Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi,
akikata utepe kwenye kitabu wakati akifungua maonyesho ya 18 ya
kimataifa ya biashara ya bidhaa za teknolojia za magari, mafuta na gesi
jijini Dar es Salaam jana. Wengine ni Meneja wa Operesheni Expogroup,
Pius Gechamet (katikati) na Meneja wa Maonyesho hayo kwa upande wa
Afrika, Neville Trindade (wa pili kulia).Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi,
amesema Tanzania inapaswa kujenga viwanda vingi vya bidhaa kama vile
vifaa vya magari na teknolojia nyingine na siyo kuwa soko na mwagizaji
pekee wa bidhaa kutoka nje.
Dk. Mengi alitoa wito huo wakati akifungua maonyesho ya 18 ya
kimataifa ya biashara ya bidhaa za teknolojia za magari, mafuta na gesi
jijini Dar es Salaam jana. “Mimi binafsi naona haya maonyesho yamefana...tukitumia fursa kama
hii, tukabadilisha sura ya viwanda. Wengi wao wamesema wapo tayari
kutengeneza bidhaa hapa hapa nchini na kuziuza hapa hapa,” alisema Dk.
Mengi na kuongeza:
“Siyo kuja kuangalia vitu tu, bali kujenga uhusiano mzuri ili ifike
mahali sisi tuingie mikataba ya ubia wa kutengeneza vitu hivi hapa
hapa. Katika ubia tutafaidika katika teknolojia na uzoefu. “
Kwa mujibu wa Dk. Mengi, maonyesho hayo yatakuwa na manufaa kwa
Tanzania iwapo kutakuwapo maelewano mazuri ya kujenga viwanda kwa ajili
ya kutengeneza bidhaa hizo nchini.
“Tanzania inahitaji teknolojia ya viwanda. Nchi yetu isiwe soko tu
la bidhaa za nje au mwagizaji tu, bali ifike mahali tuvitengeneze hapa
nchini, “ alisisitiza Dk. Mengi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Simba Trailers, Hussein
Dewji, alitoa wito kwa Watanzania kuwa na utamaduni wa kupenda na
kununua bidhaa zinazotengenezwa nchini badala ya kuagiza kutoka nje.
Meneja wa Maonyesho hayo kwa upande wa Afrika, Neville Trindade,
alisema kuwa jumla ya kampuni 80 kutoka nchi 22 za ndani na nje ya
Afrika, Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo zilishiriki.
Maonyesho hayo yanayotarajiwa kumalizika kesho Jumamosi, hufanyika mara moja kwa mwaka.
CHANZO:
NIPASHE

No comments:
Post a Comment