Social Icons

Pages

Thursday, November 13, 2014

BUNGE: HATUNA MPANGO KUWASHITAKI VIGOGO TPDC

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah
Mpango wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuwashitaki mahakamani Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Andilile na Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Michael Mwande, kwa kukaidi agizo lake umeshindikana.
Akizungumza na NIPASHE, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah (pichani), alisema Spika wa Bunge ana mamlaka ya kuamua namna ya kushughulikia suala hilo na kwamba halazimiki kufuata mapendekezo yaliyotolewa na PAC ya kuwafikisha mahakamani kwa kukaidi kuwasilisha nyaraka za mikataba 26 ya gesi kati ya serikali na wawekezaji.
Alisema baada ya PAC kuwasilisha barua ikielezea suala hilo na kuhitaji hatua zaidi kuchukuliwa na ofisi ya Spika, kinachoendelea sasa ni kuwezesha utekelezwaji wa agizo hilo kwa  kuwasilisha nyaraka hizo kwa PAC.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza kwa kina kuhusu njia na muda gani utatumika kukamilisha kazi hiyo, fahamu tu kwamba jambo hili linafanyiwa kazi kwa lengo la kupata kinachohitajika siyo kupelekana mahakamani,” alieleza Dk. Kashililah.
Mwande na Andilile walikamatwa na polisi kwa amri ya PAC iliyokutana kama mahakama kwenye ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, takribani wiki tatu zilizopita, baada ya kukaidi kuwasilisha nyaraka hizo.
Hata hivyo, waliachiwa huru bila masharti lolote, kwa kilichoelezwa kuwa taratibu hazikuzingatiwa kwa kuwa hapakuwa na hati iliyosainiwa na Spika wa Bunge.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: