
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa chama hicho, Anthony Komu.
Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro limemshikilia na
kumhoji kwa zaidi ya saa tano mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Vijijini
kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa chama hicho, Anthony Komu,
kwa madai ya kumtisha kwa bastola Katibu wa chama hicho mkoani hapa,
Basil Lema.
Hata hivyo, baada ya kuhojiwa jeshi hilo lilimwachia huru Komu na
kisha kulifuta jalada la uchunguzi lililofunguliwa dhidi yake baada ya
mlalamikaji (Lema) kuomba shauri hilo limalizwe katika meza ya
usuluhishi ndani ya Chadema.
Akizungumza na Nipashe jana nje ya Kituo Kikuu cha Polisi Moshi,
Komu alisema alishikiliwa na kuhojiwa kuanzia saa 5:00 asubuhi na
kuachiwa saa 10:00 jioni. “Niliwaeleza kwamba sijawahi kumiliki silaha na sina mpango wa
kuimiliki wakaridhika na maelezo yangu na wakakubali mzozo uliotufikisha
hapo tukaumalize nje ya vyombo vya sheria,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimanjaro, Fulgence
Ngonyani, alithibitisha kwamba mgombea huyo wa ubunge Jimbo la Moshi
Vijijini kupitia Chadema alikuwa alitumiwa ujumbe wa kuitwa polisi kwa
ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma hiyo.
Agosti 18, mwaka huu wakati wa marudio ya uchaguzi wa kura ya maoni
za Chadema katika jimbo hilo, Komu akiwa katika eneo la Kibosho, Moshi
Vijijini alidaiwa kumtisha kwa bastola katibu huyo wa mkoa alipomfuata
akitaka kujua taratibu zilizotumika kuhamisha mkutano wa uchaguzi huo
ambao ulipangwa kufanyika katika eneo la Garden, kata ya Kiboroloni,
Manispaa ya Moshi.
Naye Lema akizungumzia suala hilo alisema: “Ni kweli tumemalizana
na bosi wangu (Komu) baada ya kuafikiana wenyewe na kuomba polisi
ikubali mambo haya yamalizwe nje ya vyombo vya kisheria kutokana na
maslahi mapana ya Chadema.”
Lema alitoa taarifa polisi kuhusu Komu wiki tatu zilizopita na
kupewa hati yenye namba MOS/RB/829/2015 akilalamikia kupigwa na
kutishwa kwa silaha baada ya kupewa maelekezo na Kaimu Katibu Mkuu wa
Chadema (Salum Mwalimu) kufuatilia mgogoro uliotokana na mkutano mkuu
maalum wa marudio ya uchaguzi wa kura ya maoni ambao awali ulikuwa
umempa ushindi Lucy Owenya.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment