Fumbo kuhusiana na mtu mwenye sifa za kuwa Waziri
Mkuu wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Magufuli limeanza
kufumbuliwa.
Hali hiyo inatokana na kile alichokidhihirisha Magufuli siku moja
baada ya kuapishwa kwake na pia baada ya hapo wakati alipochukua maamuzi
kadhaa ya vitendo, ikiwamo kutoa maelekezo muhimu yaliyodhihirisha aina
ya Waziri Mkuu atakayemteua.Kwa mujibu wa muundo wa serikali, Waziri
Mkuu ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, ambaye mbali ya
kuwa kinara wa mawaziri wengine, ndiye anayetakiwa pia kutoa maamuzi
mazito linapojitokeza jambo linalomlazimu kufanya hivyo.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa
na uongozi nchini wamesema hatua alizochukua Magufuli kuanzia siku ya
kwanza ya kuapishwa kwake zinatoa picha ya wazi aina ya watu atakaotaka
kuwa nao katika serikali yake.
Baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini
Dar es Salaam, Dk. Magufuli alianza kazi siku hiyo hiyo kwa kutoa hotuba
iliyosisitiza juu ya kauli mbiu yake ya ‘hapa kazi tu’ katika kutumikia
wananchi, kuwafariji waliokuwa wapinzani wake katika urais huku
akiwasihi waungane naye kuijenga Tanzania imara na pia alimteua
Mwanasheria Mkuu, George Masaju, huku pia akitangaza siku ya kuanza
Bunge kuwa ni Novemba 17.
“Ratiba yake katika siku ya kwanza aliyoapishwa ilikuwa ngumu
kutokana na wageni wengi waliomtembelea lakini bado hakutaka kuchelewa
katika kuteua Mwanasheria Mkuu. Na siku iliyofuata (Ijumaa) akaonyesha
yeye ni Rais wa aina gani kwa kufanya ziara ya ghafla kwenye Wizara ya
Fedha na kujionea aina ya watendaji waliopo. Yote haya yanatosha
kufichua sifa za mawaziri atakaowateua,” alisema John Jacob, mkazi wa
Magomeni jijini Dar es Salaam ambaye ni mmoja wa wafuatiliaji wa siasa.
“Hivi sasa siyo kazi tena kubashiri aina ya Waziri Mkuu
tutakayekuwa naye. Magufuli ameonyesha wazi kwamba yeye ni mchapakazi na
hivyo hawezi kukubali wababaishaji au kuchagua mtu kwa sababu yoyote
isiyohusiana na kazi,” alisema Latifa Abdallah, mfuatiliaji pia wa
masuala ya siasa mwenye maskani yake jijini Arusha.
DALILI YA SIFA MUHIMU ZA WAZIRI MKUU MPYA
Baada ya uteuzi wa Mwanasheria Mkuu alioufanya siku ya kuapishwa
kwake (Alhamisi), Magufuli alisubiri saa chache tu kabla ya kutembea kwa
miguu kutoka ofisini kwake hadi katika jingo la Wizara ya Fedha ambako
alifanya ziara ya kustukiza, akiingia kila ofisi kuona shughuli za
ujenzi wa taifa zinavyoendelea.
Huko, baada ya kukuta watendaji wake wakiwa hawapo ofisini huku
akipewa majibu kuwa wameenda kunywa chai, Magufuli alikuja juu na kutoa
maagizo muhimu juu ya dhana ya kuchapa kazi.
Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo, Magufuli anaonyesha kuwa Waziri
Mkuu wake atapaswa kuwa mtu wa vitendo zaidi na siyo maneno mengi.
Kadhalika, utoaji wa maamuzi kuanzia siku ya kwanza ni sifa muhimu
ya kile alichokuwa akikisisitiza wakati wa kampeni kuwa kamwe,
hatavumilia mawaziri wanaopenda majibu ya ‘tuko mbioni’, ‘tuko kwenye
mchakato’, ‘tuko kwenye hatua nzuri’ wala ‘tuko kwenye hatua za mwisho’.
Ni kazi tu.
Aidha, Magufuli ameonyesha vilevile kuwa Waziri Mkuu wake atakuwa
ni mtu wa kutoa maamuzi kwa kasi. Sifa hii inatokana na muda alioutumia
katika kutangaza jina la Mwanasheria Mkuu na pia siku ya kuanza kwa
Bunge la 11.
Tofauti na ilivyozoeleka, juzi Jumamosi haikuwa siku iliyopita
burebure kwa Magufuli. Alifanya kikao kizito na makatibu wakuu, naibu
makatibu wakuu, gavana wa Benki Kuu (BoT) na Kamishna wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA). Katika kikao hicho, Magufuli alitoa maelekezo
kadhaa yaliyofichua sifa nyingine muhimu atakazokuwa nazo Waziri Mkuu
wake na pia mawaziri wengine.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu kuhusiana na kile
kilichoijiri kwenye kikao hicho, ni kwamba Rais Magufuli aliagiza
kufutwa mara moja kwa safari za nje za mawaziri na viongozi wengine wa
juu serikalini na kwenye taasisi za umma.
