Bunge limeridhia azimio
la kufuta na kusamehe madai au hasara itokanayo na upotevu wa fedha na
vifaa vya Serikali vya zaidi ya Sh10 bilioni za kipindi kilichoishia
Juni 30, 2011.
Katika fedha hizo, kiasi cha Sh4.9 bilioni
kilitokana na hasara ya kuharibika kwa dawa zilizoingizwa nchini kwa
ajili ya kurefusha maisha ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Hasara nyingine ni Sh4.9 bilioni iliyotokana na
kuungua kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, hivyo kufanya hasara kubwa
ya kiasi kilichoombwa kufutwa kutokana na mambo hayo mawili.
Fedha nyingine zilitokana na kupotea kwa vitabu
katika shule mbalimbali nchini, ambavyo vimeshindwa kurudishwa na
wanafunzi, kuharibika kwa gari moja aina ya Toyota Land Cruiser VX
kutokana na kuingia maji katika lita 6,000 za mafuta ya dizeli.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema
jana kuwa Bunge limefanya uamuzi sahihi kufuta fedha hizo kwenye vitabu
vya Serikali kwa kuwa hazilipiki.
“Asilimia 90 ya fedha zote tulizoomba zifutwe,
inatokana na dawa zilizokwisha muda pamoja na kuungua kwa ofisi ya mkuu
wa mkoa. Hii ni hasara ambayo ingeendelea kutuharibia vitabu,” alisema
Nchemba.
Alisema fedha hizo hazikufanyiwa wizi bali kilichotokea ni hasara baada ya mali mbalimbali za Serikali kuharibika.
Akihitimisha hoja hiyo, Waziri wa Fedha, Saada
Mkuya alisema Serikali itaangalia utaratibu mpya wa kuagiza dawa ili
kuondokana na adha ya kuharibika na kuiingizia hasara Serikali.
“Pia tutaweka bima kwa mali za Serikali kupitia Shirika la Bima la Taifa (NIC),” alisema.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI

No comments:
Post a Comment