Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
Ofisi Ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam, imewataka
 wabunge wote wateule walioko majimboni kufika katika ofisi hizo 
Jumatano wiki hii kwa ajili ya kushiriki hafla ya kuapishwa kwa Rais 
Mteule itakayofanyika Novemba 5, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu
 Katibu wa Bunge, John Joel, alisema wabunge wateule watakaohudhuria 
hafla hiyo wanatakiwa kuja na vyeti vya kuteuliwa walivyopewa na 
Wasimamizi wa Uchaguzi.
“Kila Mbunge mtarajiwa, atatakiwa kuwasilisha cheti kwa Maofisa wa 
Bunge wakati wa mchakato wa usajili  na kitambulisho kingine chochote 
kinachotolewa na mamlaka inayotambulika na kinachomtambulisha jina lake 
kamili kama linavyoonekana kwenye cheti cha uteuzi wa ubunge,” 
alisisitiza.
Aidha, alisema mchakato wa usajili wa wabunge wateule utafanyika 
katika viwanja  vya Bunge la 11 na kuongeza wabunge hao watajitegemea 
usafiri wa kuelekea bungeni.
Joel alisema mkutano huo utaanza siku ambayo Rais Mteule atakapoitisha Bunge.
Alisema siku hiyo shughuli mbalimbali zitafanyika zikiwamo za 
uchaguzi na kiapo kwa Spika, viapo vya wabunge, uthibitisho wa jina la 
Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika na ufunguzi rasmi wa Bunge la 11.
Alivikumbusha vyama  vya siasa vyenye usajili wa kudumu vinavyotaka
 kusimamisha mgombea wa nafasi ya Spika vianze mchakato wa kupata 
mgombea katika ngazi ya vyama baada ya tangazo kutolewa na kuwasilisha 
jina lake kwa Katibu wa Bunge.
Alivisistiza vyama kuzingatia kuwa mgombea wa nafasi hiyo anaweza 
kuwa mbunge au mwanachama yeyote wa chama hicho kwa masharti kwamba siyo
 mbunge mteule.
Hali kadhalika, alisema vyama vya siasa vinatakiwa kuwasilisha jina
 la mgombea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) siku tano kabla ya uchaguzi 
kujiridhisha kwamba mgombea ana sifa za kuwa mbunge.
     CHANZO:
     NIPASHE
    
 

No comments:
Post a Comment