Aliagiza kuwa masuala yote ya nje ya nchi yatekelezwe na mabalozi
waliopo huko na kwamba, kukiwa na ulazima, basi safari hizo ni lazima
ziidhinishwe na yeye (Rais) au Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu. Rais
Magufuli aliagiza kuwa anachotaka ni kuona viongozi wakifanya ziara
nyingi kwa wananchi vijijini na kuwatatulia kero zao.
Hii ni dalili nyingine ya wazi kuwa Waziri Mkuu ajaye hatakuwa mtu
wa kusafiri nje mara kwa mara na badala yake, atakuwa ni mtu wa kuwa
karibu na wananchi huku akisimamia shughuli za serikali kwa umakini
zaidi.
Agizo jingine muhimu alilotoa Magufuli ni kutaka kuona viongozi hao
wakiweka mikakati mbalimbali itakayoanza kutekelezwa mara moja ifikapo
Januari 2016, na mojawapo ya mikakati hiyo iwe ni ahadi yake ya kutoa
elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne. Aliagiza pia kuwapo kwa mikakati ya kuhakikisha kuwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu inatolewa bila shida.
Hii maana yake ni kuwa sifa mojawapo ya Waziri Mkuu itakuwa ni kuwa
mzuri katika kuandaa mikakati na kusimamia utekelezaji kwa umakini ili
kuleta matokeo chanya, tena kwa wakati.
Kadhalika, katika kikao hicho, Dk. Magufuli alisisitiza kuwa ni
lazima kila mtendaji wa serikali kuzingatia, kufuata sheria na taratibu
ili taifa lisonge mbele kimaendeleo na kwa ufanisi zaidi. Hii ni dalili
kuwa Waziri Mkuu wake na pia mawaziri wengine ni lazima wawe waumini
wazuri wa sheria na taratibu, na siyo watu wa kufanya kazi kwa mazoea.
Rais Magufuli alimuagiza Kamishna wa TRA kusimamia kwa umakini
ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kuwa kero ndogo ndogo kwa
wananchi zinatatuliwa kama alivyoahidi. Aliitaka TRA kuhakikisha inakusanya mapato hayo kutoka kwa
wafanyabiashara wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu
wala taasisi yoyote.
Hii ni ishara kuwa sifa nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu wa Magufuli
ni kufanya kazi kwa kujiamini, lengo likiwa ni kuongeza mapato ya
serikali na katika kutekeleza hili, anatakiwa kujiamini muda wote kwani
Rais atakuwa akimuunga mkono katika kila hatua na hakuna atakayefanya
ujanja ujanja kwa kutumia jina la ‘Rais Magufuli’.
Alisisitiza vilevile kuwa katika serikali yake, mtu wa kutoa
maamuzi vinginevyo zaidi ya hayo aliyowapa ni yeye (Rais), au Makamu wa
Rais. Umakini katika kuhakikisha kuwa serikali haipati hasara kutokana na
manunuzi yasiyozingatia sheria, au yenye harufu ya rushwa, ni eneo
jingine atakalopaswa kuwa nalo Waziri Mkuu mpya wa serikali ya awamu ya
tano.
Katika kikao hicho, Magufuli alisema suala la manunuzi limekuwa
likitumika vibaya na kuwa mwanya wa kuiibia serikali kwa watu kuongeza
bei ya vitu hata kama ni vya bei ndogo katika jamii. “Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja,”alisema.
Katika hili, ipo sifa nyingine anayotarajiwa kuwa nayo Waziri Mkuu
mpya, ambayo ni kuwa na jicho la ziada kuhakikisha kuwa serikali haipati
hasara kwa kuuziwa vitu kwa bei ya juu kuliko iliyopo sokoni.
UHODARI BUNGENI
Sifa nyingine muhimu kwa Waziri Mkuu ni kuwa mzoefu wa kukabili
changamoto za hoja moto za wapinzani bunegni kwani katika Bunge lijalo,
kambi ya upinzani itakuwa na wabunge 121. Kwa sababu hiyo, ni wazi
kwamba mtu atakayeteuliwa na Rais Magufuli kwa nafasi ya Waziri Mkuu ni
lazima atakuwa na sifa ya kukabiliana na maswali ya wabunge machachari
wa upinzani pale inapobidi, ikiwamo wakati wa maswali ya papo kwa papo.
Kwa ujumla, kama ilivyowahi kuripotiwa katika gazeti hili wiki
iliyopita, sifa muhimu za ujumla kwa Waziri Mkuu wa Magufuli zatarajiwa
kuwa uadilifu, kwa maana ni lazima awe mtu asiyekuwa na chembe ya
kashfa, hasa zinazohusiana na rushwa kama ilivyo kwa mwenyewe (Rais
Magufuli); Kujiamini kiasi cha kutoa maamuzi magumu na kwa wakati kwa
ajili ya maslahi ya taifa; kufanya kazi kwa pamoja na siyo kusaka
umaarufu binafsi kiasi cha kumpiku Rais; Uwezo wa kusimamia utekelezaji
wa mipango ya serikali; Kukubalika ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment