Wakati Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, imeelezwa
kwamba nusu ya wabunge 239 wa kuchaguliwa waliopo sasa, watabwagwa
katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Hiyo inatokana na wabunge kutoa ahadi nyingi kwa wapigakura ambazo hawazitekelezi hivyo kukumbwa na rungu la wananchi mwakani.
Hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi
ya Twaweza ambayo yalitangazwa Dar es Salaam jana ambayo yanaonyesha
Watanzania wanane kati ya 10 wanawafahamu kwa majina na vyama wabunge
hao.
Akiwasilisha taarifa hiyo, mtafiti Elvis Mushi
alisema: “Walipoulizwa kama watampigia tena kura mbunge wao wa sasa,
karibu nusu ya Watanzania (asilimia 47) walisema hapana, asilimia 47
walisema ndiyo na asilimia tano walisema hawajui.
“Waliosema wasingempigia kura mbunge wao ni wale
walioripoti pia kuwa mbunge wao ama ametekeleza ahadi chache au
hajatekeleza ahadi yoyote aliyoitoa katika uchaguzi uliopita,” alisema
Mushi.
Aliongeza: “Wapigakura wanane kati ya 10 sawa na asilimia 79 wanakumbuka ahadi zilizotolewa na wabunge wao wakati wa kampeni.”
Mushi alisema ahadi nyingi zilikuwa zinahusu
ujenzi; kujenga au kukarabati barabara (asilimia 77), kujenga au
kuboresha vyanzo vya maji (asilimia 64), ujenzi wa hospitali asilimia 38
na ujenzi wa madarasa katika majimbo yao asilimia 23.
“Kwa bahati mbaya ni mwananchi mmoja tu kati ya
wanane, sawa na asilimia 12, aliyeripoti kuwa mbunge wake ametekeleza
ahadi zake zote.”
“Asilimia 54 ya wananchi walisema mbunge wao
alikuwa ametekeleza baadhi tu ya ahadi zake huku wananchi wanne kati ya
10 sawa na asilimia 38 wakiwa wamefuatilia wenyewe au jamaa zao ndani ya
jamii utekelezaji wa ahadi hizo za mbunge wao,” alisema Mushi.
Kuhusu elimu ya mbunge, Mushi alisema watu watatu
kati ya wanne sawa na asilimia 74 walisema wangeangalia kiwango cha
elimu ya mgombea.
“Nusu ya waliohojiwa wanatarajia mbunge awe na
angalau elimu ya shahada, umri wa mgombea na uaminifu wa mgombea,
mnyoofu, mkweli au mwadilifu. Kati ya wale waliotaja umri walifikiria
mbunge anapaswa kuwa na umri wa miaka 40 au zaidi ambao ni asilimia 55,”
alisema Mushi.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment