Social Icons

Pages

Wednesday, August 13, 2014

SERIKALI: UCHUNGUZI WA EBOLA VIWANJANI, MIPAKANI

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid. Picha na Maktaba

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii, imeweka mikakati maalumu ya kuimarisha utambuzi juu ya ugonjwa wa ebola katika viwanja vya ndege na maeneo ya mipakani ili kuwabaini wasafiri wenye dalili za ugonjwa huo ulioshika kasi katika baadhi ya nchi za Afrika.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid, aliyasema hayo Dar es Saaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tahadhari iliyochukuliwa na Serikali ili kuudhibiti ugonjwa huo.

Alisema, wizara hiyo umeunda kamati ya dharura ambayo itakuwa inakutana kila wiki chini ya mawaziri mbalimbali ili kutathmini hali halisi ya ugonjwa huo na kupitia taarifa za Shirika la Afya Duniani.

Aliongeza kuwa, fomu maalumu zimeanza kutumika kwa wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), kuanzia Agosti 5 mwaka huu ili kuwatambua abiria wanaoingia nchini na nchi wanazotoka.

"Fomu hizi pia zitatumika katika maeneo yote ya mipakani, pia tumeunda kikosi kazi kinachohusisha wadau kutoka taasisi mbalimbali na wajumbe kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

"Kikosi hiki kimeandaa mpango wa dharura kukabiliana na ugonjwa huu kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya, mpango huu unaainisha namna ya kutambua na kuchukua sampuli, matibabu ya ugonjwa, mwongozo na kutenga sehemu maalumu na uelimishaji kwa umma," alisema.

Alisema ugonjwa huo husababishwa na virusi vya ebola ambavyo vipo katika kundi la familia ya 'filovirus', ambapo kuna aina tano za virusi hivyo ambavyo ni Bundibugyo, Cote D'lvoire, Reston, Sudai na Zaire.

Dkt. Rashid alisema vurusi aina ya Bungibugyo, Sudan na zaire huleta milipuko mikubwa kwa binadamu na kusababisha idadi kubwa ya vifo ikikadiriwa asilimia 25 hadi 90 ya waliopata maambukizo ya ugonjwa huo, hufariki dunia.

Aliongeza kuwa, hivi sasa katika nchi za Afrika Magharibi, kirusi aina ya Zaire kimethibitika kusababisha mlipuko huo ambapo kwa kawaida, virusi hivyo hubebwa na popo ambapo uambukizo wa kwanza kabla ya kueneo kwa binadamu huanzia kwa wanyama hususan nyani na sokwe.

Alisema binadamu hupata maambukizo ya ugonjwa huo kutoka kwa popo au kupitia wanyama ambao wameambukizwa au kufa ambao ni sokwe, nyani na swala wa porini ambapo uambukizo huo hutokea wakati wa shughuli za uwindaji.

"Binadamu anapopata maambukizo, uambukizo kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine huenea kwa kasi kwa kugusa damu au majimaji kutoka mwilini kwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu au kugusa maiti ya mtu aliyekufa kutokana na ebola.

"Hadi sasa, hakuna mgonjwa wa ebola aliyeweza kugundulika nchini, hivyo watu wasiwe na wasiwasi...Wizara imejipanga kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu," alisema.

Dkt. Rashid alisema ugonjwa huo hauna tiba maalumu wala chanjo, bali mgonjwa hutibiwa kutokana na dalili ambazo atakuwa nazo ambapo dalili zake ni homa kali, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kutokwa na vidonda kooni.

Dalili hizo humfanya mgonjwa atapike, kuharisha, kutokwa na vipele vya ngozi, figo pamoja na ini kushindwa kufanya kazi ambapo baadhi ya wagonjwa hutokwa na damu ndani na nje ya mwili na dalili hizo huonekana kati ya siku mbili hadi 21.

"Njia za kujikinga na ugonjwa huu ni kuepuka kugusa mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji yaliyotoka mwilini mwa mgonjwa, kuepuka na kushughulikia maiti ya mtu aliye na ugonjwa huu na mtu akihisi dalili aende kwenye kituo cha afya haraka," alisema.

Chanzo: MAJIRA

No comments: