa hiyo kwa Bunge ili Watanzania wapate kujua ukweli.
“Mheshimiwa Naibu Spika, tuna uzoefu hata katika msiba anayelia sana ndiye aliyeua, hivyo tunahitaji muda zaidi wa kujadili taarifa hii, ambayo ni muhimu sana kutokana na kuwahusisha mawaziri na hata wabunge,” alisema Lusinde.
Alisema suala la Escrow limekuwa na ‘makandokando’ mengi, huku baadhi ya wabunge na hata mawaziri wakitajwa kuhusika.
”Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muongozo wako, sakata hili ni kubwa na wabunge tunataka kujadili kwa kina. Sasa mkitupa siku moja, ni sawa na kutupa dakika 10 au saba na wachangiaji wanaweza kuwa wawili au watatu na hata wabunge wengi kukosa nafasi na uwanja wa kujadili suala hili,” alisema Lusinde.
Alisema ratiba ya shughuli za sasa za Bunge inaonyesha kuwa PAC itawasilisha taarifa yake na kujadiliwa kwa siku moja.
Akijibu muongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema ni kweli jambo hilo linahitaji muda.
Hivyo, akasema amechukua ushauri huo na ataufikisha kwenye Kamati ya Uongozi wa Bunge kwa ajili ya maamuzi zaidi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: